Nairobi, Kenya. Mahakama ya Juu kesho inatarajiwa kutoa maelezo kamili kuhusu hukumu ya kihistoria ya kesi ambayo ilisababisha kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika Agosti 8.
Wanasheria wa vyama mbalimbali vya siasa walitaarifiwa jana kuhusu kutolewa kwa hukumu nzima kazi itakayoanza saa 4.00 asubuhi. Kutokana na uamuzi wa majaji wengi, mahakama hiyo iliamua kufuta ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta ikitaja dosari kadhaa na kukosekana uhalali wakati wa kutuma matokeo.
Jaji Mkuu David Maraga, Makamu wake Philomena Mwilu, majaji Smokin Wanjala na Isaac Lenaola walifuta uchaguzi huo Septemba 1 mwaka huu na kuamuru Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuandaa uchaguzi mwingine ndani ya siku 60 kama inavyosema Katiba.
Lakini majaji wawili JB Ojwang na Njoki Ndungu walitupilia mbali kesi hiyo iliyofunguliwa na kiongozi wa muungano wa Nasa, Raila Odinga. Pia na wao watatoa maoni yao kesho.
Tayari IEBC imetangaza Oktoba 17 kuwa siku ya uchaguzi wa marudio lakini sintofahamu imejitokeza kuhusu tarehe hiyo.
Joto limeanza kupanda mitaani kwani leo asubuhi mamia ya wafuasi wa Jubilee waliandamana nje ya Mahakama ya Juu wakiishutumu kwa “kuiba ushindi wao.”
Wakinyanyua mabango na vipeperushi, waandamanaji hao wengi wao vijana walilalamikia majaji waliotoa hukumu hiyo kwamba haikuwa halali.
No comments:
Post a Comment