Mjumbe wa Korea Kaskazini amesema kuwa silaha za kinyuklia za taifa hilo haziwezi kujadiliwa.
Choe Son Hui amesema kuwa Marekani inafaa kujiandaa kuishi na Korea Kaskazini yenye silaha za kinyuklia.
Amesema kuwa ndio njia pekee ya kuwa na amani ya kudumu kati rasi ya Korea.
Mkurugenzi wa shirika la kijasusi nchini Marekani Mike Pompeo awali alikuwa ameonya kwamba Korea Kaskazini inaweza kuishambulia Marekani na kombora la kinyuklia katika kipindi cha miezi michache ijayo.
Korea Kaskazini imesema kuwa tayari ina uwezo huo.
Bwana Pompeo amesisitiza kuwa Washington bado inataka kutatua swala hilo kidiplomasia na vikwazo lakini ikasema inaweza kulazimika kutumia nguvu.
Akizungumza katika kongamano la kuzuia kuenea kwa silaha za kinyuklia mjini Moscow, bi Choe alisisitiza matamshi yaliotolewa awali na maafisa wa Korea Kaskazini kwamba silaha za kinyuklia ni swala la ''maisha na kifo'' kwa taifa hilo.
Mapema mwaka huu, aliripotiwa akisema kuwa taifa hilo liko tayari kufanya majadiliano na Marekani iwapo mazingira yataruhusu.
Lakini siku ya Ijumaa bi Choe alisema kuwa Korea Kaskazini itaangazia utekelezwaji wa maamuzi ya vikwazo vya Umoja wa mataifa akivitaja kuwa ni hatua ya uchokozi na vita.
Tangu Korea Kaskazini ilipoanza kufanyia majaribio makombora yake mwaka huu, vikwazo dhidi ya taifa hilo vimeongezeka.
Serikali ya Australia ilisema siku ya Ijumaa kwamba ilipokea barua kutoka Korea Kaskazini ambayo pia ilikuwa imetumwa kwa mataifa mengine ikiitaka Australia kutoshirikiana na Marekani.
Siku ya Alhamisi bwana Pompeo alionya kuwa makombora ya Pyongyang yalikuwa yanapiga hatua kwa kasi hivyobasi kuwa vigumu kwa majasusi wa Marekani kuwa na hakika kuhusu ufanisi wake, lakini akasema watagundua hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment