Katika kesi hiyo iliyovuta wananchi wengi waliojitokeza nje ya jengo la Mahakama, makosa matatu yanawahusu washtakiwa wanane na moja la kwanza linawahusu wote tisa.
Mbali ya Musukuma ambaye ni mshtakiwa wa nane; wengine ni Steven Werema ambaye ni mshtakiwa wa kwanza na ni mwananchi wa kawaida.
Wengine ni madiwani, Costantine Morandi, Winfrida Malunde, Ngudungu Joseph, Martin Kwilasa, Adija Said, Michael Kapaya na Maimuna Mengisi (anashtakiwa kwa kosa la kula njama pekee).
Mbele ya Hakimu Mkazi, Ushindi Swalo Wakili wa Serikali, Emil Kiria amedai washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka manne. Wakili mwingine wa upande wa mashtaka ni Hezron Mwasimba.
Mbali na kosa la kula njama, wanadaiwa pia kufanya kusanyiko lisilo halali, kufunga barabarana kusababisha wafanyakazi wa mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) kushindwa kuingia kazini na kufanya uharibifu wa mali.
Wanadaiwa Septemba 13 saa nne asubuhi katika ukumbi wa Gedeko ulioko katika Halmashauri ya Mji wa Geita walitenda kosa la kula njama ya kutenda kosa kinyume cha kifungu cha 386 (1)(e) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa mapitio mwaka 2002.
Katika kosa la pili wanadaiwa Septemba 14 saa 12:00 asubuhi katika Mtaa wa Mtakuja walifanya kusanyiko lisilo halali kinyume cha kifungu cha 74(1) na cha 75 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa mapitio mwaka 2002.
Washtakiwa katika kosa la tatu wanadaiwa kufanya kizuizi kwenye barabara ya umma kinyume cha kifungu cha 239 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa mapitio mwaka 2002 .
Wanadaiwa Septemba 14 saa 12:00 asubuhi katika Mtaa wa Mtakuja wilayani Geita walitenda kosa kwa kufunga barabara inayoingia GGM na kusababisha wafanyakazi wa mgodi kushindwa kufika kazini siku hiyo.
Mbele ya Hakimu Swalo, washtakiwa katika kosa la nne wanadaiwa kufanya uharibifu wa mali kinyume cha kifungu cha sheria namba 326(6A)(a) na (6B) (e) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa mapitio mwaka 2002.
Wanadaiwa saa 12:00 katika Kijiji cha Nungwe kwa nia ovu waliharibu bomba linalosambaza maji katika bwawa la Nyankanga na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh12 milioni.
Upande wa mashtaka umedai hali hiyo ilisababisha shida ya maji katika mgodi wa GGM na kwa wananchi wa mji wa Geita.
Washtakiwa wanaotetewa na mawakili Deo Mngengeli na Neema Christian walikana kutenda makosa hayo na wako nje kwa dhamana.
Hakimu aliwataka kuwa na mdhamini mmoja kila mmoja atakayesaini bondi ya Sh5 milioni. Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 10 itakapotajwa.
No comments:
Post a Comment