IDADI ya watu wanaofika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kupata matibabu ya ugonjwa wa homa ya ini imeongezeka mara nne zaidi ya idadi ambayo ilikusudiwa hali ambayo inafanya kitengo hicho kuelemewa.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ini na Mfumo wa Chakula wa Muhimbili, John Rwegasha, alisema ongezeko hilo limetokana na mwitikio mkubwa wa wananchi kujitokeza kupima mapema ili kujua iwapo wanasumbuliwa na ugonjwa huo au la.
“Muhimbili tulianza mradi wa upimaji na uchunguzi dhidi ya ugonjwa huo kwa kushirikiana na Taasisi ya ‘Centre for Disease Control’ ya nchini Marekani mwaka 2016, dhumuni lilikuwa kuwatafuta wagonjwa wa ini ambao hawakuwa wanapata tiba.
“Wenzetu kutoka Marekani walitusaidia kufanya uchunguzi na kuwapatia dawa iitwayo Tenofovr, gharama yake ilikuwa kubwa na wagonjwa wengi walishindwa kumudu,” alisema.
Alisema pindi walipoanza mradi huo walikusudia kupata wagonjwa 40 lakini kwa wastani walikuwa wakipata wagonjwa 160 ambayo ni mara nne ya wale waliokusudiwa.
“Katika kipindi cha miezi sita tulitarajia tutakuwa tumeona wagonjwa 440, lakini kwa kuwa imeongezeka mara nne maana yake imefikia wagonjwa 950 na bado kuna kipindi cha mwezi wa kumi na mbili ambapo bado hatujaona wagonjwa.
“Itakapofika kipindi hicho, ikiwa idadi itaendelea kuongezeka maana yake tutakuwa na wagonjwa 1,800 idadi ambayo ni kubwa, hii ni changamoto,” alisema.
Alisema changamoto nyingine ambayo inawakabili ni baadhi ya wagonjwa ambao wameingizwa kwenye mfumo wa matibabu kushindwa kurejea hospitalini hapo kwa awamu nyingine.
“Kati ya hao 950 ambao wamesajiliwa, wagonjwa 500 tumewaingiza kwenye mfumo wa matibabu lakini kati ya hao asilimia 45 wanashindwa kurejea tena kwa awamu nyingine kwa ajili ya matibabu,” alibainisha na kuongeza:
“Kwa hiyo tunakusudia kuwasilisha haya kwa Wizara ili itusaidie tuweze kuwafikia wagonjwa ambao wanashindwa kuendelea na tiba.
No comments:
Post a Comment