Kuna baadhi yao wamepitia katika mazingira magumu na yenye kukatisha tamaa lakini walisimama na kila walipoanguka walijitahidi kunyanyuka tena.
Consoler Eliya ni mama mlezi wa watoto wa wa kituo cha ‘New Hope for Girls’ aliyepitia mateso, manyanyaso, kupigwa kila mara katika familia aliyokuwa akiishi.
Kwa zaidi ya miaka saba mlo wake haukuwa wa uhakika, sehemu pekee aliyojihakikishia kupata chakula ni jalalani.
Akiwa na miaka 11 alinusurika kuolewa na mwanaume mchuuzi wa magazeti aliyetafutiwa na mama yake mdogo huku akiambiwa kuwa mtoto wa kike akijua kusoma na kuandika inatosha.
Pamoja na yote aliyoyapitia alisimama na kuweka nia kuwa ni lazima afanikiwe na afikie kile anachokihitaji kupitia elimu ili awasaidie watoto wa kike wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kama aliyoyapitia.
Baada kusoma kwa shida na kufanikiwa kumaliza shahada ya Sosholojia kuna mtu alivutiwa na huduma anayoitoa kwa watoto wa kike hivyo alimpatia udhamini wa kusoma shahada ya uzamili ya ‘Social Work’. “Baada ya kusoma niliamua kufanya utafiti wa wasichana wanaoishi katika mazingira magumu na matatizo wanayoyapita ambao uliniwezesha kugundua mambo mengi,” anasema Consoler.
Apata ulemavu wa kudumu
Kutokana kupigwa mara kwa mara alipata ulemavu wa kudumu wa mgongo na kichwa uliosababisha afanyiwe upasuaji mkubwa.
“Nikiwa kidato cha kwanza nilipigwa shuleni kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 11 jioni ikiwa ni baada ya mama mdogo kuja kusema kwa walimu kuwa namfanyia makusudi ya kujitapisha mbele ya mama na kukojoa kitandani jambo ambalo lilikuwa bahati mbaya,” anasema.
Anasema baada ya kupigwa alikaa siku tatu bila kupata huduma ya matibabu jambo lililosababisha damu kuvilia ndani ya kichwa na kuweka usaha katika baadhi ya maeneo.
“Mwaka 2009 nilifanyiwa upasuaji mkubwa wa mgongo na madaktari kutoka Marekani lakini sikuweza kutengamaa na mwaka 2013 nilipelekwa India kufanyiwa upasuaji wa kichwa kutokana na maumivu makali niliyokuwa nayapata na kunisababishia kushindwa kuona vizuri,” anasema Consoler.
Mara ya mwisho aliambiwa na madaktari kuwa hatakiwi kuajiriwa, kuolewa, kupanda daladala wala bodaboda kutokana na hali yake ya afya.
Kuanza kulea watoto
Anasema daima alikuwa mtu wa kupenda kuwasaidia watoto waliokosa tumaini na kuishi katika mazingira magumu, kwa kuwapatia upendo walioukosa kutoka kwa wazazi na elimu ili waweze kufikia malengo yao.
Alipenda kuwa mama wa watoto wa kike wenye matatizo na alipofika kidato cha sita alikuwa akikutana na mtoto wa kike anaishi katika mazingira magumu aliahidi kumsaidia ingawa alikuwa hajui atawasaidia vipi.
Mwaka 2005 akiwa chuoni alianza kuhudumia wasichana saba kwa kutumia mkopo aliopewa aliweza kuwarudisha shule, watano kati yao alikuwa akiishi nao chuoni na wawili walikuwa wakiishi na kaka yake mkubwa.
Anasema hadi hivi sasa ameweza kusaidia watoto zaidi ya 200 huku 18 kati yao wakiwa tayari wamemaliza masomo na kufanya kazi sehemu mbalimbali nchini. Wapo walioolewa na wengine wakijitegemea wenyewe.
Anasema wasichana wengine wanne wamemaliza chuo kikuu, wawili wamemaliza vyuo vya kati na mmoja yupo chuoni.
Wasichana wanne wapo kidato cha tano na sita, wanne wanasoma elimu ya ufundi stadi huku wengine wakisoma elimu ya msingi na sekondari.Anasema kutokana na hali ya maisha na ukubwa wa nyumba anayotumia, anaishi na wasichana 34 nyumbani kwake kama sehemu ya familia na kuwapatia kila hitaji wanalotaka.
“Watoto wengine wanaishi katika maeneo tofauti jijini hapa kwa misaada ya wananchi jambo linaloendelea kumtia moyo,” anasema Consoler.
Changamoto
Anasema kuishi na wasichana hao kuna changamoto nyingi anazozipitia kwa sababu wanatoka katika mazingira tofauti, dini na hata makabila.
Asilimia kubwa wamekuwa na tabia ngumu na humchukua hata miaka minne hadi sita katika kumrudisha katika mstari ulionyooka huku silaha kubwa anayoitumia katika kufanikisha jambo
“Kuna wakati wanaumwa hata watoto 17 kwa wakati mmoja jambo linalotulazimu kuangalia wale wenye hali mbaya zaidi ndio tunawapatia dawa za malaria huku wengine walio katika hatua za awali tunawapatia dawa za kupunguza maumivu,” anasema Consoler.
Anasema wanafanya hivyo kwa sababu ya kukosa fedha za kutosha kununua dawa kwa ajili ya watoto wote kwa wakati mmoja.
Pia, anasema watoto wanaokolewa sio wote wanaenda katika shule za kawaida wengine walikuwa tayari wamemaliza darasa la saba na kufaulu kidato cha kwanza lakini wanakosa nafasi ya kwenda shule kwa wakati kutokana na kuchukuliwa kufanya kazi za ndani.
“Kuna mwingine anaweza kusema nilifaulu lakini uwezo wake ni mdogo hivyo tunachokiangalia tunampima kwa kumpa karatasi na kumwambia ajielezee hapo ndio tutaweza kutambua uwezo wake na kumtafutia shule,” anasema Consoler.
Anasema wakiona mtoto anajua kujieleza na nia ya kusoma anayo analazimika kumtafutia shule binafsi na kuingia makubaliano nao.
“Mara nyingi huwa naandika maelezo ya mtoto, hali anayoishi na kuomba niruhusiwe kulipa ada kidogo kidogo katika muda wote atakaosoma hapo na mara nyingi nimekuwa nikikubaliwa,” anasema Consoler.
Mbali na kusoma wengine pia wamekuwa wakilazimika kusubiri nyumbani mpaka pale wadhamini wanaojitokeza ili waweze kupata ada ya kuwalipia.
Alisema mpaka sasa hawajaweza kupata makazi ya kudumu ila tayari wamepata eneo la ekari 9 katika eneo la Kibaha ambalo amepanga kujenga kijiji kitakachoweza kuchukua wasichana wengi Zaidi kutoka Tanzania nzima.
“Ingawa bado hakujapimwa lakini tuliweza kufuatilia na kuambiwa ni eneo salama ambalo halijaweza kuvamiwa na watu na tunasubiri tu lipimwe na mipango miji,” anasema Consoler.
“Kwa sasa hata akitokea mtoto mwenye uhitaji sana nitashindwa jinsi ya kumsaidia na siwezi kuishi naye kutokana na eneo nililopo sasa,” anasema Consoler.
Anasema mume wake amekuwa msaada mkubwa sana katika kumuunga mkono katika mambo anayoyafanya jambo linaloendelea kumtia moyo.
Kama umeguswa kusaidia watoto hawa wasiliana na Consoler Eliya 0715 025 565.
No comments:
Post a Comment