Tuesday, October 3

Asilimia 70 ya wabunge wanatumia dawa za kufubaza makali ya virusi


Harahe, Zimbabwe. Mbunge mmoja amesema kwamba zaidi ya asilimia 70 ya wabunge wa Zimbabwe wanaishi na virusi vya ukimwi na wanatumia dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo (ARV).
Madai hayo yametolewa na mbunge mwakilishi wa Jimbo la Matabeleland Kusini, Priscilla Misihairabwi-Mushonga (MDC) ambaye aliwatupia lawama wenzake kwa kujipendelea kwamba wanaunga mkono Sheria ya Kodi ya Ukimwi kwa ajili yao ili wahudumiwe na serikali huku wakiwaacha bila msaada watoto walioathirika baada ya kuzaliwa kutokana na ngono isiyo salama.
Mwanamama huyo alisema hayo ndani ya Bunge la Taifa wiki iliyopita alipowasilisha hoja akitaka Wizara ya Huduma za Umma, Kazi na Huduma za Jamii kutoa ripoti ya serikali kulaani dhuluma ya kingono inayofanyika kwa kizingizio cha “kufanya biashara ya ngono”.
Hata hivyo, mbunge huyo hakueleza namna alivyopata takwimu hizo.
"Mnajua namna sisi binadamu tulivyo wabinafsi, virusi vya Ukimwi na Ukimwi ulipofika hadi kwetu, watu walipoanza kufa, haraka sana tulibuni Mfuko wa Ukimwi uliotuwezesha kwenda kununua dawa kwa sababu tunatka kuishi. Asilimia 76 ya watu waliokaa ndani ya Jengo hilo wanaishi na virusi vya ukimwi na Ukimwi na wanatumia ARVs," alisema Misihairabwi-Mushonga huku akizomewa na wenzake.
"Ndiyo, ni ukweli mtupu. Bado hamthubutu kuweka kiasi kidogo cha fedha ili kitumike kwa ajili ya matunzo ya watoto hawa. Haya sisemi kwa wabunge wengine pekee bali najisema na mimi pia, kwa sababu si haki kwamba naingia humu nakaa wakati kuna mtoto mwenye umri wa miaka minane au tisa na anabakwa kila siku na kudhulumiwa, ni vibaya sana Mheshimiwa Spika.”
Siku za nyuma wabunge walikuwa wakijitolea kutoa ushauri na kupima virusi vya ukimwi kama sehemu ya kuongoza kwa mfano, lakini hakuna hata mmoja aliyewahi kuweka wazi majibu.

No comments:

Post a Comment