Wednesday, September 6

Sura mbili za Uhuru Kenyatta





Siku 60 za marudio ya uchaguzi wa rais wa Kenya zinazidi kukatika baada ya Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika Agosti 8, mwaka huu.
Mahakama ilifuta matokeo hayo yaliyompatia ushindi Rais Uhuru Kenyatta dhidi ya mpinzani wake wa Muungano wa Nasa, Raila Odinga baada ya kuridhika kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini humo (IEBC) iliendesha uchaguzi huo kinyume na Katiba na sheria.
Odinga aliyepata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74 dhidi ya kura 8,203,290 (asilimia 54.27) za Kenyatta, alipinga matokeo hayo mahakamani.
Sura ya kwanza
Mara baada ya IEBC kutangaza matokeo hayo na Raila kuyapinga, wafuasi wa kiongozi huyo wa upinzani waliingia mitaani kuandamana lakini walikumbana na vikwazo na baadhi yao kuuawa.
Haya hivyo, kinyume na matarajio ya wengi, Rais Kenyatta aliingilia kati na kuruhusu waandamane kwa amani kufikisha ujumbe wa kupinga matokeo hayo bila kuharibu mali za watu wengine.
Kenyatta aliwataka polisi kujizuia kutumia nguvu kubwa na badala yake wawape ulinzi wakati wa maandamano hayo ya amani na yanayoruhusiwa kisheria kwa watu ambao hawafurahii matokeo ya uchaguzi.
Rais Kenyatta alisema hayo alipokuwa akitoa ujumbe kwa wagombea walioshindwa katika uchaguzi huo akiwa katika Jengo la Harambee alikokwenda kukutana na Kamati ya Maandalizi ya Hafla ya kuapishwa kwake.
Katika ujumbe huo uliomlenga zaidi Odinga aliyekuwa mgombea urais kupitia muungano wa Nasa, Kenyatta aliwataka wagombea wote ambao hawakuridhishwa na matokeo ya uchaguzi wachukue hatua zilizobainishwa na Katiba ili kupata wanachotaka — mojawapo ni kwenda mahakamani.
Kauli hiyo ya Kenyatta haikushangaza sana, maana kutokana na hulka ya mshindani wake, inaonyesha ni mtu wa kauli na matendo ya kidemokrasia kuliko viongozi wengi wa Afrika.
Katika kipindi chake cha uongozi, Rais Kenyatta ameruhusu wapinzani kufanya siasa bila bugudha, mikutano ya kisiasa na maandamano bila vikwazo na mambo mengi yanakwenda kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo.
Hata hivyo, mara baada ya Odinga kuwasilisha malalamiko katika Mahakama ya Juu ambayo ilitoa hukumu ya kufuta matokeo ya uchaguzi huo, Rais Kenyatta alihutubia Taifa na kutangaza kutokubaliana na uamuzi huo lakini akasema ataheshimu mahakama. Zaidi, alisisitiza amani na utulivu wakati Wakenya wanasubiri uchaguzi wa marudio.
Hatua hiyo ilikuwa tisa na ikapongeza na dunia nzima, lakini muda mfupi baadaye, ndani ya saa 24, Kenyatta ameanza kuonyesha sura yake ya pili; alianza kutoa lugha za vitisho na kashfa kwa majaji waliohusika katika hukumu ya kihistoria iliyofuta ndoto za kuapishwa mapema.
INAENDELEA UK 18
INATOKA UK 15
Kenyatta anasema akirudia uchaguzi huo na akashinda tena, majaji hao walioongozwa na Jaji Mkuu David Maraga watamtambua.
Anasema haiwezekani uamuzi uliofanywa na mamilioni ya Wakenya ukatenguliwa na watu wanne, na kuwa hapo kuna tatizo ambalo itabidi alishughulikie baada ya kurejea madarakani.
Katika hukumu hiyo, majaji wanne kati ya saba walitoa hukumu ya kutengua uchaguzi huo, wawili walitaka matokeo yabaki vilevile na mmoja hakutoa hukumu kwa kuwa alikuwa anaumwa.
