Wakati Profesa Mukandala akisema yeye ndiye afisa masuhuri wa taasisi hiyo, PAC ilisema anayetakiwa kuwajibika kwa masuala hayo ni mwenyekiti wa Baraza la Udsm.
Hiyo ilitokea jana baada ya wabunge kubaini kasoro katika taarifa za hesabu za UDSM, hasa ujenzi wa maduka ya Mlimani City na kuhoji sababu za mwenyekiti huyo kutoenda pamoja na uongozi wa chuo mbele ya kamati.
Hata hivyo, PAC ililazimika kuahirisha kikao hicho cha kupitia hesabu za taasisi hiyo baada ya mwenyekiti huyo, Peter Ngumbullu kutohudhuria.
Wabunge pia walihoji sababu za wakuu wa idara kuwakilishwa kwenye kikao hicho.
Baada ya mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka kutaka kujua sababu za mwenyekiti huyo kutofika, makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema barua ya wito iliwaelekeza waje na mhasibu, ofisa ugavi na wakuu wengine wa idara ambao anaona watamsaidia kujibu hoja za ukaguzi.
“Kwa hiyo naomba msamaha wako mheshimiwa mwenyekiti. Labda sikuelewa vizuri lakini mimi nilifuata maelekezo ambayo tulikuwa tumepewa,” alisema Profesa Mukandala.
Kutokana na majibu hayo, Kaboyoka alitaka kumjua ofisa masuhuri na kujibiwa na Profesa Mukandala kuwa kwa kawaida ni makamu mkuu wa chuo.
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Aeshi Hillaly alisema ni lazima mwenyekiti huyo afike mbele ya kamati hiyo.
“Sijui kama ulikuwa umejipanga. Lakini aliyekuwa anatakiwa kujibu hapa ni ofisa masurufu ambaye ni mwenyekiti. Sasa sijui kama uliamua kuja mwenyewe ili kutukomoa sisi ama ulipata barua yenye maelekezo haya,” alisema Aeshi.
Alisema kikao hicho kisingeweza kuendelea kwa sababu kutokuwepo kwa mwenyekiti wa bodi.
Mbunge wa Nyamagana (CCM), Stanslaus Mabula alihoji sababu za kuwepo watu wanaokaimu na kushauri kuwa siku ya kikao kingine wafike wakuu wa vitengo husika.
Naye Profesa Mukandala aliwahakikishia wabunge hao kuwa katika uongozi wakati amekuwa akitii mamlaka na hasa pale anapoamriwa kufanya jambo kwa maandishi.
“Kwa hiyo nikiri kwamba hata mimi nilishangaa barua haikumtaja mwenyekiti kwa sababu mara zote nilipoitwa na kamati hii, nilikuja na mwenyekiti na hata wakati mwingine nilifikiria kumwambia makamu mwenyekiti,” alisema.
Lakini Kaboyoka alisema:“Mnajua kuwa kuna mambo ambayo hayaendi sawa, sikuona sababu yoyote kwamba mmekuja bila mwenyekiti wa baraza. Mnajua hapo nyuma kuna mambo mengi sana mmekiuka ambayo mlipewa na kamati hii ya Bunge, sijui kama mnajua mamlaka ya kamati hii.
“CAG ndio jicho letu, akileta hapa si ni sehemu ya Bunge kwa sababu tumepewa dhamana ya kupitia na kutoa maelekezo na wahusika wanapaswa kutekeleza.
“Kutokana na hayo tunawapa hadi keshokutwa mje kwenye kamati na mwenyekiti ndio tutaweza kujadiliana.”
Pia Kaboyoka aliagiza maofisa wote watakaofika kesho wawe waliopewa dhamana na si wanaokaimu kama walivyojitambulisha jana.
“Hesabu zenu zimekaa ndivyo sivyo kwa hiyo tunataka kufanyia kazi, kamati ipate muda wa kujikita zaidi siku ya kesho (leo) na kesho kutwa (kesho),” alisema.
No comments:
Post a Comment