Safi si tajiri wala kigogo ndani ya Serikali na hajawahi kuwa ofisa katika asasi za kiraia kiasi kwamba akashawishika au kushawishiwa kufanya kazi hiyo.
Lakini upendo wake wa maendeleo ya kijiji hicho ndio ulimfanya aanzishe masomo ili kuwaandaa watoto kwa ajili ya kusaidia visiwa hivyo siku zijazo.
Mvuna, kisiwa anachoishi Safi, ni miongoni mwa visiwa vitano katika Ziwa Tanganyika na ni kitongoji cha Kijiji cha Mandakerenge chenye changamoto lukuki za huduma za kijamii kama elimu na afya.
Kijiji cha Mandakerenge, ambacho kipo Kata ya Kipili, kina vitongoji 13 vinavyotegemea shule moja ya msingi. Kutokana na umbali na changamoto za usafiri, watoto wa Mvuna hawawezi kuvuka maji ya Ziwa Tanganyika kuifikia shule hiyo kupata elimu.
Akieleza sababu iliyomsukuma kuanzisha shule hiyo mwaka 2014 hivi karibuni kisiwani humo, Safi ambaye elimu yake ni ya msingi, anasema aliona uchungu kuona watoto wengi wakiishi bila kupata elimu.
“Kilichonisukuma mimi ni kuona watoto wanakaa nyumbani bila kuwa na kazi yoyote na bila kuwa na elimu. Niliwakusanya watoto wapatao 120 na kuanza kuwafundisha nikiungwa mkono na kanisa langu la Agape,” anasema.
Anasema alipeleka wazo lake kwa uongozi wa kitongoji na baadaye Halmashauri ya Wilaya ya Namanyere ikapata taarifa na ndipo alipopewa jengo linalotumiwa kama zahanati ya dharura alitumie kama darasa lake.
Katika safari hiyo, Safi anasema kanisa analosali lilimsaidia kumpa posho ya kujikimu kwa kuwa hakuwa na muda mwingine wa kufanya shughuli za kiuchumi kama ilivyokuwa awali kabla ya kuanzisha shule.
Katika shule hiyo ya darasa moja, Safi anafundisha watoto hao kusoma, kuandika na kuhesabu na tayari wameshaanza kuonyesha mwamko wa masomo.
“Ndoto yangu ni kuhakikisha shule hii inakuwa kubwa,” anasema Safi huku sura yake ikibadilika na kuonyesha masikitiko.
Hata hivyo, kama wahenga wasemavyo “ng’ombe wa maskini hazai”, baada ya miezi mitatu ya kufundisha, Safi alianza kuugua ugonjwa ambao hakuufahamu na akawa akipoteza fahamu na baadaye akawa haoni.
“Hali hiyo iliendelea kwa miezi kadhaa, hivyo nikashindwa kutimiza ndoto yangu ya kutoa elimu kwa watoto walioikosa,” anasema Safi.
Kukatishwa kwa ndoto ya Safi ndiyo kumesababisha watoto wapatao 200 kukosa elimu na kuendelea kuishi katika ujinga uliotopea.
Safi anasema anajisikia vibaya kuwaona watoto hao wakiishi bila elimu lakini anashindwa kufufua ndoto yake kwa sababu bado hali yake haijawa nzuri.
Kuzimika kwa ndoto hizo kumewagusa wazazi ambao walishakuwa wameanza kuona nuru ya maisha mapya ya watoto wao.
Miongoni mwa wazazi wanaoathirika kwa kukosekana kwa shule kisiwani humo ni Juma Kakozi, ambaye kazi yake kuu ni uvuvi katika ziwa hilo lenye kina kirefu kuliko yote barani Afrika.
Kakozi, mwenye mke mmoja na watoto wanane, ameshindwa kuwapeleka watoto wake shule kwa sababu ya uwezo mdogo wa kifedha na shule ya Safi ndiyo ilikuwa mkombozi pekee.
Mtoto wake wa kwanza ana umri wa miaka 15, lakini hadi sasa hajaandikishwa shule kwa sababu huduma hiyo muhimu haipo kisiwani hapo.
“Unawaona watoto wote hawa, nimeshindwa kuwasomesha kwa sababu hapa hakuna shule,” anasema Kakozi ambaye anafanya biashara ya samaki lakini fedha apatazo haziwezi kumudu gharama za usafiri wa watoto wake kwenda shule.
Kutokana na ukosefu wa shule katika Kisiwa cha Mvuna wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa, watoto hulazimika kukaa nyumbani na jamaa zao muda wa masomo. Picha na Elias Msuya
“Hata nikiamua kuwapeleka shule huko Kirando, nitalazimika kuwa na fedha za kuwalipia nyumba ya kupanga. Wenye nyumba wenyewe wanataka kodi ya kuanzia miezi mitatu hadi minne, nitapata wapi?”
Kakozi anawalaumu wanasiasa akisema wakati wa kampeni hutoa ahadi za kujenga shule kisiwani hapo, lakini uchaguzi ukiisha wanawatelekeza.
“Wagombea udiwani huja wakisema watatujengea shule, lakini uchaguzi ukiisha hawatujali tena. Watoto wote hawa mimi nitawapeleka wapi?” alihoji.
Mtoto wa kwanza wa kakozi, Asha Juma anaonekana kukata tamaa ya kupata elimu, akisema ameshasubiri kwa muda mrefu, lakini baba yake ameshindwa na hivyo ndoto yake kuyeyuka.
Baadhi ya wazazi wenye uwezo kidogo wa kifedha kisiwani hapo wamelazimika kuwapeleka watoto wao vijiji vya mbali ili wakapate elimu huku wao wakisalia kisiwani hapo kwa ajili ya uvuvi.
