Marekebisho hayo yanakuja miezi miwili baada ya Mkutano wa Saba wa Bunge (bajeti) kupitisha Muswada wa Sheria Mbalimbali, pamoja na mambo mengine sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho.
Marekebisho hayo yaliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na kuridhiwa na Bunge jana yapo katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 3 wa Mwaka 2017.
Masaju alisema kifungu hicho kwa namna kilivyoandikwa kinapingana na masharti ya Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu Umiliki wa Maliasili na Raslimali za Nchi ya Mwaka 2017 na Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba inayohusu Maliasili ya Nchi Mwaka 2017.
Alisema sheria hizo zinaainisha kuwa Bunge linaweza kupitia mikataba iliyoingiwa na Serikali kuhusiana na maliasili na rasiliamali za nchi, si kutoa kibali cha kuanza kutumia.
“Hivyo ibara ya 16 ya muswada huu inapendekeza kifungu hicho kifutwe. Lengo la marekebisho haya ni kuwianisha masharti ya sheria hizo kuhusiana na nafasi ya Bunge kutekeleza ipasavyo wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri ipasavyo Serikali, kwa mujibu wa ibara 63(2) ya Katiba,” alisema Masaju.
Akitoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh Ally alihoji sababu ya Serikali kufanya tena marekebisho ya kifungu hicho kwa kuondoa mamlaka kwa Bunge.
“Ni mwezi wa pili sasa, Sheria ya Petroli ifanyiwe marekebisho na kuongeza kifungu kidogo cha sita na kulipatia Bunge mamlaka ya kuridhia mikataba yote ambayo inahusiana na rasilimali ya mafuta ya petroli.” alisema Saleh na kuongeza:
“Marekebisho ya Sheria mara nyingi huletwa baada ya mamlaka za Serikali kupata uzoefu wa utekelezaji wa sheria husika, suala la kuhoji hapa ni kuwa ni uzoefu gani ambao Serikali imepata ndani ya miezi miwili baada ya kutungwa kifungu hiki?”
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa alisema kamati imekubaliana na mabadiliko hayo.
Alisema kama Bunge litapitisha mikataba hiyo hakutakuwa na dhana ya kuisimamia katika mihimili ya dola, hivyo kulifanya Bunge kuwa Sehemu ya makosa au matatizo yanayotokana na mikataba hiyo.
Akichangia Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara alisema marekebisho ya sheria hiyo yaliletwa Bunge hivi karibuni na wao wakalalamikia kuletwa kwa dharura.
“Nguvu kubwa inayotumika hapa. Wakati ujao hii habari ya dharura tuache, tuzingatie utaratibu tupokee ushauri tusiangalie sura yake wala chama chake, dharura imeligharimu Taifa hili, imetuumiza na hili tatizo linaendelea kujirudia,” alisema.
Naye Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali alisema wapo mawaziri waliopita kwa kukosea kidogo tu na pengine kwa kushauriwa na wanasheria, hivi sasa wapo matatani. “Kwa nini huyu Mwanasheria Mkuu wa Serikali naye asiwajibishwe, ameiabisha Serikali lakini analeta sheria zinazopingana na nyingine. Naamini sheria zote zinazokuja hapa zinapitia mezani kwako na wewe unazipitia,” alisema.
No comments:
Post a Comment