Sunday, September 17

Lissu alivyoufunika mkutano wa Bunge


Mkutano wa Nane wa Bunge la Kumi na Moja umemalizika huku tukio la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu likifunika mambo mengine manne muhimu yaliyojitokeza.
Lissu alijeruhiwa Septemba 7 akiwa kwenye gari nyumbani kwake Area D na kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alikopatiwa huduma ya dharura kabla ya kuhamishiwa Nairobi, Kenya kwa matibabu zaidi kwa kile ambacho familia na wabunge wenzake wa upinzani walikieleza kuwa ni kuhofia usalama wake.
Tukio hilo na mengine yaliyoambatana nalo yameonekana kujadiliwa zaidi kiasi kufunika shughuli nyingine za vikao vya Bunge.
Shambulio hilo liliwashtua na kuwaogofya wabunge kiasi cha Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe kuomba mwongozo wa Spika Septemba 8 akisema tukio kama hilo halijawahi kutokea katika historia ya nchi.
Bashe alisema linaogofya kwa sababu matukio mengine yaliyolitangulia ya kupotea kwa Ben Saanane ma kutishiwa bastola kwa Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, hawajasikia taarifa zozote ya vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu waliohusika hayo.
Alishauri kwamba kwa kuwa matukio hayo yameharibu heshima ya Taifa, Kamati ya Bunge ya Mambo Nje, Ulinzi na Usalama ikutane na vyombo vya ulinzi na usalama ili wapate taarifa iliyojitosheleza.
“Hali inavyoendelea hakuna mwenye uhakika na maisha yake ya kesho. Dhamana tuliyopewa na chama chetu na wananchi ni kulinda usalama, mali na raia wa nchi hii,” alisema Bashe.
Spika wa Bunge, Job Ndugai alikubaliana na hoja hiyo na kuipa kamati hiyo inayoongozwa Mbunge wa Muheza, Adadi Rajab jukumu la kufuatilia suala hilo na mengine ambayo ni tishio la usalama, lakini hadi mkutano huo unamalizika juzi Ijumaa, haikuwa imekamilisha kazi hiyo.
Mbali ya kazi ambayo kamati hiyo imekabidhiwa, wakati akiahirisha Bunge, Spika Ndugai aliwataka wabunge kuwa makini na usalama wao kwa kuacha kwenda katika maeneo ambayo ni hatari na pia kuwashauri wapigakura wao kuwa makini.
Hata Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akitoa hoja ya kuliahirisha Bunge, alizungumzia kwa kirefu suala hilo akisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vitahakikisha vinawakamata waliohusika na shambulio hilo.
Mbali na suala la Lissu kujitokeza kama hoja mahsusi, suala la kushambuliwa kwake liliendelea kulitikisa Bunge kwani mawaziri na wabunge kwa nyakati tofauti, walikuwa wakiliunganisha wakati wakichangia hoja mbalimbali.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi alisema Serikali imeunda kikosi kazi kinachoshirikisha vyombo vyote vya ulinzi kwa ajili ya kushughulikia matukio hayo na kukusanya silaha za kivita.
Kauli hiyo ilikuja baada ya Mbunge wa Chambani (CUF), Yusuf Salim Hussein kusema kuna matatizo ya matumizi silaha za kivita ambazo kisheria zinatakiwa kumilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kutolea mfano tukio hilo la Lissu.
Licha ya Lissu kuzungumzwa mara kwa mara ndani ya Bunge, pia katika mitandao ya kijamii na hasa baada ya taarifa rasmi kutolewa bungeni Septemba 8, mijadala kuhusu tukio la kushambuliwa kwale ilitawala mingine ikitoka kwa wabunge ambao hawakuwapo Dodoma.
Kutokana na uzito wa mashambulizi hayo, Spika Ndugai alilazimika kuwajibu baadhi yao na kuibua mvutano mpya ambao pia ulikuwa gumzo kuliko hata shughuli nyingine za Bunge.
