Tanzania imetangaza zabuni ya ujenzi wa mradi mkubwa wa bwawa la kuzalisha umeme katika moja ya hifadhi kubwa zaidi za wanyama nchini humo.
Mradi huo wa uzalishaji wa umeme katika Maporomoko ya Maji ya Mto Rufiji, yafahamikayo pia kama Stiegler's Gorge, ambayo hupatikana ndani ya hifadhi ya Selous utaongeza uzalishaji wa umeme nchini Tanzania mara dufu.
Mpango huo umepingwa sana na wanamazingira ambao wanaamini kwamba utaathiri pakubwa wanyamapori pamoja na jamii zinazoishi eneo hilo.
Hifadhi hiyo ya wanyama imeorodheshwa miongoni mwa Turathi za Dunia.
Tanzania imekuwa ikikabiliwa na tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara kwa muda sasa.
Serikali imesema mradi huo utazalisha umeme wa kiasi cha megawati 2,100 na na utagharimu kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 2 ambazo zitatolewa na Serikali ya Tanzania.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani alikuwa mapema wiki hii amesema kwamba serikali ya Tanzania inazo fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi husika.
Dkt. Kalemani alisema taratibu za awali za utekelezaji wa mradi huo zimekwisha anza ambapo Wataalam kutoka ndani na nje ya nchi wamekwishakutana na kupitia nyaraka za mradi ikiwemo kuchagua eneo ambalo mradi husika utajengwa.
Alisema miongoni mwa mengine, kumefanyika upembuzi yakinifu wa kujengwa miundombinu ya umeme jukumu ambalo limefanywa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakati Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza maandalizi ya ujenzi wa barabara katika eneo husika.
„Mkandarasi atakayepewa kazi ya kujenga mradi huo ni yule atakayeridhia kujenga mradi husika kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi wa mwaka mmoja na nusu zaidi ya ule uliowekwa wa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwezi Oktoba au Novemba mwaka huu," Dkt Kalemani amenukuliwa kwenye taarifa iliyotolewa na wizara ya madini na nishati Tanzania.
Dkt. Kalemani amesema malengo ya Serikali ni kuzalisha umeme kiasi cha megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020 na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025 kama Sera ya Nishati ya mwaka 2015 inavyoelekeza.
"Tunataka kujenga Tanzania ya Viwanda. Tunataka ifikapo mwaka 2019-20 tufike megawati 5,000. Tanzania ya Viwanda inahitaji umeme, mradi kama huu na pia ya Kinyerezi I Extension, MW 185 Kinyerezi II MW 240 na miradi mingine itawezesha kufikia lengo letu," alisema Dkt. Kalemani.
Mradi huo wa Stiegler's Gorge ulikuwa umekawia kwa muda mrefu lakini mwezi Juni, Dkt Magufuli alipozulu Mkoa wa Pwani alitangaza kwamba mradi huo utatekelezwa.
"Stiegler's Gorge mradi ambao ulifanyiwa utafiti tangu enzi ya Mwl. Julius Nyerere, tukautelekeza, nataka tujenge bwawa litakalozalisha umeme utakaotosheleza katika nchi yetu, nchi ya viwanda, ili Watanzania wasilalamikie tena suala la umeme, nataka tuachane na umeme wa matapeli wanaokuja hapa wanawekeza kwa lengo la kutuibia.
No comments:
Post a Comment