Saturday, September 23

Nyanduga: Serikali inawajibika kulinda haki ya watu kuishi


Hivi karibuni kumekuwa na hali ya wasiwasi wa usalama kutokana na matukio kadhaa ya mauaji, kutekwa, kupotea au kushambuliwa kwa risasi kwa wananchi.
Mapema mwaka huu kulitokea mauaji ya kuvizia katika Wilaya za Kibiti na Rufiji mkoani Pwani ambapo zaidi ya watu 40 wakiwamo askari Polisi waliuawa. Hata hivyo, mauaji hayo yalikuja kudhibitiwa kwa kuwakamata baadhi ya wahusika na wengine kuuawa.
Kabla ya mauaji hayo kulikuwa na tukio la maiti sita zilizookotwa kando ya mto Ruvu mkoani Pwani zikiwa ndani ya viroba mwishoni mwa mwaka 2016, huku na kupotea kwa kada wa Chadema, Ben Saanane.
Tukio la karibuni ni la kushambuliwa kwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu katika eneo la Area D mjini Dodoma Septemba 7, mwaka huu.
Kufuatia matukio hayo, Gazeti la Mwananchi limefanya mahojiamo maalumu na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga ambaye pamoja na mambo mengine, anasema hali ya usalama nchini ina changamoto kubwa kutokana na kutishiwa kwa haki ya kuishi. Endelea.
Swali: Naomba kupata historia ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na unaonaje upatikanaji wa haki hizo nchini kwa sasa?
Jibu: Tanzania imekuwa ni nchi iliyojikita katika kuheshimu haki za binadamu na hali hiyo imetoka na historia yake tangu tupate uhuru.
Katika tamko la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa anatangaza Tanzania kujiunga na Umoja wa Mataifa alisema nchi hii itakuwa inaheshimu Azmio la Ulimwengu la Haki za Binadamu.
Azimio lile lililokuwapo tangu mwaka 1948 linazungumzia mambo mengi zikiwamo haki za siasa na uraia, uchumi na kijamii na kiutamaduni na jinsi miaka ilivyokwenda zimetanuka zikahusisha haki za makundi.
Haki hizo zilikuja kuwekwa kwenye mikataba mbalimbali, kuna mikataba ya kikanda iliyokubalika katika Bara la Afrika.
Katika ngazi ya Taifa, haki hizi zilikuwa zinaheshimiwa tangu wakati huo, Mwalimu Nyerere aliona ili Taifa ambalo limetoka kutawaliwa lipate haki hizo, inabidi watu wawe huru, wafanye kazi na ndiyo maana kukawa na misemo kama uhuru na kazi, uhuru na maendeleo.
Yalikuwa ni matamko ya kisiasa lakini ni ya haki za binadamu. Sasa kitaifa haki hizi zilionekana kama matamko ya kisiasa, lakini zilikuja kuundwa taasisi za kuyalinda.
Mwaka 1965 Serikali ya awamu ya awamu ya kwanza iliunda Tume ya Kudumu ya Uchunguzi ambayo jukumu lake kubwa lilikuwa kuhakikisha watawala wanawatendea haki wananchi ndani ya misingi ya sheria. Kipindi kile kilikuwa cha mfumo wa chama kimoja, kwa hiyo ikaundwa ili kuwadhibiti viongozi.
Pale kiongozi wa umma anapozidi madaraka yake anawajibishwa.
Hapo mihimili kama Bunge, Mahakama ilikuwapo pamoja na Tume ile.
Hiyo iliendelea hadi mwaka 1984 ambapo haki za binadamu ziliingizwa kwenye Katiba. Mikataba ambayo Serikali iliibali iliingiza kwenye Katiba. Kulikuwa na mijadala iliyosababisha mabadiliko hayo.
Hakukuwa na mfumo wa kupata haki mpaka ilipoundwa sheria ya kuzitambua haki za msingi ilikuwa ikimwezesha mtu kama haki zile zikivunjwa aweze kuzidai mahakamani.
Inaendelea uk 24
INATOKA UK 23
Hiyo ilikuwa miaka ya 1990 na ilipofika mwaka 2001 ilianzishwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora ambayo ilianzishwa na ikawa mbadala wa Tume ya Uchunguzi. Hapo ikaongezewa majukumu, ikiwa pamoja na watumishi walioko ndani ya mipaka ya Serikali kuhakikisha wanafuata sheria na vilevile ikatoa fursa ya mwananchi kulalamika kwa kuwa hiyo ni haki ya msingi.
Majukumu ya Tume ni pamoja na kupokea malalamiko ya wananchi, kuyachunguza na kuyatolea mapendekezo. Nyingine ni kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na kuishauri Serikali pale inapoona misingi inavunjwa.
Swali: Kwa hiyo hali ya haki za binadamu ikoje kwa kipindi cha walau miaka miwili hadi sasa?
