Wachimbaji wawili wa dhahabu katika mgodi wa Sekenke One kitalu namba moja wilayani Iramba wanahofiwa kufa baada ya kufukiwa na udongo.
Mgodi huo katika Kijiji cha Konkilangi kata ya Nwike tarafa Shelui mkoani Singida.
Ajali hiyo imetokea jana Jumamosi saa 7:47 usiku mgodini humo na pia imesababisha majeruhi watano.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Isaya Mbughi amesema wachimbaji wanaohofiwa kufa ni Simon Odochi (26) maarufu kwa jina la Wamwanza mkazi wa Jiji la Mwanza.
Mwingine ni Kashinde Nkula (27), mkazi wa Kijiji cha Mangusu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Amesema juhudi za kuwaokoa zimeanza tangu usiku wa manane na kwamba hadi leo Jumapili saa 3:30 asubuhi wachimbaji hao walikuwa bado hawajapatikana.
Kaimu Kamanda Mbughi amesema ajali hiyo pia imesababisha majeruhi ambao ni Ayubu Msengi (34), mkazi wa Ntwike; Mwita Salumu (42) wa Gumanga; Lazaro Edward (28) wa Kiomboi Soweto; Jeremi Idd (41) wa Kijiji cha Gumanga na Jumanne Said (24) wa Kijiji cha Mgongo.
Majeruhi hao watano amesema waliokolewa na wenzao na chanzo cha ajali hiyo ni kutitia kwa udongo.
No comments:
Post a Comment