Majaji waliobatilisha uchaguzi kwa kuwa na kasoro za kikatiba na kisheria ni Jaji Mkuu Maraga, Naibu Jaji Mkuu, Philomena Mwilu, Smokin Wanjala na Isaac Lenaola. Majaji waliotoa msimamo tofauti ni Jaji Jackton Ojwang na Njoki Ndung’u ambao walisema hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuonyesha kama uchaguzi huo unapaswa kufutwa. Jaji Mohammed Ibrahim ambaye hakuwapo kutokana na kuwa mgonjwa.
Hotuba ya Kenyatta
Katika sehemu ya hotuba yake kuhusu hukumu ya mahakama, Rais Kenyatta aliwaambia wafuasi wake kwamba Jaji Mkuu Maraga anatakiwa kutambua kwa sasa yeye (Kenyatta) si rais mtarajiwa tena ila ni rais anayekalia kiti.
Rais huyo ametoa kauli za namna hiyo kwenye mikutano ya hadhara aliyofanya katika maeneo mbalimbali nchini humo na kurushwa na vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Pia, alifanya hivyo alipozungumza na baadhi ya viongozi waliochaguliwa katika majimbo kupitia chama chake.
“Si Maraga na majaji wenzake hao wakora (waporaji) wamesema hiyo uchaguzi ipotee, si ndiyo, sasa mimi si mtarajiwa tena, na tukimaliza uchaguzi hawa watu tuta deal nao (tutawashughulikia), wala msijali, wasituchezee hawa bana, maamuzi ya watu mamilioni yashindwe na watu watano? aliwauliza wafuasi wake waliokuwa wakishangilia kauli hizo.
Kenyatta alihoji ushindi mkubwa wa nafasi ya maseneta kupitia Jubilee huku akiwatoa hofu wafuasi hao kuhusu uchaguzi mkuu ujao kwamba watashinda.
“Hawa watu sita wameamua kwamba, watachagua rais, sasa tutaonana nao kwa debe (sanduku la kura), mko tayari au hamko tayari? Aliwahoji wafuasi wake huku wakimjibu kwa kushangilia kuwa tayari katika uchaguzi ujao.
“...kwa sasa tutulie, kampeni tutapiga lakini hawa majamaa (majaji) tutawaona huko mbele,” alisema.
Kenyatta amekosea wapi?
Akijadili sura hizo mbili za Rais Kenyatta, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Bashiru Ali anasema Kenyatta amevuka mipaka na anatakiwa kuwaomba radhi Wakenya kwa sababu ametukana taasisi na siyo majaji na amebeza Katiba iliyowapa mamlaka hayo kupitia Wakenya.
“Tunaweza kusema ni sawa na mkuki kwa nguruwe, kwa binadamu mchungu. Mwaka 2013 Odinga alilalamika katika mahakama hiyohiyo na alishindwa kesi, hatukuona majaji wakishambuliwa, lakini leo (mwaka 2017), mahakama ambayo imetumia Katiba hiyo inashambuliwa. Kenyatta leo amekuwa kama mbongo aliyejeruhiwa,” anasema Dk Bashiru.
Anafafanua kwamba, jeuri aliyoionyesha kiongozi huyo itakuwa imepunguza imani ya wananchi kwake endapo atarejea Ikulu.
Vitisho vitafanikiwa
Licha ya dosari hiyo inayoweza kupunguza Imani kwa Wakenya, Dk Bashiru anasema kwa bahati mbaya, Kenyatta hana mamlaka ya kufukuza, kuteua au kufanya maamuzi yanayoweza kuwaathiri majaji hao wala kwenda mahakama ya kimataifa dhidi yao, badala yake amebakiza mahakama ya umma pekee itakayoamua hatma yake.
Dk Bashiru anasema hofu iliyopo kwa Taifa hilo ni kuporomoka kwa imani ya Nasa dhidi ya Tume ya Uchaguzi wanayotaka ivunjwe huku Jubilee ikiitetea.