Jibu: Tuna maeneo au mafungu makubwa matano ya haki, kwa mfano, haki ya kuishi au uhai (haki mama), haki ya uhuru wa kwenda popote mtu anapotaka, fungu la uhuru wa maoni na kujieleza, haki ya kuabudu na imani, haki ya utu wa mtu yaani utu wako uheshimiwe, kuna haki ya ushiriki wako katika maamuzi yanayokugusa, au jinsi jamii inavyoendeshwa.
Vilevile kuna haki ya kupata huduma za msingi, haki ya kutambuliwa hasa pale kunapokuwa na unyonge katika hali au kundi kama watoto, wanawake, wazee, wote hawa wana haki.
Kwa ufupi naweza kusema haki hizi zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa na kuna maeneo ambayo kuna changamoto au hatujafanikiwa.
Swali: Hivi karibuni kumekuwa na matukio ya mauaji kama yale yaliyotokea wilaya za Kibiti na Rufiji mkoani Pwani, watoto kutekwa, maiti kuokotwa mtoni kwenye viroba na tumeona Mbunge Tundu Lissu akishambuliwa kwa risasi. Mnayachukuliaje matukio haya kwa kigezo cha haki ya kuishi?
Jibu: Cha msingi katika hilo kuna changamoto na ili kuiona kuwa ni changamoto ni vizuri tujue kwamba kimataifa, kwa sababu Tanzania siyo kisiwa, katika msingi wa jumuiya ya kimataifa, jukumu la usalama ni la Serikali.
Kutokana na hiyo dhana, kila mtu aliyeko ndani ya mipaka ya nchi, anastahili kulindwa haki yake ya uhai, na ndiyo maana kuna vyombo vya ulinzi na usalama.
Changamoto hii ukiichambua kwa matukio hayo uliyotaja moja moja, inabidi tuwe na maelezo ya kitaalamu yanayozungumzia taaluma ya ulinzi na usalama.
Kama Tume, tunasema kumekuwa na changamoto, lakini ni kwa nini changamoto zinajitokeza kwa maana kwamba utaona zinatokana na vyombo vyenye taaluma ya ulinzi.
Kama ni uhalifu ndiyo maana nikasema katika ile jukumu la Serikali, ni lazima vyombo vya ulinzi na usalama vishughulikie matatizo haya au changamoto hizi kwa misingi ya kisheria.
Kama watu wanauawa au kuna matukio ya vifo, kwa haki ambayo inapotea, ni lazima ipatikane sababu ya kiini. Dhana iliyopo ya utawala wa sheria, lazima sheria zitumike katika kujua tatizo ni nini na suluhu yake ni nini.
Baada ya mambo hayo ndiyo utajua tatizo la upatikanaji wa miili huko Mto Ruvu, mauaji ya Kibiti na mengineyo, panahitajika kufanyika uchunguzi wa kubainisha chanzo chake ni nini.
La msingi ni kwamba haki lazima ilindwe, sheria zifuatwe, kwa sababu kuna msemo unaosema, sheria ichukue mkondo wake.
Sasa sheria imetokea, ichunguzwe limetokana na nini chanzo chake kikijulikana sheria ichukue mkondo wake. Kuna dhana muhimu ambayo ni utawala wa sheria katika nchi inayojiendesha katika mfumo wa kidemokrasia na utawala bora. Ukiifuatilia kwa kiwango kikubwa unaweza kutetea haki za binadamu.
Swali: Pamoja na matukio hayo, kumekuwa na malalamiko ya ukandamizaji wa demokrasia na hapa tumeona vyama vya siasa vikilalamikia katazo la mikutano ya hadhara na maandamano lililotolewa na Serikali. Nini kauli yako?
Jibu: Kama tulivyosema awali, hizi ni changamoto zilizojitokeza ambazo, kweli Katiba na sheria zinatamka matamko yote ya haki hizo. Zinapotokea changamoto inatakiwa zizungumzwe na zitatuliwe.
Zimechukuliwa hatua kadhaa za kutafuta haki hizi kwa kwenda mahakamani kutafuta tafsiri ya sheria hizo.
Labda niseme kwenye utawala wa sheria na demokrasia na utawala bora, zinapotokea changamoto hizi, ni vizuri zitafutiwe tafsiri ya kikatiba.
Mnapokuwa na nchi ambayo mihimili inafanya kazi, mihimili hiyo inafanya kazi katika dhana ya ‘check balance’, mihimili inategemeana, lakini mhimili mmoja usiingilie mwingine. Huu ni utenganifu wa mihimili.
Inapotokea changamoto ya mhimili mmoja kuingilia mwingine, hatuna budi kufuata taratibu zinazowezesha kuchanganua kama mchanganyiko umetokea.
Katika haya, Katiba iko wazi, uhuru wa maoni upo, haki ya vyama kufanya mikutano, sasa ikishindikana mihimili kufanya kazi, itakuwa ni tatizo kubwa.
Lakini ninavyoliona, naamini kuna kesi zimefikishwa mahakamani zinazojaribu kuhoji, je mihimili inaingiliana? Kama haki ya vyama kufanya mikutano.
Sasa ni mpaka hapo mahakama zitakapotoa majawabu, ndiyo tutajua tafsiri.
