Thursday, October 12

Aga Khan aondoka nchini



Dar es Salaam. Kiongozi wa madhehebu ya Ismailia duniani, Aga Khan ameondoka nchini leo Alhamisi saa 7:25 mchana baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku mbili kwa mwaliko Rais John Magufuli.
Kiongozi huyo ameagwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) na jumuiya ya ismailia hapa nchini pamoja na viongozi wa Serikali ambao ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Kikundi cha ngoma kilitoa burudani kwa kiongozi huyo kabla hajapanda ndege yake aina ya LX - PAK na kuanza safari.
Aga Khan aliwasili nchini jana Jumatano saa 4 asubuhi akitokea Uganda alikokwenda kuhudhuria sherehe za uhuru wa nchi hiyo kwa mwaliko wa Rais Yoweri Museveni.
Akiwa hapa nchini, Aga Khan alikutana na Rais Magufuli na kuzungumzia mambo matatu ambayo ni afya, elimu na vyombo vya habari.
Katika mazungumzo yao, Aga Khan aliahidi kushirikiana na Serikali katika kutoa huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na mkakati wa taasisi zake kupanua Hospitali ya Aga Khan na kujenga Chuo Kikuu cha Aga Khan huko Arusha ambacho kitakuwa kikubwa.
Aga Khan ndiyo mwasisi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) ambao unatoa huduma mbalimbali nchini na sehemu nyingine duniani katika sekta za afya, elimu, kilimo, fedha na bima.

No comments:

Post a Comment