Ephraim Pondamali, mwenye watoto tisa, anasema amelazimika kuwapeleka Kijiji cha Kalungu ambako wanasoma shule ya Msingi ya Mkinga.
“Kazi yangu ni uvuvi wa kujikimu tu. Tusingeweza kukaa na watoto wote hapa kwa sababu hakuna shule, hivyo tuliamua kuwapeleka Kalungu angalau wapate elimu watusaidie baadaye,” anasema Pondamili.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Elias Mlea anasema kuna watoto zaidi ya 200 waliokosa fursa ya elimu kwa sababu ya kutokuwa na shule.
“Tumeshapeleka kero hii kwa mbunge wetu, Ally Keissy lakini nilimsikia kwa masikio yangu mwenyewe akisema kwa kuwa tumechagua viongozi wa Chadema, hatatusaidia,” anasema Mlea.
“Hiki kisiwa kimekuwepo enzi na enzi. Mimi nimezaliwa hapa na nimemkuta babu yangu akiishi hapa. Isitoshe, kisiwa hiki kinatambulika kisheria na ndiyo maana kuna uongozi na kila uchaguzi ukifika wanakuja hapa kupiga kampeni.
“Lakini sasa tunashangaa wanapotutaka tuondoke.”
Mwenyekiti wa tawi la CCM la Mvuna, King Mwaliwa anadai chama hicho kimeshindwa kutekeleza ilani yake ya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kutoa fursa ya elimu kwa wote.
“Utekelezaji wa ilani ya CCM hapa kisiwani haujafikia kiwango cha kuridhisha, kama unavyoona,” anasema.
“Hapa hatuna shule na tunao watoto wanaohitaji kusoma, hili ni tatizo na tulijaribu kuzungumza na uongozi wa wilaya na wa chama akiwemo Mwenyekiti wa Mkoa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Nkasi, lakini hadi sana hakuna mafanikio.”
Diwani wa Kipili, Wilbrod Chakukila ndioo anafuta kabisa matumaini ya wakazi hao kuwa na shule baada ya kueleza kuwa kisiwa hicho cha Mvuna si makazi ya kudumu.
“Kile ni kisiwa cha wavuvi. Mwaka 1974 wakati Mwalimu Nyerere akiwa Rais, aliwaondoa pale kwa sababu walikuwa wachache na waliishi kama wavuvi kwa sababu hawatapata huduma za jamii,” anasema Chakukila.
Pamoja na kuondolewa wakati huo, anasema watu wamerudi na kuweka makazi ya kudumu na wengine kuishi kwa msimu wa uvuvi.
“Ni kweli kwa sasa watu wapo wengi, lakini ni hao wanaoishi kwa uvuvi tu. Kwa hiyo pale si makazi, hata mbunge alishawaambia waondoke,” anasema.
Alipoulizwa sababu za kwenda kisiwani hapo kufanya kampeni wakati si makazi yanayotambulika kisheria, Chakukila anajibu:
“Ni kweli wakati wa kampeni tunakwenda kwa sababu kuna watu. Kampeni haijali idadi ya watu, hata pakiwa na nyumba mbili, mnakwenda tunatoa ahadi.
“Sasa utakwenda pale mtu atakuuliza ‘utatusaidiaje?’ Utafanyaje sasa? Siyo ahadi za uongo kwa sababu ukiishauri Serikali nayo inakupa mipango yake.”
Akizungumza kwa njia ya simu, mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy amesisitiza kuwa hakuna mpango wa kujenga shule wala zahanati katika kisiwa hicho kwa sababu si makazi rasmi ya binadamu.
“Mvuna ni kijiji cha wavuvi na hakina eneo la kujenga shule, ni makambi ya wavuvi,” anasema.
“Wewe si umefika pale? umeona hata sehemu ya kujenga choo pale? hakuna hata nusu ekari ya kujenga shule. Mimi nimezaliwa kule, ni kambi ya wavuvi.
“Kama wanataka huduma za jamii waende Kisiwa cha Mandakerenge kuna shule na zahanati. Nimeshawaambia wahame, hawasikii. Wengi wanatoka Congo DR, Burundi sijui na wapi,” anasema Keissy.
Hali ya elimu
Wananchi wa kijiji hicho wanataabika licha ya elimu kuwa ni haki ya msingi ya binadamu iliyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 11(2).
“Kila mtu anayo haki ya kujielimisha, na kila raia atakuwa huru kutafuta elimu katika fani anayopenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake,” kinasomeka kifungu hicho cha Katiba ya mwaka 1977.
Haki hiyo pia iko kwenye lengo namba nne la Malengo ya Maendeleo endelevu (SDGs) linalozizitiza kufanikisha Elimu ya Shule ya msingi kwa wote, kuandikisha watoto waliofikisha umri wa kwenda shule na na kuwawezesha wafaulu na kuendelea na elimu ya sekondari.
Kauli ya Mkurugenzi
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Julius Kaondo anakiri kuwepo kwa changamoto nyingi za huduma ya jamii katika wilaya hiyo kuliko uwezo wa kuzitatua.
“Tunazijua changamoto za upatikanaji wa huduma za jamii katika visiwa vya Ziwa Tanganyika, lakini uwezo wetu ni mdogo, hivyo tunazitatua hatua kwa hatua.
“Tuliwaelekeza wanaokaa kwenye maeneo ambayo hayana huduma ya elimu, wajenge ‘satellite schools’ (shule za mfano) madarasa ya awali halafu sisi tutaunga mkono.
Maeneo mengine wameshafanya, kwa mfano Kata ya Kala, kuna Kata ya Wampembe wamefanya, tukafanya harambee tukapata fedha ya kuwaunga mkono na bado tunaendelea,” anasema Kaondo.
No comments:
Post a Comment