NA AZIZA MASOUD – DAR ES SALAAM
KITENDO cha Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), kuwasilisha kusudio la kutaka kuwasilisha muswada binafsi wa mabadiliko ya Katiba bungeni ili kuongeza ukomo wa Bunge, kimepingwa vikali na baadhi ya wasomi na wanasiasa, huku baadhi yao wakidai huenda akawa anatafuta umaarufu.
Nkamia aliwasilisha kusudio hilo ofisi za Bunge kwa mujibu wa kanuni ya 81(2) ya kanuni za Bunge toleo la 2016.
Katika barua yake aliyoisaini Septemba 12, mwaka huu na kuwasilishwa ofisi ya Katibu wa Bunge Dodoma, ameeleza kusudio lake la kuwasilisha muswada huo aliouita Muswada Binafsi wa Sheria ya Mabadiliko ya 15 ya Katiba.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana, Mhadhiri wa Masuala ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema pamoja na kwamba ni mawazo binafsi, lakini anapaswa kutoa sababu za msingi za marekebisho hayo yatakayokuwa kinyume na Katiba iliyopo.
“Lazima tuangalie mawazo haya kayatoa kwa muktadha gani, huenda ana lengo la kujitafutia umaarufu ili na yeye aonekane kaingiza agenda fulani katika jamii, huyu mtu aliwahi kuwa naibu waziri, isije ikawa anabembeleza nafasi ya uwaziri,” alisema Dk. Bana.
Alisema sababu zinazofanya kuwe na uongozi wa miaka mitano zilizotolewa na Watanzania bado zipo hai, hivyo kama angekuwa muungwana angepeleka hoja ya nafasi ya ubunge kutozidi miaka 10.
Pia alisema Nkamia alipaswa ajitafakari kabla ya kuwasilisha kusudio hilo kwa kuwa hoja ya kuongeza muda wa urais ilishakataliwa na Rais Dk. John Magufuli, hivyo asitafute sababu ya kuibadili.
“Maoni yake hayaakisi uhalisia hata kidogo, Watanzania tuna Katiba na bado haijabadilika, asitake ajiwekee mazingira ya kuonekana anampigia chapuo rais,” alisema Dk. Bana.
Naye mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Mwesiga Baregu, alisema kauli ya Nkamia inaonyesha nchi ilivyo na wanasiasa waroho wa madaraka.
“Hizi ni kauli za wagonjwa na walevi wa madaraka, hilo suala lipo ndani ya Katiba, sasa labda kama atakuwa na sababu ya msingi ya kuhitaji mabadiliko hayo atuambie, lakini mimi sijaridhika, sioni kama kuna sababu,” alisema Baregu.
Alisema masuala ya ukomo wa Bunge yalishazungumziwa katika Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba mpya, kwamba ukomo wa rais ulipaswa kuwa vipindi viwili wakati Bunge vipindi vitatu.
Profesa Baregu alisema misingi ya demokrasia ni kuchochea mawazo mapya na maoni tofauti, lakini suala la ukomo wa umri na mihula ni ugonjwa katika nchi za Afrika.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia ni wakili wa kujitegemea, Profesa Abdallah Safari, alisema kitendo cha Nkamia kutoa kauli hiyo katika nchi za demokrasia kama Tanzania, kinamfanya kumwona wa ajabu.
“Namwona ni mtu wa ajabu, nchi zote zenye demokrasia kama Uingereza na Marekani, wana awamu nne za urais, lengo ni kumfanya kiongozi asibweteke.
“Mawazo aliyoyatoa ni uhuni wa kutaka kuwa masultani na hii si kauli yake, lazima kuna mtu atakuwa amemtuma,” alisema Profesa Safari.
Alisema Tanzania haiwezi kuiga mfano wa Rwanda kwa kuwa nchi hiyo inaendeshwa kinyume na sheria za kimataifa.
Naye Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Charles Rwechungura, alisema Nkamia anaweza kufanikisha suala hilo endapo atakuwa na sababu za msingi.
“Mimi nadhani tuone kwanza sababu zake za kutaka mabadiliko, labda ana sababu za msingi, lakini pia akiweza kuwashawishi wabunge basi sisi wananchi hatutakuwa na jinsi,” alisema.
Kwa upande wake, Nkamia, alishangazwa na kitendo cha nyaraka hiyo aliyoita ya siri kusambaa katika mitandao ya kijamii na alikiri kuwasilisha kusudio hilo na kusisitiza kuwa ataweka wazi sababu za kufanya hivyo muda utakapofika.
“Ni kweli nimewasilisha kusudio hilo na nitatoa sababu muda utakapofika, lakini mmenishangaza hiyo nyaraka ni ya siri na bado ilikuwa katika ngazi ya kiofisi, sijui imefikaje uko kwenu,” alisema Nkamia.
No comments:
Post a Comment