Saturday, October 21

Acacia wadai hawana pesa za kuilipa Tanzania

Rais Dr Magufuli na Mwenyekiti wa Barrick Gold Profesa Thornton
Mamlaka ya juu kabisa toka kwa kurugenzi ya fedha ya Gold miner Acacia Mining Plc  imesema haina uwezo wa kuilipa Tanzania Dola za Kimarekani milioni 300 kama ilivyokubaliwa katika mazungumzo baina ya Tanzania na Barrick Gold hivi karibuni.
Shirika la habari la Reuters limeripoti Ijumaa kuwa Mkuu wa Fedha Andrew Wray amesema wakati wa uchambuzi juu ya kutatua mgogoro huo Ijumaa kuwa haitoweza kufanya malipo hayo.
Alhamisi Serikali ya Tanzania ilisema kuwa mazungumzo kati ya magwiji wa sheria na mambo ya mikataba ya madini na timu ya wataalamu wa Barick yamefikia maelewano na tayari Barrick Gold imekubali kulipa 300$m.
Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimesema kuwa mazungumzo hayo yamechukua muda Mrefu kutokana na unyeti wake.
Lakini wachambuzi wa mambo ya uwekezaji wanasema kuwa ni mapema sana kwa Tanzania kutangaza ushindi katika mazungumzo hayo.
Wanadai kuwa kuzungumza na Barrick Gold haitoshelezi kwani kampuni ya Acacia bado ni muhimu katika kufikia makubaliano katika mgogoro huo.
Rais Magufuli alisema Alhamisi kuwa Tanzania haitofanya mazungumzo yoyote na Acacia kwani wao sio wamiliki wakubwa wa uchimbaji huo, na kuwa mazungumzo yote yatafanyika baina ya Barrick Gold na Serikali ya Tanzania.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Barrick Gold amesema mbele bado kuna matumaini makubwa na wana kazi kubwa ya kufanya na maamuzi yote yanatakiwa yapitishwe na bodi ya wakurugenzi iliyopo Uingereza ambao wanamiliki 64% ya Acacia.

Mwenyekiti huyo Profesa John L. Thornton amesema kulikuwa na kutokukubaliana kati ya Tanzania na kampuni ya Acacia kuhusu masuala ya kodi, hata hivyo wamekubali kulipa dola milioni 300 kwa ajili ya kukuza uaminifu.

Kutokana na ugumu wa suala lenyewe wamekubaliana kuunda timu ndogo ambayo itashirikisha pande zote mbili kwa ajili ya kuendelea kushughulikia masuala machache yaliyobakia.
Lakini wachambuzi wanadai kuwa Acacia bado ni muhimu kushirikishwa katika mazungumzo hayo ili kufikia ufumbuzi wa kudumu kwani wao ndiyo wanahusika na shughuli za uchimbaji nchini Tanzania.
Wakati wa kupokea ripoti hiyo Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli alisema Barrick Gold wamekubali kulipa kile kinachostahili kwenye Halmashauri.
"Naomba Barrick walipe hizo Shilingi bilioni 700 haraka kwa sababu ninataka kuzitumia"

Pia aliwahikikishia Barrick Gold kwamba Serikali ya Tanzania sasa itaanza kufanya kazi moja kwa moja na kampuni hiyo.

"Barrick your true partner and your here to stay" akimaanisha Barrick nyinyi ni wabia wa kweli na mtaendelea kuwepo kufanya biashara hapa nchini,” aliwahakikishia Rais.

Rais pia aliiagiza Kamati hiyo iliyoshughulikia mgogoro wa Barrick Gold iendelee kufanya mazungumzo na makampuni yanayochimba Almasi na Tanzanite, kwa kutumia misingi ya mazungumzo yaliyofanywa na Barrick Gold, akiiagiza kuwa “kazi hiii ianze haraka na mapema"
Dkt Magufuli amesema kuwa kampuni hizo kama zikiwa hazitaki kuingia katika mazungumzo ili kufikia muwafaka juu ya uchimbaji madini ya almasi na tanzanite basi waondoke na kuiachia nchi madini yake.

No comments:

Post a Comment