Wednesday, October 18

Barclays imetenga Sh 157milion kwa ajili ya wanafunzi


Dar es Salaam. Kuongeza ufadhili, Benki ya Barclays Tanzania imetenga Sh157 milioni kwa ajili ya masomo ya wanafunzi 23 wenye mahitaji maalumu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika mwaka wa masomo unaoanza 2017.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo itakayowanufaisha wanafunzi 23 ambaye kila mmoja atapata Sh6.8 milioni, mwenyekiti wa bodi ya benki hiyo, Simon Mponji amesema fedha hizo zinahusisha ada, malazi na matumizi binafsi kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na chuo.
"Asilimia 50 itatoka wakiwa mwaka wa kwanza, asilimia 25 watakapokuwa mwaka wa pili na asilimia 25 inayobaki itatoka mwaka wa tatu. Asilimia 60 ya wanufaika ni wanawake," amesema Mponji.
"Taasisi nyingi zinahitaji watu wenye. Tuliowajengea uwezo tumewatafutia taasisi ambazo wanaweza kufanya kazi kwa kujitolea kwa muda," amesema Mponji.
Akitaja sifa za kupata ufadhili huo, mkurugenzi wa bodi ya wahitimu UDSM, Dk Lulu Kaaya alisema muombaji ni lazima awe anatoka familia duni au yatima ambaye amechaguliwa kujiunga na chuo hicho na akakosa mkopo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).
"Kozi zitakazopewa kipaumbele ni rasilimaliwatu, mawasiliano na uhusiano wa umma na usimamizi wa biashara," amesema Kaaya.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Taknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amezitaka kampuni nyingine kuiiga benki hiyo kuisaidia serikali kuendeleza wanafunzi wenye uhitaji.
"Serikali imeongeza fedha za mikopo ya wanafunzi hadi Sh487 bilioni lakini hazitoshi, uhitaji ni mkubwa," amesema Ndalichako.
Amesema ufadhili huo ni mkubwa na anaamini utazidi kuongezeka kila mwaka huku serikali ikiendelea kuzihamasisha taasisi na nchi rafiki kutoa ufadhili kwa wanafunzi.
"Tunaishukuru serikali ya Hungary kwa kutoa msaada kwa wanafunzi 30 kila mwaka hii inamaanisha kuwa ndani ya miaka 3 wanafunzi wetu 90 watakiwa wamenufaika na ufadhili huo," amesema Ndalichako

No comments:

Post a Comment