Wakijadili masuala mbalimbali yanayoikabili kata hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, wazee hao walidai mzigo wa kulima umebaki kwao huku vijana wengi wakijihusisha na usafirishaji wa abiria bila kwenda shambani.
Mmoja wa wazee hao, Fransisca Rutashoborwa alidai kuwa wanalazimika kulinda mazao shambani ili kudhibiti wizi unaofanywa na baadhi ya vijana waliokwepa kilimo na kukimbilia bodaboda.
Rutashoborwa aliiomba Serikali ya kijiji kuingilia kati suala hilo kwa kuwa kutokana na umri wao hawana uwezo wa kulinda mazao shambani huku wakipambana na vijana wanaoweza kuwatishia hata usiku.
Mzee Anatory Rutanjunwa kutoka Kijiji cha Katorelwa aliwalaumu wazazi kwa kutowafundisha watoto wao njia bora za maisha, ikiwamo shughuli za kilimo hali inayosababisha wakikua wakimbilie mjini.
Hata hivyo, Brighton Tibangayuka kutoka Kijiji cha Luhano alionekana kutofautiana na wenzake kwa kuwatetea vijana akisema biashara ya boda boda imekuwa mkombozi kwa kundi hilo kutokana na kujiingizia kipato cha kumudu maisha tofauti na awali walipokuwa wakishinda viijiweni.
“Tunachopaswa kufanya ni kuwaelekeza ili watumie sehemu ya kipato chao kugharamia shughuli za shamba; tusianze kuwashutumu kwa sababu kazi hii inawaingizia kipato,” alisema Mzee Tibangayuka.
Mmoja wa vijana wanaooendesha bodaboda, Johnson Rweikiza alikiri baadhi yao kutozingatia suala la kilimo kwa fikra kwamba kazi hiyo inastahili kufanywa na wazee vijijini, jambo alilosema limechangia kuwapo kwa upungufu wa chakula tofauti na kipindi cha nyuma.
Akizungumzia mkutano huo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Katano, Anafrida Kimela alisema lengo la kukutana kwao ni kujadili na kuweka misingi itakayowawezesha vijana kushiriki shughuli za maendeleo, hasa kilimo cha mazao ya chakula na biashara.
No comments:
Post a Comment