Ukivalia viatu vyako bila soksi unajiweka katika hatari ya makubwa zaidi kuliko kunuka kwa miguu pekee.
Chuo cha tiba ya miguu nchini Uingereza kinasema karibuni kumekuwa na ongezeko la maambukizi ya maradhi yanayosababishwa na kuvu kutokana na kuvuma kwa mtindo wa kuvalia viatu bila soksi, hasa miongoni mwa vijana.
Mtaalamu Emma Stephenson anasema amekuwa akipokea wanaume wa kati ya miaka 18-25 walio na matatizo kwenye miguu yao ambayo yametokana na kutovalia soksi au kuvalia viatu visivyowatosha vyema.
Kutovalia soksi siku hivi kumekuwa mtindo maarufu wa mavazi, na mwanamuziki Sam Smith ni miongoni mwa watu wanaojitokeza hadharani wakiwa na viatu bila soksi.
Wanaume wengi katika maonesho ya mitindo pia mara nyingi huonesha mavazi wakiwa na viatu bila soksi.
Mwanamuziki Tinie Tempah amejishindia tuzo nyingi kwa sababu ya mitindo na mara nyingi katika maonesho ya mitindo ya Londo huketi viti vya mbele.
Yeye pia huwa mara nyingi havai soksi - lakini anafahamu madhara yake?
"Miguu ya binadamu kwa kawaida hutoa nusu painti (ambayo ni sawa na lita 0.28) ya jasho kila siku," Emma Stephenson anasema.
"Unyevu mwingi na joto unaweza kusababisha maambukizi ya maradhi yanayotokana na kuvu mfano ugonjwa unaosababisha mwasho na kuchubuka kwa ngozi (kwa Kiingereza athlete's foot)."
Kwa mujibu wa Emma, madhara yake yanaweza kuwa mabaya.
"Moja ya visa vibaya nilivyowahi kukumbana navyo ni cha mwanamume mmoja wa miaka 19 aliyefanya kazi ya kuosha magari. Miguu yake ilikuwa inatokwa na jasho sana na ilikuwa imechubuka sana."
Lakini bila shaka itachukua ujasiri kumwambia bingwa wa UFC Conor McGregor kwamba anaweza kupata matatizo kutokana na mtindo wake wa kuvalia viatu.
Emma anashauri kwamba siri ni kutozidisha, iwapo bado utataka kutovalia soksi.
Jaribu usivae viatu bila soksi kwa muda mrefu.
Jaribu pia kuweka kitu cha kukausha jasho kwenye soli ya kiatu chako kabla ya kukivalia bila soksi.
Kadhalika, kuwa makini kuchunguza miguu yako. Ukigundua unaumwa pahali tafuta usaidizi upesi.
No comments:
Post a Comment