Kiongozi wa Muungano wa Upinzani nchini Kenya (Nasa) Raila Odinga, ameilaumu Ikulu ya Nairobi ya State House, kwa kuwazuia vigogo wa muungano huo, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula kusafiri kwenda nchini Uganda.
Bw. Odinga amesema kuwa viongozi hao wawili walizuiwa kwenye uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta walipokuwa wakiondoka kwenda nchini Uganda ambapo Bw. Musyoka angekuwa ahutubie mkutano wa sherehe za kufuzu.
Musyoka alikuwa akielekea kwenye chuo cha Uganda Technology and Management ambapo yeye ni chansela.
Licha ya wawili hao kuruhusiwa kuondoka, Bw. Odinga alisema kuwa hiyo isharaya kuzoroteka kwa haraka kwa hali ya kisiasa nchini na mikakati ya kujaribu kuzua hofu nchini.
Kupitia taarifa Bw. Odinga alisema kuwa polisi waliwaambia wawili hao kuwa viongozi wote wa upinzani watahitaji ruhusa kutoka Ikulu ya Nairobi kabla ya kuondoka ndani ya nchi.
"Nasa inalaani jihada za hivi punde ya kuingilia uhuru na kuwahangaisha viongozi wake wakuu," taarifa hiyo ilisema.
Alisema kuwa upinzani utapuuza agizo lolote kwa kuwa viongozi wake hawahitaji ruhusa yoyote ya kusafiri nje ya nchi.
"Upinzani nchini Kenya ni lazima uwe huru kama sehemu ya siasa za Kenya na ni lazima uruhusiwe kuendelea na mikakati yake kama serikali mbadala na sauti ya watu kwa mujibu wa katiba, kwa mujibu wa katiba." Odinga alisema.
No comments:
Post a Comment