Vyama hivyo ni AFP, DP, Demokrasia Makini, UPDP, Chama Cha Kijamii (CCK), ADC, TLP, UMD, NRA, ADA Tadea, Sauti ya Umma (SAU) ambapo vimesema mbali na tukio la Lissu, pia wameitaka Serikali kutafuta ufumbuzi wa uhalifu katika maeneo ya ofisi za mawakili.
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi wakati wa mkutano na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam walipokutana kutoa tamko la kuishinikiza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuongeza muda katika utoaji wa maoni kuhusu sheria mpya ya vyama vya siasa nchini.
“Hata Rais na Watanzania wengi hawakufurahishwa na tukio hilo, tunaungana pia na Bunge na Rais aliyezungumza hadharani, akaagiza watafutwe wachukuliwe hatua. Nadhani kuna mambo mengi kwa pamoja tunatakiwa kuwa na kauli moja kama Watanzania, tutatoa tamko la pamoja kuhusu hali hiyo kisiasa na hali ya usalama wa raia,” alisema mwenyekiti wa umoja huo, Renatus Muhabi.
Katika hatua nyingine, vyama hivyo vimekubaliana kufuta mapendekezo yake katika mchakato wa kuandaa sheria mpya ya Vyama vya Siasa baada ya mchakato huo kutumia muda mwingi bila kuendelezwa huku wakiachwa nyuma bila kushirikishwa katika hatua inayoendelea kwa sasa.
Muhabi aliwaambia waandishi wa habari tayari wameshawasilisha nakala ya barua hiyo kwa msajili na nyingine wakiwasilisha ofisi ya waziri mkuu na Baraza la Vyama vya Siasa.
Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza alipoulizwa kuhusu hilo amesema ni kweli barua ya vyama hivyo wameipokea. Kuhusu hoja ya kupewa rasimu, Nyahoza amesema hakuna rasimu yoyote iliyoandaliwa hadi sasa na ndiyo maana ya kuwataka watoe maoni yao.
“Wao watupatie maoni yao, unatoa maoni ndiyo unatengenezewa rasimu, halafu unapewa uangalie kilichoandaliwa,” amesema Nyahoza.
No comments:
Post a Comment