Kinyeto, Singida. Saa 2:00 asubuhi katika Zahanati ya Kinyeto wilayani Singida Vijijini, wagonjwa wanane wapo kwenye foleni ya kusubiri kumuona daktari.
Sehemu nyingine, wajawazito wawili wapo chumba cha kujifungulia wakisubiri kujifungua.
Wote hao wanasubiri huduma ya daktari mmoja, Joyce Temu aliyekuwa zamu akimhudumia mgonjwa mwingine aliyefika kutibiwa.
Kutokana na wingi wa majukumu, daktari analazimika kuingia chumba cha kujifungulia kila baada ya muda, hasa anaposikia sauti ya akina mama hao wakilalamika kwa uchungu.
Wakati Dk Temu akikabiliana na majukumu hayo tofauti, Hadija Hango (46) anafika hapo nusu saa baadaye akiwa ameongozana na binti yake anayeitwa Amina Ramadhani (18) aliyekuwa akilalamika kwa uchungu wa kujifungua.
Wanapoingia ndani, Amina, aliyekuwa akitarajia mtoto wa kwanza, analalamika zaidi na kumfanya daktari awaache wagonjwa wengine na kumkimbilia ili amhudumie.
“Kwanini mmemleta hapa badala ya kumpeleka hospitali ya rufaa kama ilivyoandikwa kwenye kadi ya kliniki?” anahoji Dk Joyce.
Kwa kuwa chumba cha kujifungulia kina vitanda viwili pekee, Dk Temu analazimika kumuingiza Amina chumba cha tabibu na baada ya vipimo anatoa taarifa.
“Mtoto huyu amekaa vibaya na hawezi kujifungua kwa njia ya kawaida. Ni lazima awahishwe Hospitali ya Rufaa,” anasema.
Anajaribu kupiga simu kwa Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) kuomba usafiri, lakini anakosa. Wakati anaendelea kuhangaika kutafuta usafiri mwingine, anampigia simu muuguzi aliye mapumzikoni akimtaka afike zahanati haraka kwa kuwa hawezi kumuacha Amina aende hospitali mwenyewe.
“Ni hatari siwezi kumuacha mwenyewe. Barabara yetu ni mbovu. Kutokana na mitikisiko ya gari anaweza kujifungua njiani, kwa hiyo ni lazima nimfikishe na nitakaa huko mpaka ajifungue,” anasema Dk Temu huku akiandaa vifaa vya dharura kwa ajili ya Amina.
Wakati Dk Temu anajiandaa kwa takriban saa moja huku akimsubiri muuguzi aliyekuwa mapumzikoni afike, wagonjwa wote waliokuwa wakisubiri huduma, wanaonekana kugugumia kwa maumivu.
Haya ni maisha ya kila siku ya wakazi wa Kata ya Kinyeto ambao hawana sehemu nyingine ya kupata huduma za afya zaidi ya zahanati hiyo yenye uhaba mkubwa wa watumishi. Mbadala wa zahanati hiyo ni Hospitali ya Rufaa ya Singida iliyo umbali wa zaidi ya kilomita 18.
Zahanati hiyo ina watumishi wanane pekee wa afya wanaowahudumia zaidi ya watu 12,082 kutoka vijiji vinne vya Kinyeto, Ntunduu, Minyaa na Mkimbii, wakati Sera ya Afya ya mwaka 2007 inataka kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya.
Pia, uhaba huo wa watumishi upo kinyume na sera hiyo inayoagiza zahanati kuwa na watumishi 12 mpaka 15, lakini Kinyeto ina tabibu, msaidizi wake, muuguzi na mhudumu wa afya. Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa zahanati inapaswa kuwa na watumishi wasiopungua 15.
Bashir Juma, mkazi wa kijiji cha Minyaa aliyekuwa akisubiri huduma ya matibabu kwenye zahanati hiyo, anasema hali hiyo wameshaizoea na wakati mwingine mhudumu anapokosekana husubiri muda mrefu hadi mwingine awasili.
“Kuna siku alikuwepo mkunga peke yake. Mjamzito alipotakiwa kuwahishwa hospitali kubwa kwa dharura, alituacha hapa tukasubiri tangu saa 3:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana alipokuja mganga ambaye alikuwa mapumzikoni,” anasema Bashir.
