Saturday, September 23

Polisi: Watu hawataki kufuata sheria


Kamishna wa Polisi Jamii, Musa Ali Musa amesema Serikali inaheshimu misingi ya utawala bora lakini tatizo lililopo ni kwamba watu hawataki kufuata sheria.
Akizungumza leo, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Amani duniani ambayo Kitaifa imefanyika Wilayani Temeke na kushirikisha asasi mbalimbali, mashirika ya kimataifa pamoja na Jeshi la Polisi viongozi wa dini.
Kamishna huyo amesema amani iliyopo hapa nchini haitakiwi kuchezewa na kwamba Jeshi hilo halitavumilia vitendo vya uvunjaji wa Sheria utokanao na itikadi za kisiasa, dini au makabila.
Amesema, nchi yoyote yenye amani, watu wake wanafuata misingi ya Sheria na taratibu za nchi hivyo ili kudumisha amani ni lazima kila mwananchi akubali kuheshimu sheria.
"Tanzania ni nchi inayoheshimu haki na misingi ya utawala bora lakini Kuna fikra imejengeka kuwa kuwa huru ni kufanya jambo lolote bila kufuata taratibu za nchi, "amesema
"Jeshi la Polisi litafanya lolote liwezekanalo ili amani iliyopo idumishwe."
Pia, ameonya juu ya usambazaji wa taarifa za kichochezi kupitia mitandao ya kijamii hasa vijana na kuwataka kujishughulisha na shughuli za maendeleo.
Ametolea mfano, Mlipuko wa mabomu ya  Mbagala ya mwaka 2014 na kusema kuwa licha ya kuwa ilikuwa bahati mbaya jamii ijifunze kuheshimu amani ili hali kama hiyo isije kujitokeza.
Mratibu wa Mtandao wa kutetea haki za watoto, GNRC, Yusuph  Masanja amesema ni muhimu kwa jamii kuheshimu haki za watoto ili kuwa na kizazi bora siku zijazo.

No comments:

Post a Comment