Na Bashir Yakub -
1.LESENI YA MAKAZI NININI.
Leseni ya makazi ni leseni/kibali maalum kinachotolewa kwa mmiliki wa makazi ili kutambua na kurasimisha makazi hayo.
Leseni ya makazi ni nyaraka ya umiliki wa makazi kama ilivyo nyaraka nyingine za umiliki wa ardhi. Leseni ya makazi ni kwa ajili ya ardhi makazi tu na si ardhi nyingineyo.
2. JE LESENI ZA MAKAZI ZINATAMBULIWA NA SHERIA.
Ndio, leseni za makazi ni kwa mujibu wa sheria namba 4/1999 Sheria ya Ardhi. Leseni za makazi zinatambuliwa na kifungu cha 23 cha sheria hiyo.
Kwahiyo wanaodhani kuwa leseni za makazi ni mpango tu wa serikali za mitaa na watendaji wa kata wajue sio kweli. Leseni za makazi ni nyaraka iliyo kisheria kwa mujibu wa kifungu hicho japo juu.
3. TOFAUTI YA LESENI YA MAKAZI NA HATI .
Hati ni “Right Of Occupancy” kwa jina la kitaalam, wakati leseni ya makazi ni “Derivative Right” . Tofauti za viwili hivi ni nyingi ila kubwa ya kukufanya uelewe ni kuwa, leseni ya makazi hutolewa kwa makazi ya mjini ambayo hayajapimwa na hayakuwa rasmi lakini yasiyo hatarishi.
Wakati hati hutolewa katika makazi rasmi na ambayo yamepimwa. Isipokuwa la kuzingatia ni kuwa iwe leseni ya makazi ama hati vyote vinatambuliwa na serikali kama nyaraka rasmi za umiliki na kila moja ina haki sawa na nyingine katika umiliki.
4. NANI HUTOA LESENI ZA MAKAZI.
Leseni za makazi hutolewa na manispaa husika. Iwe kubadili jina au kupata mpya ni kazi inayofanywa na manispaa ya yalipo makazi husika. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 23( 3) Sheria ya Ardhi.
5. MASHARTI YA KUPATA LESENI YA MAKAZI.
Kwanza, muombaji awe Mtanzania aliyefikisha umri wa miaka 18 au zaidi. Pili, awe ndiye mmiliki wa makazi husika. Tatu, eneo lisiwe katika maeneo hatarishi au maeneo ya hifadhi. Nne, eneo liwe maeneo ya mjini. Tano, yawe ni makazi kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu. Sita, lisiwe eneo ambalo lina hati ya kawaida au hati ya kimila. Saba, malipo ya ada na tozo nyingine zitalipwa kwa mujibu wa kifungu cha 23 (3)( c ).
6. FOMU INAYOJAZWA NA MUOMBAJI.
Muomba leseni ya makazi anatakiwa kujaza fomu namba 73 kwa mujibu wa kifungu cha 170 Sheria namba 4 ya ardhi. Kwenye fomu hiyo jina la mwombaji litahitajika, anuani yake na ya makazi, aina ya umiliki anaoomba kama ni binafsi, kundi, familia, kampuni, taasisi nk, taarifa za mtaa, kata, wilaya, taarifa za matumizi ya ardhi kwa sasa, matumizi mapya yanayoombewa leseni, ukubwa wa eneo husika, kutakuwa na sehemu ya maoni na mapendekezo ya mwenyekiti serikali ya mtaa, sahihi yako, dole gumba na picha zako.
Fomu hii inapatikana kwa wanasheria, au manispaa, au hata ofisi nyingine za kata wanazo.
7. MUDA WA LESENI YA MAKAZI.
Kifungu cha 23 (3) ( b ) kinasema kuwa leseni ya makazi itatolewa kwa muda ambao sio chini ya miezi sita lakini sio zaidi ya miaka 5. Kwahiyo muda wowote utakaopewa kati ya muda huo utatakiwa uhuishe ( renew) baada ya kuisha kwake.
Maana yake, ukipewa miaka 2 basi ikiisha huisha(renew). Halikadhalika miaka 3, 4 5, 1,miezi 6 ,8, 10 nk.
Kwa ufupi haya yatakufaa.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI KILA JUMANNE. 0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment