Saturday, October 28

Afya ya Lissu yazidi kuimarika


Dar es Salaam. Kaka wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Alute Mughwai amesema mdogo wake anaendelea na mazoezi na afya yake inaimarika siku hadi siku.
Lissu anayeendelea na matatibu hospitali ya Nairobi nchini Kenya anakoendelea na matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa katika makazi yake Area D mjini Dodoma Septemba 7 na hadi sasa amefanyiwa upasuaji mara 17.
Akizungumza na Mwananchi lililotaka kujua hali ya Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) alisema: ‘’Lissu anaendelea vizuri na mazoezi anafanya…afya yake imekuwa ikiimarika siku hadi siku.”
Mwananchi lilipotaka kujua utaratibu wa kumsafirisha nje ya Kenya kwa matibabu zaidi, Alute aliyeko Nairobi alisema; ‘’Wiki ijayo nitakuwa na ‘Press Conference’ (mkutano na waandishi wa habari) nitazungumza yote na ‘the way forward.”
Picha mbalimbali zimekuwa zikitoka zikimwonesha Lissu akiwa mwenye tabasamu na wakati mwingine akiwa nje ya wodi katika kiti cha magurudumu pale anapotembelewa na ndugu,jamaa na marafiki.
Oktoba 17, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu afya ya Lissu, alisema baada ya matibabu awamu ya pili kukamilika, awamu ya tatu itafanyikia nje ya Kenya.
Alisema baada ya Chama hicho kushiriki kwa ukaribu zaidi katika awamu ya kwanza na ya pili, jukumu la usimamizi wa matibabu ya awamu ya tatu itakayofanyika nje ya Nairobi wataiachia familia ila wakishirikiana nao pale itakapohitajika.

No comments:

Post a Comment