Sunday, October 1

Kutana na wanawake Singida waliozaa zaidi ya watoto kumi bila kufika hospitali



Kama waendesha kampeni ya “uzazi wa mpango” wanadhani wamekaribia kufanikiwa, bado wana safari ndefu.
Na Kata ya Kinyeto mkoani Singida inaweza kuwapa picha halisi; wanaume wanataka wazae watoto wengi ili kizazi kipanuke, baadhi ya wanawake wanataka wazae hadi mayai yaishe ili kujaza nyumba.
Lakini wengi wao hawaendi kliniki, hawatumii dawa za kinga na wanajifungulia nyumbani ama kwa mazoea au kutokana na zahanati kuwa mbali.
Katika umri wa miaka 45, Amina Musa, mkazi wa kitongoji cha Msaghaa kilichopo kijiji cha Kinyeto wilayani humo tayari ameshazaa watoto 12, wa mwisho akiwa na umri wa miaka mitatu ikiwa ni wastani wa mtoto mmoja kila baada ya miaka miwili kuanzia akiwa na umri wa miaka 20.
Amina ambaye anafanya kibarua cha kumwagilia katika shamba la mbogamboga, anasema mumewe aliondoka miaka miwili iliyopita bila kuaga na sasa katika boma lake amebaki na watoto 12 wanaomtegemea.
“Tulikuwa na shamba dogo kwa ajili ya chakula. Kutokana na ukame tulishindwa kuvuna chochote,” anasema katika mahojiano na Mwananchi.
Huku machozi yakimlenga, Amina anasema, “mume wangu alianza kufanya vibarua mashambani hivyo kila alicholipwa kiliishia kwenye chakula na bado watoto walipata mlo mmoja kwa siku, akaamua kuondoka.”
Amina ni miongoni mwa wanawake 11 wa Kata ya Kinyeto ambao walipeleka malalamiko yao ofisi za serikali ya kijiji, kuripoti kutelekezwa na waume zao baada ya kushindwa kumudu kutunza familia kubwa.
Mtendaji wa Kijiji cha Kinyeto, Alute Alute anasema imekuwa ni kawaida ofisi yake kupokea kesi za aina hiyo.
“Wanapokuja hapa tayari ni kwamba tatizo limekuwa limetokea, hivyo tunafanya utaratibu wa kuwatafuta wahusika,” anasema Alute.
“Kwa bahati, wengi wakifanikiwa huko waendako huanza kutuma chochote nyumbani, lakini asilimia kubwa yao huondoka moja kwa moja.”
Kwa mujibu wa ofisa mtendaji wa Kinyeto, Romana Haule, wanaume hao hupata watoto wengi kwa kisingizio cha kutaka mayai yao ya kizazi yaishe.
“Siku zote lugha yao ni moja kwamba anataka azae mayai yake yaishe,” anasema Haule.
“Mume mmoja anaoa wake watatu hawa wote wazae watoto 10 kila mmoja, atawalea vipi?”
Anasema kwa mila na desturi za Kinyaturu, mwanamume anayepata watoto wachache anaamini kuwa kizazi chake hakipanuki.
Romana anasema viongozi wa kata wamejitahidi kwa kadri ya uwezo wao kuhakikisha wanatoa elimu ya uzazi wa mpango, lakini wanawake hawapo tayari kuzungumzia matatizo yao kwa viongozi ili kupata msaada.
“Katika kata yangu, mwanamke akikoma kuzaa au akikataa ni talaka au mwanaume huoa mke mwingine,” anasema Romana.
“Kuna mwingine ana watoto 12 ambaye mumewe hukataa kuhudhuria kliniki. Huwa tunamtafuta na anaingia kinguvu. Lazima sheria itumike ili twende sawa,” anasema Romana.
Wenye watoto wengi
Kati ya wanawake wanane niliobahatika kukutanao nao, watano walijifungua kwa njia ya kawaida wakisaidiwa na wakunga wa jadi, huku wawili wakijifungua nyumbani kwa msaada wa waume zao.
Tatu Ilangi, mkazi wa Kijiji cha Minyaa ambaye pia katika umri wa miaka 45 ameshapata watoto 13, ni mmoja wa wanawake wasio na utamaduni wa kufika zahanati kwa kuwa iko umbali wa zaidi ya kilomita nane kutoka anapoishi.
Mwajuma Soa, mwenye umri wa miaka 39, tayari ana watoto 10 na kati yao tisa amejifungulia nyumbani kwa msaada wa mumewe na mama mkwe. Mmoja wa mwisho alijifungua mchana akiwa peke yake nyumbani.
Hata hivyo, Mwajuma anayeishi kijiji kimoja na Tatu, anasema watoto kwake wametosha. Lakini tatizo ni atawezaje kufanikisha hilo bila ya kutumia njia za uzazi wa mpango.
“Nikipata mimba nyingine, itabidi nizae. Sisi tumechagua kwamba hatutumii njia hizo (hata kama) hatujui kama kuna madhara au la,” anasema.
“Tumeamua kuwa na watoto wengi na tulishakataa kushawishiwa kwamba tuache kuzaa.”
Serikali inafanya nini?
Mganga mfawidhi wa Zahanati ya Kinyeto, Dk Joyce Temu anasema tatizo kubwa ni wanawake kushindwa kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito mpaka kujifungua.
“Kiwango cha kawaida cha kuzaa ni watoto wanne,” anasema Dk Temu.
Anasema pamoja na kwamba aina hiyo ya uzazi wa watoto wengi inaweza kuwa salama kwao, kujifungulia kituoni kungewaweka salama zaidi. Mganga Mkuu wa Wilaya ya Singida, Sungwa Kabissi anasema mila na desturi hizo zinatokana na wengi kutoelewa masuala ya uzazi salama.
Akitoa takwimu za kata hiyo, mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto Wilaya ya Singida, Juliana Ndosi anasema wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 20 ndiyo wanaoongoza kujifungulia nyumbani ikilinganishwa na wale walio chini ya umri huo.
“Takwimu za miaka mitano iliyopita kati ya mwaka 2013 mpaka 2017, inaonyesha wazazi waliojifungulia nyumbani walikuwa 1,027, kwa wakunga wa jadi 1,513, njiani walikuwa 803 na wale waliojifungua katika vituo vya afya walikuwa 12,710,” anasema.

No comments:

Post a Comment