Miongoni mwa wabunge walioingia katika mvutano na Spika hadi kupelekwa kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ni Saed Kubenea (Ubungo-Chadema) ambaye akiwa katika Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima alikaririwa akisema kuwa Spika alisema uongo kwa idadi ya risasi alizopigwa Lissu.
Spika pia akijibu hoja ya mtandaoni, alitangaza kumsamehe Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akitumia hoja iliyoibua mjadala zaidi kuhusu gharama za kukodi ndege iliyomsafirisha Lissu kwenda Nairobi.
Lema aliandika kwenye mtandao wa kijamii, akisema Bunge limekataa kugharamia matibabu ya Lissu nje ya nchi lakini Spika akasema anamsamehe kwa kuwa wakati wa tukio hilo hakuwapo Dodoma.
Pia Spika alisema Dola 9,200 za Marekani za kukodi ndege iliyompeleka Lissu Nairobi, zililipwa na Mbunge wa Mpendae (CCM), Salim Hassan Turky.
Madai hayo yalimwibua Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa ambaye kupitia mtandao wa kijamii alitoa stakabadhi kuthibitisha kwamba Chadema ndiyo iliyolipa fedha hizo huku akumshutumu Ndugai.
Hoja hiyo ilimwibua Turky ambaye alisema hakulipa fedha hizo bali aliidhamini Chadema kwa kuwa anafahamiana na mmiliki wa ndege hiyo.
Waziri, Naibu Waziri ajiuzulu
Kama si suala la Lissu, pengine tukio kubwa zaidi katika mkutano huo lingekuwa kujiuzulu kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani baada ya kutajwa kwenye ripoti za kamati za Bunge zilizoundwa kuchunguza biashara za madini ya almasi na Tanzanite.
Mawaziri hao walijiuzulu wakiwa bungeni Dodoma na taarifa zao kutolewa bungeni baada ya Rais John Magufuli kukabidhiwa ripoti hizo na kuwataka viongozi waliotajwa kukaa pembeni wakati wanachunguzwa.
Rais alipokea ripoti hizo, siku moja baada ya wenyeviti wa kamati hizo kukabidhi uchunguzi wao kwa Spika katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge.
Wabunge na kamati ya maadili
Mbali na Kubenea, pia Ndugai alimpeleka mara mbili katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT - Wazalendo), Zitto Kabwe kutokana na kauli zake kwenye mitandao ya kijamii.
Kiongozi huyo wa ACT – Wazalendo alipelekwa mbele ya kamati hiyo baada ya kusema kwamba Bunge limewekwa mfukoni na mhimili fulani wakati alipotoa maoni kuhusu ripoti hizo za almasi na Tanzanite.
Mbali na shutuma hizo, mbunge huyo alindika katika akaunti yake ya Twitter kwamba, “Hatujawahi kuwa na Spika anayedhalilishwa na Rais kwamba aliuliza wajumbe gani awaweke kamati za uchunguzi za Bunge.”
Pia anadaiwa kusema; “Wabunge wazoefu tulikuwa na matumaini makubwa na Spika Ndugai, tulimpigania dhidi ya njama za kumhujumu kutoka Ikulu. Anatuangusha... Spika Ndugai amekuwa Spika wa kwanza katika historia ya nchi yetu kushuhudia mbunge anapigwa risasi Mkutano wa Bunge ukiendelea,” baada ya kauli hizo, ndipo Spika alipolitangazia Bunge kwamba Zitto apelekwe kwa mara ya pili katika kamati hiyo kuhojiwa kwa kulidharau Bunge.
Wabunge CUF waapishwa
Mkutano huo ulianza kwa kuwaapisha wabunge viti maalumu wa CUF upande wa Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama, Profesa Ibrahim Lipumba, walioteuliwa kuziba nafasi za wenzao waliofutwa kutoka kambi ya Katibu mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad. Wabunge wa Ukawa walisusia tukio hilo.

No comments:

Post a Comment