Polisi na kundi la waandamanaji waliokusanyika katika eneo la Mahakama Kuu mjini Nairobi wametimua mbio baada ya kuvamiwa na nyuki wanaodaiwa kuwadhuru watu kadhaa.
Tukio hilo limetokea wakati majaji wa Mahakama wakiongozwa na Jaji Mkuu, David Maraga wakisoma hukumu kamili kuhusu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Rais yaliyompa ushindi mgombea wa Jubilee, Uhuru Kenyatta.
Kulikuwa na hali ya taharuki wakati kundi la nyuki lilipovamia eneo hilo ambalo lilikuwa limezingirwa na askari wakiwa na magari ya doria.
Mmoja wa watu waliokuwepo eneo hilo ambaye ni mlemavu alipatiwa msaada kwa kuondolewa kwa gari la wagonjwa baada ya kujeruhiwa na nyuki hao.
Waandishi wa habari walikuwa sehemu ya waliotimua mbio wakinusuru maisha yao kutokana na uvamizi huo.
Kabla ya nyuki kuvamia eneo hilo, baadhi ya wafuasi wa Nasa walisikika wakiwashambulia kwa maneno askari waliokuwa wamezuia barabara kuelekea Mahakama Kuu.
Inadaiwa nyuki walikuwa wameweka maskani karibu na eneo hilo lakini hakuna aliyejua.
Kwa mujibu wa taarifa, kelele za waandamanaji ndizo zilizowafanya nyuki kutoka na kuwashambulia.
No comments:
Post a Comment