Sera ya Viwanda ya mwaka 2003 imevigawa viwanda katika makundi makubwa manne kulingana na idadi ya watumishi ilionao pamoja na ukubwa wa mtaji.
Kundi la kwanza ni viwanda vidogo sana ambavyo huwa na watumishi kati ya mmoja hadi wanne na mtaji ukiwa chini ya Sh5 milioni. Kundi la pili ni viwanda vidogo ambavyo vina kati ya watumishi watano hadi 49 na mtaji wa kuanzia Sh5 milioni hadi Sh200 milioni.
Kundi la tatu ni viwanda vya kati vinavyoendeshwa na kati ya wafanyakazi 50 hadi 99 na mtaji wa kuanzia Sh200 milioni hadi Sh800 milioni. Na kundi la mwisho ni viwanda vikubwa vyenye watumishi kuanzia 100 na kuendelea na mtaji unaozidi Sh800 milioni.
Kwa mujibu wa sensa ya viwanda ya mwaka 2015, Tanzania ina jumla ya viwanda 49,243 kati ya hivyo, vidogo kabisa ni 41,919 sawa na asilimia 85.1 na vidogo ni 6,907 sawa na asilimia 14 wakati vile vya kati ni 170 sawa na asilimia 0.3.
Kwa aina ya viwanda vidogo vilivyopo sasa na namna vinavyoendeshwa mchango wake katika mapambano dhidi ya umasikini na kutengeneza fursa za ajira zenye tija bado ni changamoto. Viwanda hivi vinakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo zinakwamisha jitihada za kuufikia uchumi unaomilikiwa na wazawa.
Kitabu cha Mwalimu Nyerere cha Ujamaa kilichochapishwa mwaka 1970 kinaeleza mapinduzi ya viwanda yatakuwa na tija pale uchumi wake utakapokuwa unamilikiwa na wazawa na si wao kuwa wafanyakazi au vibarua wa mabepari.
Uwezeshwaji unaweza kufanyika kwa Serikali kuanzisha utaratibu wa kila mwaka kuwa na maonyesho ya viwanda vidogo kama ilivyo kwa yale ya biashara maarufu kama Sabasaba. Hapa inaweza kualika nchi zilizoendelea kwa viwanda mfano China kuja kuonyesha na kuuza teknolojia nafuu na rahisi kwa Watanzania.
Kwa Mtanzania wa kawaida anayetamani kumiliki kiwanda kidogo si rahisi kugharamia safari ya kwenda China kwa mfano, kuona na kujifunza namna wenzetu walivyofanikiwa kwenye uchumi wa viwanda vidogo ili aje kuwekeza nchini.
Ni vyema taasisi za fedha zikaacha utaratibu wa kutoa mikopo ya fedha taslimu kwa wenye nia ya kufungua viwanda vidogo na badala yake ianze kuwanunulia mitambo na mashine wanazozihitaji na kutoa ushauri wa kibiashara.
Licha ya hilo, taasisi za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Vyuo vya Ufundi (Veta), Shirika la Viwanda Vidogo (Sido), Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (Tirdo), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), na Shirika la Viwango nchini (TBS) pamoja na wadau wengine kuwa na mkakati wa pamoja kusaidia umiliki na uendeshaji wa kiwanda vidogo kwa watu wenye nia ya kumiliki viwanda nchini.
Serikali inaweza kuwawezesha wananchi kupitia misamaha ya kodi kwa wote wanaoanzisha viwanda. Inaweza kutungwa sera itakayowahamasisha wananchi, kwa mfano, kuruhusu Mtanzania yeyote atakayeanzisha kiwanda kidogo kuruhusiwa kuingiza mashine na mitambo bila kulipa kodi au kulipa kodi nafuu na kupewa angalau miaka miwili ya kutolipa kodi wala tozo yoyote ili kuvutia na wazawa wengi kufanya hivyo.
Kwa sasa gharama ya kuingiza vifaa vya kuanzisha viwanda vidogo nchini ni kubwa kuliko ununuzi wa kifaa husika nje ya nchi. Kama wawekezaji wakubwa wanapewa misamaha ya kodi mpaka miaka mitano kwa nini isiwe miaka kadhaa kwa mzawa?
Tanzania kuwa nchi ya viwanda inawezekana, Serikali iwawezeshe Watanzania kumiliki viwanda vidogo kwa kuwawekea mazingira ya kukua na kumiliki vya kati hatimaye vikubwa. Ni wakati wa vitendo na si maneno. Tumuunge mkono Rais Magufuli kutimiza azma hii.
Maendeleo ya kiuchumi yanahitaji kuimarishwa kwa soko la bidhaa za ndani ambazo zinapaswa kuwa za bei nafuu kadri iwezekanavyo. Kupunguza kodi au kutoa ruzuku kwa wajasiriamali ni miongoni mwa njia muafaka za kusaidia kupunguza gharama za uzalishaji hivyo bei ya bidhaa au huduma husika.
Mamlaka za udhibiti na serikali lazima ziwe na mkakati wa kuhakikisha gharama za uwekezaji na uzalishaji zinakuwa chini kwa kuweka mazingira rafiki. Viwanda vingi vikianzishwa na kuzalisha kama inavyotegemewa ajira zitaongezeka.
Kuongezeka kwa ajira kutaimarisha kipato cha wananchi, kukuza mzunguko wa fedha na kuinua Pato la Taifa (GDP) na mwisho wa siku kuiondoa Tanzania kwenye orodha ya nchi maskini.
Mapambano dhidi ya umaskini yanahitaji ushiriki wa kila mdau kutoka alipo. Serikali na sekta ya umma zikishirikiana, lengo litatimia ndani ya muda mfupi ujao hiovyo kutimiza malengo tuliyojiwekea.
Mwandishi ni Mtakwimu na Ofisa Mipango wa Halmashauri.
No comments:
Post a Comment