Wahudumu wafichua zaidi
Akiungumzia upungufu huo, Dk Temu anasema zahanati hiyo ilipaswa iwe na angalau wakunga wawili, waganga wawili, mfamasia, mtunza takwimu mfanya usafi hivyo ingepunguza uzito wa kazi.
Kutokana na upungufu, Dk Temu hufanya kila kitu anapokuwa zamu; hulazimika kumhudumia mgonjwa, kumwandikia dawa na kwenda kumchukulia dawa hizo.
“Jana mchana na usiku nilikuwa zamu. Asubuhi nimeingia tena kama ulivyoona jana kulikuwa na wajawazito wawili waliokuja kujifungua na mmoja nilimpeleka mkoani,” anasema.
“Ikitokea dharura kama hiyo anaitwa mwingine aliye mapumzikoni kuendelea kutoa huduma. Kwetu ni tatizo, mtumishi huna uhuru wa kwenda mbali na kituo.”
Muuguzi msaidizi wa kituo hicho, Janeth Philipo anasema mara nyingi wanakosa muda wa kufanya shughuli muhimu za kijamii kutokana na kituo hicho kuhudumia wagonjwa wengi.
“Tunahitaji watumishi waongezwe, iwapo wataongezwa na zahanati ikapanuliwa itakuwa na huduma muhimu kama wodi ya kulaza kinamama kwa kuwa hawa ndio wengi zaidi na hakuna wodi za kuwalaza,” anasema Janeth.
Lakini tatizo hilo si la muda mfupi.
Godfrey Kiria, ambaye ni tabibu msaidizi, anasema tangu kujengwa kwa zahanati mwaka 1972 haijawahi kuwa na watumishi wa kutosha.
“Zahanati inatakiwa kuwa na watumishi 15 lakini mpaka sasa tupo wanne pekee. Serikali iangalie katika ajira zilizopo waongezwe watumishi wa afya Kinyeto,” anasema Kiria.
Mbali na uchache wao, watumishi bado wanakabiliwa na tatizo la makazi. Kuna nyumba moja tu inayotumiwa na mganga mfawidhi na mkunga. Watumishi wengine wawili wamepanga mtaani ambako ni mbali na zahanati.
Nyumba na zahanati vyote havina vyoo.
Mikakati ya Kinyeto
Kinyeto ina mpango wa kupunguza tatizo hilo. Mtendaji wa kata, Romana Haule anasema huwa anapeleka taarifa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ambaye humpangia watumishi kwenye eneo lake.
“Uhaba wa watumishi wa sekta ya afya ni tatizo la nchi nzima, Serikali imetoa kibali cha kuajiri zaidi ya watumishi 3,000 ambao watatusaidia kupunguza upungufu huu,” anasema Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida (DMO), Sungwa Kabissi.
“Halmashauri inaendelea na utaratibu wa kuomba kibali na kuajiri watumishi wanaohitajika.”
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Singida, Rashid Mandoa anasema mbali na kuongeza watumishi, wana mikakati ya kupanua zahanati na kuanzisha kituo cha afya kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18, lakini kwa sasa wameelekeza nguvu katika maeneo korofi zaidi Singida Vijijini zikiwemo Kata za Ilongero na Lamba.
“Tunatekeleza Sera ya Afya ya mwaka 2007 kwa kila kijiji kuwa na zahanati. Tumepita vijiji vyote na tumeshawaeleza wenyeviti kuwa wanatakiwa kujenga na tayari vijiji vya Lamba na Malolo vimeshajengwa na tunaendelea kuzikamilisha kwa kushirikiana nao,” anasema.
“Lakini pale ambapo wananchi wameamua kujenga na wakafikia hatua ya kupaua, halmashauri inakamilisha kwa kuunga mkono jitihada zao.”
Anataja baadhi ya maendeleo waliyopata katika sekta ya afya kuwa ni kujenga kituo cha afya kila tarafa kama Mgori, Ilongero na hospitali upande wa tarafa ya Mtiko Singida na vijiji vyake kuna zahanati kila kata isipokuwa zipo ambazo zina uchakavu wa miundombinu.
Hata hivyo, Mandoa anasisitiza kuwa katika sekta ya afya mapungufu mengi yakiwemo upungufu wa maabara na wanaendelea kuyafanyia marekebisho na kujenga vyumba vya upasuaji vya uzazi na macho katika kata ya Mgori kwa mwaka huu wa fedha.
No comments:
Post a Comment