Sunday, September 17

Mdee kuongoza mazishi ya diwani Chadema


Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Halima Mdee ataongoza mazishi ya aliyekuwa diwani wa viti maalumu Mbeya Mjini,Ester Mpwiniza yatakayofanyika kesho.
Taarifa ya Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, Obadia Mwaipalu imesema mbunge huyo Ijumaa jioni alianguka nyumbani kwake na alipelekewa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya alikofariki dunia kutokana na shinikizo la damu.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amesema Mpwiniza aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Bawacha Wilaya ya Mbeya Mjini, alikuwa kiunganishi ndani na nje ya chama hicho, hivyo wameamua kumzika kesho Jumatatu.
Amesema uamuzi huo unalenga kutoa nafasi kwa wageni kuhudhuria maziko  wakiongozwa na viongozi wa kitaifa watakaoingia Mbeya leo Jumapili.
“Mama Mpwiniza alikuwa kiongozi mkubwa ndani na nje ya chama, hivyo hatuwezi kuharakisha maziko yake. Tunasubiri viongozi wa kitaifa akiwamo Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Halima Mdee na viongozi wengine. Sijajua makaburi atakakopumzishwa lakini itakuwa ni hapahapa Mbeya Mjini,” amesema Sugu.
Amesema awali walipanga shughuli zote za msiba huo zifanyike Mtaa wa Ghana kwa ndugu wa marehemu lakini baadaye familia ilihamishia kwenye nyumba yake aliyokuwa akiijenga eneo la Iyela jijini hapa.
Mwenyekiti wa Chadema, Mbeya Mjini Mwaipalu amesema, pia wanasubiri utaratibu wa ndugu za marehemu ukamilike.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mchungaji Peter Msigwa ametuma rambirambi kwa familia ya marehemu, ofisi ya Meya wa Jiji la Mbeya, Chadema na wananchi kwa jumla.

No comments:

Post a Comment