Monday, September 11

Kikosi maalum chatua Mwadui kuchunguza almasi


Kikosi Maalumu cha upelelezi kinachoundwa na maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam tayari kimeanza kazi ya kuchunguza shughuli za uzalishaji na biashara ya madini ya almasi katika mgodi wa Mwadui unaomilikiwa na kampuni ya Williamson Diamonds Limited.
Kutokana na mahojiano yanayoendelea, shughuli za mgodi huo ulioko Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga zimesimama kuanzia juzi kutoa fursa kwa viongozi na watumishi wa vitengo nyeti vinavyosimamia uchimbaji, uthamini na usafirishaji kuhojiwa.
Akizungumza kwa njia ya simu leo Jumatatu asubuhi Agosti 11, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Tellack amethibitisha uwepo wa kikosi kazi hicho mkoani humo na kufafanua kuwa shughuli za mgodi huo zitarejea kama kawaida baada ya mahojiano kukamilika.
“Hawajafunga mgodi; kinachofanyika ni mahojiano na uchunguzi unaofanywa na maofisa wa ngazi za juu kutoka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama. Yakikamilika shughuli zitarejea kama kawaida,” amesema Tellack
Licha ya kuthibitisha uwepo wa kikosi kazi hicho mkoani mwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule amesema hawezi kuzungumzia utendaji wake kwa sababu linahusisha na kusimamiwa na maofisa kutoka makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam.
Bila kutaka kuingia kwa undani kuhusu suala hilo, ofisa uhusiano wa mgodi huo, Joseph Kaasa ameliambia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa yuko kituo cha polisi na kuahidi kutoa taarifa atakapokamilisha kulichompeleka kituoni hapo.
Kampuni ya WDL juzi imesitisha kwa muda baadhi ya shughuli za uzalishaji mgodini.
Uongozi wa kampuni hiyo katika taarifa kwa wafanyakazi iliyotolewa juzi Jumamosi kwa tangazo namba 3311 imesema kwa mtazamo wa uchunguzi ulioanzishwa na Serikali na kwa sababu za kiusalama, umeamua kusitisha kwa muda baadhi ya shughuli za uzalishaji katika mgodi.
Taarifa hiyo imesema shughuli ambazo zitaendelea ni za huduma maalumu za ulinzi, tiba, umeme, maji, zimamoto na usafiri unaohitajika katika huduma hizo.
“Huduma za kiutawala zitaendelea kufanya kazi. Tutawajulisha wakati uzalishaji utakaporejea,” imesema .
WDL imesema inasubiri kuachiwa kifurushi namba WI-FY18 cha almasi iliyokuwa ikisafirishwa nje kutoka mgodini.
Hata hivyo, serikali imezuia kusafirishwa kifurushi hicho kwa misingi ambayo haijawasilishwa rasmi kwa uongozi wa kampuni ya WDL isipokuwa kwa taarifa zilizotangazwa na vyombo vya habari vya redio na runinga.
Hatuwezi kutoa maoni yoyote kutokana na matokeo ya uchunguzi huo. Vifurushi vyote vinavyosafirishwa kwa biashara nje hukadiriwa thamani yake hapa mgodini na watumishi wa Tansort (Hiki ni kitengo cha kukadiria thamani ya almasi na vito) ambao wanawakilisha Wizara ya Nishati na Madini. Kifurushi kinaposafirishwa kinapigwa mihuri miliwiili ya vyombo viwili vya serikali.
Sisi kama uongozi hatuna ujuzi wanaotumia tansort wa kukadiria na kuthamini au kukokotoa thamani ya alimasi. Huwa tunapokea hati ya ukadiriaji kutoka tansort ambayo hutumika kukadiria kwa muda malipo ya mrabaha wa serikali. Malipo ya mrabaha yanakamilishwa baada ya kupatiwa matokeo halisi ya zabuni ya wazi ya almasi za WDL (uaminifuunaothibitishwa na tansort) kutoka Wizara ya Nishati ana Madini.
kama mnavyotambua, serikali ni mbia asilimia 25 katika WDL. Tupo kwenye mazungumzo na serikali ili kuafikiana njia ya kufuata.
Tunawashukuru kwa kuendelea kutoa ushirikiano na kuelewa.

No comments:

Post a Comment