“Sijui kama Nasa watakubaliana na IEBC isimamie uchaguzi. Wanaweza kuingia barabarani. Na huo ndiyo mtihani kwa Wakenya katikati ya wanasiasa wanapokerwa na maamuzi ya Katiba ili kulinda masilahi yao ya muda mfupi. Katiba imejenga jamii moja ya Wakenya lakini mwanasiasa anataka kulinda masilahi yake ya miaka mitano Ikulu,” anasema.
Anasema vipimo kwa Taifa hilo ni viwili tu; kulinda amani na utulivu hadi marudio ya uchaguzi yatakapomalizika na uvumilivu wa kisiasa kwa pande hizo mbili (Nasa na Jubilee).
Heshima ya Kenyatta
Tayari Chama cha wanasheria wa Kenya (LSK) na kile cha Afrika Mashariki vimemkosoa Rais Kenyatta baada ya kuwashambulia na kuwatishia majaji wa Mahakama ya Juu kufuatia uamuzi wa kubatilisha matokeo ya uchaguzi.
Rais wa LSK, Isaac Okero anasema Rais Kenyatta hakutakiwa kutoa vitisho kwa Jaji Mkuu Maraga na majaji wengine wa mahakama hiyo kwamba wamekosea kutoa hukumu hiyo.
Okero anasema matamshi ya rais kwamba majaji hao wasubiri rais achaguliwe katika uchaguzi ujao hayafai kutoka kwa kiongozi wa Taifa ambaye chini ya Katiba ya Kenya ni nembo ya umoja wa Wakenya.
Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala bora, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania(OUT), Dk Emmanuel Mallya anasema matamshi hayo yanatoka kwa kiongozi aliyekuwa na matarajio ya kupata ushindi wa mahakama hiyo. Pili, ametoa kauli hiyo akitaka kuionyesha mahakama kutokuwa sahihi katika hukumu waliyoitoa dhidi yake.
“Akiingia madarakani anaweza kutekeleza vitisho vyake lakini kwa kubadili Katiba yenyewe kwa sababu ya idadi kubwa ya wabunge alionao kutoka Jubilee, vinginevyo kauli hizo za vitisho hazitakuwa na athari zozote,” anasema Dk Mallya.
Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe anasema Rais Kenyatta alikuwa tayari ameshajijengea heshima ya kuwa mshauri wa masuala ya demokrasia Afrika kwa kuwa nchi nyingi za bara hilo zinayumbishwa na mifumo ya demokrasia.
Anasema baada ya kusema anaheshimu mahakama, alitakiwa kunyamaza kimya, heshima yake ingekuwa kwenye kumbukumbu nzuri sana na baada ya kustaafu angenufaika sana kama mshauri wa demokrasia Afrika na duniani. “Sasa kauli za vitisho zimetia dosari, kilichomponza nadhani ni wapambe wake, kuwatisha majaji ili ikitokea tena kesi ya aina hiyo wasimwangushe, waogope,” anasema.
Afrika ni zaidi ya Kenyatta
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanasema sura mbili zilizoonekana kupitia kauli za Rais Kenyatta, ni ndogo kuliko hali ilivyo kwa matendo ya viongozi wenzake wa nchi za Afrika katika eneo la uvumilivu wa kisiasa.
Baadhi ya viongozi hao ni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye yupo madarakani kwa miaka 30 tangu alipotwaa madaraka huku mpinzani wake Dk Kizza Besigye akiwa katika misukosuko isiyokoma ya kisiasa.
Rais wa Sudan, Omar Al-Bashir ndiye rais wa nchi hiyo tangu mwaka 1989 hadi sasa. Kiongozi huyo aliingia madarakani baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Sadiq al-Mahdi kuondolewa na jeshi.
Baada ya uchaguzi wa mwaka 2010, Bashir alishinda tena nafasi hiyo na kuendelea kuwa Rais wa Sudan na hadi mwaka huu, anatimiza miaka 28 ya kuwa madarakani.
“Kwa Afrika ni ngumu sana kiongozi kuonyesha uvumilivu wa kisiasa. Imeonekana Ghana na Senegal ambao wamekuwa wakiachiana madaraka na wapinzani, lakini tusilaumu sana kwa Kenya, kuheshimu uamuzi wa mahakama ni hatua kubwa,” anasema Dk Mallya.

No comments:

Post a Comment