Saturday, September 2

Mufti atumia baraza la Eid el Hajj kusisitiza amani


Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limewataka waumini kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa.
Akizungumza leo Septemba Mosi wakati wa baraza la Eid el Hajj lililofanyika katika Msikiti wa Taqwa, Ilala Bungoni jijini Dar es Salaam, Mufti wa Tanzania Sheikh Mkuu, Abubakar Zubeir amesema ni jukumu la kila muumini kudumisha amani kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo.
Mufti amesema hakuna kinachoweza kufanyika bila kuwepo amani na kwamba, Mtume Muhammad (S.A.W), ilisisitiza amani.
Amewataka walimu wa madrasa na maimamu kusimamia miongozo inayojenga amani, umoja na kupendana miongoni mwao kwa kuwa hakuna neema wala baraka zilizowahi kutokea popote duniani kama wananchi hawasimamii misingi hiyo.
“Mtume Muhammad (S.A.W) alikataa kufarakana kwa sababu ndani yake kuna mabaya, haijawahi kutokea baraka na neema ndani ya kufarakana,” amesema.
Amewataka waumini kila mmoja kuwa mlinzi wa amani popote alipo kwa kuwa hakuna mbadala wake, wala shughuli yoyote ya maendeleo inayoweza kufanyika bila amani.
Pia, ameeleza kusikitishwa na baadhi ya taasisi zilizochukua fedha za waumini kwa ajili ya kuwasafirisha kwenda hija lakini ikashindwa kufanya hivyo.
Mufti amesema wametoa miezi sita kwa taasisi hizo, zikiwemo Twaiba na Jamarat kurejesha fedha za waumini waliokwama kusafiri ili mwakani waweze kwenda hija.
Mgeni rasmi katika baraza hilo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi amewataka waumini kuendelea kuliombea Taifa. Pia amesisitiza suala la amani.
Dk Mwinyi amesema maendeleo ya nchi yanategemea ustawi wa amani, hivyo ikikosekana hata ibada zinazoendelea kufanyika hazitawezekana.

No comments:

Post a Comment