Swali: Vipi kuhusu uhuru na mamlaka ya Tume hii? Mnawezaje kuiwajibisha Serikali ikiwa yenyewe ndiyo inawapa bajeti na inateua viongozi wake?
Jibu: Hizi tume ziko nchi nyingi tu na ziko hivihivi. Kwa sababu unaposema kuiwajibisha Serikali, sisi siyo polisi. Tume haifanyi kazi kama hivyo. Wananchi wanadhani ili uiwajibishe Serikali lazima utumie mabavu, utawala wa sheria unasema lazima liwe dude lenye maguvu.
Katika dhana ya uwajibikaji, mathalani, Tume inafanya kazi kwa kupokea malalamiko na kutoa mapendekezo. Ni tofauti na hukumu ya mahakama. Kwa maana ya kwamba amri ya mahakama inatekelezeka moja kwa moja, wakati pendekezo la tume lina utaratibu wa kutekelezwa.
Kwa maana kwamba anayeshauriwa anatakiwa achukue sheria ya kurekebisha.
Ni utaratibu wa kiutawala kwamba kwa sababu kuna sheria ambazo ni administrative (za kiutawala) na nyingine ni judicial (kimahakama), zile za kimahakama zinatakiwa ziheshimike.
Kwa hiyo Tume siyo Mahakama, lakini ikitoa mapendekezo lazima yaheshimiwe. Kutokuheshimika kwa mapendekezo ndiyo kunaifanya tume ionekane kama haina mamlaka.
Meno ya tume yanatokana na Katiba kwa sababu imeundwa na Katiba, kwa hiyo usipotekeleza maana yake huheshimu Katiba.
Pili, mapendekezo yale yasipotekelezwa yanaweza kuwekewa sheria. Kwa hiyo Tume imepewa mamlaka hayo ili iweze kutekeleza utawala bora.
Mara nyingi malalamiko yanayohusu uvunjifu au kukiuka madaraka au utendaji. Kwa hiyo yule anayelalamikiwa anatakiwa atekeleze kwa sababu uchunguzi wa tume utakuwa umejua ni kigezo gani kilichovunjwa.
Kwa hiyo kutotekeleza ni namna ya kutowajibika, ni kutowajibika kwa sababu anawajibika kufuata sheria.
Suala la kulipwa mshahara na Serikali wala isingekuwa kigezo, kwa sababu mbona Mahakama wanalipwa na Serikali? Mbona majaji wanateuliwa na Serikali? Hilo wala wananchi wasifikirie hivyo.
Kitu cha msingi ni kujiuliza, je, Tume inafanya majukumu inayotakiwa kufanya? Je, inapotoa mapendekezo yanatekelezwa katika dhana ya kuheshimu sheria na uwajibikaji?
Sasa hapo suala la msingi ambalo wenye mamlaka au wale wanaolalamikiwa zaidi wajue kwamba kutekeleza maelekezo ya Tume haina maana kwamba lazima ifike hatua ya kupelekana mahakamani.
Kwa hiyo unaposema tume haina meno haimaanishi kwamba inafanya kazi kama polisi kukuweka rumande, bali inafanya kazi kwa kuheshimu sheria.
Tume hii haiko chini ya kitu chochote, iko huru na imeundwa na Katiba, inapokea malalamiko ya wananchi na kutoa mapendekezo. Kwa hiyo haipokei maagizo kwamba usifanye hiki au ufanye hiki, inafanya kazi kwa mujibu wa Katiba.
Swali: Hivi karibuni Tume yako ilitoa tamko baada ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kutoa kauli za kejeli kwa wananchi wasiokuwa na mapenzi na chama tawala (CCM), lakini kauli kama hizo zinaendelea kutolewa na viongozi wengine walioko madarakani na hamkemei?
Jibu: Nadhani kama ni mizania uko huru kutupima, mimi siko hapa kutetea kila kitu. Hilo sitaliingilia.
Pili, nimekwambia kuna kesi zinazoulizia uhuru wa vyama vya siasa na kesi zikishaingia mahakamani sisi hatuingilii. Lakini, unaweza kuweka mizania, kwa sababu siyo kila kitu kikitokea unatoa tamko.
Kuna vitu vya msingi tunavyozungumzia, hatufanyi kazi kwa vyombo vya habari tu. Suala la Mkapa tulizungumzia kwa sababu ya dhana. Kuna suala la ushirikishwaji, kuheshimu hoja za kila mtu, lakini linapoonekana linakuwa la jamii, la kukwaza watu na hasa linapojirudia, maana lilianza mwaka 2015, sasa utauliza mbona lilipotokea hamkutoa tamko?
Watanzania tusiwe watu wa kusukuma majukumu, ibara ya 26 ya Katiba inawataka Watanzania kuilinda katiba hiyo.
Wajibu wa kulinda na kutetea Katiba lisiwe la Chadema au tume tu, ni la kila raia, ni wajibu wa msingi wa kila raia kuilinda Katiba.
Kama hatuna utamaduni wa kuitetea tunangoja wengine tunakuwa hatuitendei haki Katiba.

No comments:

Post a Comment