Friday, September 29

Tumbaku yauzwa bei ya hasara


Hatimaye wakulima wa tumbaku Kahama mkoani Shinyanga wamekubali kuuza ziada ya kilo milioni 3.2 iliyozidi kwenye makisio ya mwaka 2016/17 kwa bei yoyote, badala ya kuiacha kwenye maghala.
Walisema ikiachwa itaharibika, kupungua uzito na kupoteza ubora. Hali hiyo imekuja baada ya kampuni za kununua zao hilo TLTC na Alliance One kununua kiwango kilichokuwa kwenye mkadirio ya msimu ambazo ni kilo milioni 6.5.
Katika mkutano wao wa dharura uliofanyika juzi mjini Kahama na kuratibiwa na Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (Kacu) kinachohudumia Mbogwe mkoani Geita na Ushetu mkoani Shinyanga, baadhi ya wakulima waliiomba Serikali iziruhusu kampuni hizo ziinunue tumbaku hiyo kwa bei yoyote.
Mmoja wa wakulima hao, Safari Manjara alisema hali waliyonayo ni mbaya kiuchumi kwani tumbaku iliyobaki kwenye maghala inazidi kuharibika na kwamba hata wakigoma kuuza kwa bei ndogo, ni hasara zaidi kwa kuwa zao hilo halina soko mbadala.
Manjara alisema wapo tayari kuuza kwa bei yoyote ambayo kampuni zimeweka masharti na kuitaka Serikali ifupishe mazungumzo, kwani zikisusia matokeo yake wakulima watapata hasara.
Naye Phoni Masanja alisema kosa lililojitokeza la kuzalisha tumbaku nje ya mkataba. ambalo siyo tatizo la kampuni bali wakulima ambao wamezalisha zaidi, hivyo wanapaswa kuwa wapole.
“Mwenyekiti, kosa ni letu wenyewe wewe umeambiwa mwaka huu lima kiasi fulani mnaandikishana, wewe unalima zaidi kosa ni la nani?” alihojiMasanja.
Pia, Masanja alimuomba Mwenyekiti wa Kacu, Emmanuel Peter kuhakikisha kampuni hizo zinanunua zao hilo bila masharti kwa kuwa bila hivyo mwaka huu hakuna uzalishaji kutokana na wakulima wengi hajazauza.
Msimamo wa wanunuzi
Mwenyekiti wa Kacu, Peter alisema kampuni hizo zimekubali kununua kwa bei ya Dola moja ya Marekani kwa kilo, tofauti na Dola mbili walizonunulia tumbazo iliyokuwa kwenye mkataba.
“Tumbaku iliyokuwa kwenye mkataba ilinunuliwa kwa Dola mbili kwa kilo, ingawa hadi kufikia juzi makubaliano yalianza kwenda vizuri kutokana na Alliance One kukubali kununua kwa Dola 1.35 kwa kilo hali hiyo ni zaidi ya asilimia 50 ya bei ya mwaka jana,” alisema Peter na kuongeza: “TLTC wao bado wana bei ya dola 1 kwa kilo sawa na asilimia 50 ya bei waliyonunulia kwenye mkataba,”

No comments:

Post a Comment