Wednesday, September 20

Rita yazifuta taasisi 230


Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) imetangaza kuzifuta taasisi 238 za muunganisho wa wadhamini kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao pamoja na kushindwa kutoa taarifa za mabadiliko katika taasisi hizo.
Pia, sababu nyingine ni kutofanya marejesho ya wadhamini kwa kipindi kirefu baada ya kusajiliwa.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Msimamizi Mkuu wa Wadhamini wa Rita, Emmy Hudson imeeleza kuwa asasi hizo zimefutwa kutokana na kushindwa kutoa Maelezo ya kwanini zisifungiwe kufuatia  notisi ya siku thelathini.
Imeeleza kuwa hatua hiyo imetokana na Rita kuzifanyia uhakiki taasisii hizo na kubaini kuwa zinakiuka baadhi ya taratibu za kisheria ya asasi hizo ya mwaka 2002.
“Hatua hii imechukuliwa baada ya notisi ya siku 30 ya kusudio la kufutwa kuisha bila muunganisho wa taasisi au asasi hizo kutoa sababu za kutokufutwa kama kifungu 23(1)(d) cha Sheria ya Muunganisho wa Wadhamini,” imeeleza taarifa hiyo.
Kutokana na hatua hiyo, Rita imezitaka taasisi hizo kurejesha mara moja hati za usajili (certificate of Icorporation) za miunganisho ya wadhamini kulingana na kifungu cha 23(4) cha Sheria ya Miunganisho ya Wadhamini.

Pia, Rita imeueleza umma kwamba mali zote zilizokuwa chini ya usimamizi wa wadhamini wa asasi hizo zitawekwa chini ya usimamizi wa Ofisi ya Rita mpaka pale utaratibu mwingine utakapotolewa.

Hiyo ni mara ya pili kwa Rita kufuta taasisi za  Miunganisho ya Wadhamini kwa kipindi cha hivi karibuni ambapo awamu ya kwanza taasisi 181 zilifutwa.

Katika hatua nyingine, Rita imezitaka taasisi ambazo hazijafanya marejesho na hazijatajwa katika orodha kufanya marejesho haraka kabla hatua ya kuzifuta hazijachukuliwa.
“Taasisi zote ziendelee kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria na Katiba walizoziwasilisha wakati wa usajili,” imeeleza taarifa hiyo.
Baadhi ya taasisi hizo ni pamoja na Umoja wa Maendeleo na Huduma kwa Jamii Mkoa wa Dodoma, Chalinze Agricultural  Development Centre, Usambara Lishe Trust, Kibo Development Association, Wanawake Katika Kilimo, Ufugaji na Mazingira na Human Settlement and Services Trust Fund

No comments:

Post a Comment