Wednesday, September 20

Wawekezaji wazungumzia ushindani unavyoathiri bidhaa za ndani


WAWEKEZAJI katika sekta ya kilimo na mifugo wamelalamikia ushindani unaoletwa na bidhaa kutoka nje kutokana na serikali kushindwa kuzidhibiti kwa njia ya kupunguza kodi na tozo mbalimbali katika uzalishaji.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana wawekezaji hao ambao pia ni sehemu ya wabia wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo, Maji na Umwagiliaji katika Kongani ya Ihemi mkoani Iringa na Njombe, walisema ipo haja serikali ikaangalia suala hilo kwa jicho pana ili kulinda bidhaa za ndani.

Mkurugenzi wa kiwanda cha maziwa cha ASAS Dairies Limited kilichopo mkoani hapa, Bwana Fuad Abri alisema haiwezekani Tanzania iwe nchi ya pili kwa idadi ya ng’ombe barani Afrika baada ya Ethiopia lakini bado inapitwa katika uzalishaji na uingizaji maziwa nchini.

“Wenzetu Kenya wanazalisha lita 1,500,000 za maziwa kwa siku lakini Tanzania inazalisha lita 120,000 kwa siku. Wakati huohuo sisi tunawapita kwa umbali katika idadi ya ng’ombe, kama hiyo haitoshi bidhaa za maziwa kutoka mataifa jirani zinaingia kwa wingi na kutoa ushindani mkubwa na bidhaa za ndani,” alisema Bw. Abri.

Alisisitiza kuwa zipo namna nyingi za kuzuia ushindani huu kwa sababu Serikali ya Kenya inashirikiana kwa kiasi kikubwa na wazalishaji maziwa na ndiyo maana wana uwezo wa kusafirisha nje kwa bei shindani.

“Katika biashara hii ya maziwa kitu kikubwa kinachotakiwa kuangaliwa ni namna gani unapata maziwa yako, bei utakayonunulia ikupe faida lakini faida yenyewe iwe katika soko shindani,” alisema Bw. Abri.

Wabunge hao wakiongozwa na mwenyeji wao Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT, Bwana Geofrey Kirenga ambapo kwa upande wao waliongozwa na kaimu mwenyekiti wa kamati Bwana. Mashimba Ndaki, walitembelea kiwanda cha kuzalisha chakula cha mifugo na ufugaji kuku wa nyama na mayai, Silver Land kilichopo mkoani hapa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Bwana Jack Bennie alisema mbali ya kuwepo na utaratibu wa kulipa kiasi kidogo cha kodi kutokana na utaratibu wa kiuwekezaji lakini bado bidhaa za kuku na chakula cha mifugo vinaathiri soko kutokana na kuzalishwa chini ya kiwango lakini vingine vinaingia nchini na kuuzwa kwa bei ndogo inayovuruga ushindani.

“Tumeamua kufanya uwezekazi mkubwa katika sekta hii ya mifugo, lakini kuna tatizo la ushindani usioendana na uhalisia ambapo bidhaa kutoka nje zilituathiri kwa kiasi kikubwa, tunashukuru kwa sasa serikali imezuia kuingiza vifaranga vya kuku kutoka nje, tunaomba washikilie hapohapo kwa sababu kukosekana kwa vifaranga hivyo kumesaidia wazalishaji wa ndani kupata soko,” alisema Bwana Bennie. Akizungumzia hali hiyo mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo Dkt. Immaculate Sware alisema wawekezaji wakubwa namna hiyo ni fursa kwa watanzania hivyo serikali haina budi kuangalia namna ya kuwatengenezea mazingira mazuri ya biashara ili walipe kodi vizuri lakini pia wanufaishe jamii.

“Tumetembelea miradi mingi iliyo katika ubia na SAGCOT, mradi huu wa Silverlands ni mkubwa kwa hiyo tunapopata muda wa kusikiliza kero zao inakua jambo jema kujua namna ya kuzifikisha ili zitatuliwe na kusaidia jamii ambayo ndiyo wanufaika kwa njia nyingi ikiwemo kupata ajira na kupata huduma au bidhaa,” alisema Dkt. Sware.

SAGCOT imeamua kuwatembeza wajumbe wa kamati hiyo ya bunge ili kuona shughuli zinazofanyika katika kongani ya Ihemi ambayo ni miongoni mwa kongani sita zilizopo katika kituo hicho. Maeneo mengi waliyotembelea ni ile inayosimamia mnyororo wa ongezeko la thamani katika mazao ya nyanya, viazi mviringo, soya na maziwa.
 Mkurugenzi wa kiwanda cha maziwa cha ASAS Dairies Limited mkoani Iringa, Bwana Fuad Abri akitoa mada juu ya uendeshaji wa kiwanda chake na ubia wao na Kituo cha Kuendeleza kilimo Nyanda za juu kusini mwa Tanzania (SAGCOT) alipotembelewa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo,Mifugo , Maji na Umwagiliaji. Lengo la ziara ya Kamati hiyo ni kujionea na kujifunza juu ya Kongani ya Ihemi na shughuli za SAGCOT.
Mkurugenzi wa kiwanda cha maziwa cha ASAS Dairies Limited, Bwana Fuad Abri (kulia)akitoa maelekezo ya uendeshaji wa kiwanda chake alipotembelewa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo,Mifugo , maji na umwagiliaji. Ikiwa ni sehemu ya ziara ya kamati hiyo kujionea na kujifunza juu ya kongani ya Ihemi na shughuli mbalimbali za Mpango wa Kuendeleza Kilimo Nyanda za juu kusini mwa Tanzania(SAGCOT). Wapili kulia ni Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni mbunge wa Maswa Magharibi, Bwana Mashimba Ndaki. Watatu kulia ni Mjumbe wa kamati ambaye pia Mbunge wa viti Maalum Bibi Khadija Hassan Aboud. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT , Bwana Geoffrey Kirenga

No comments:

Post a Comment