Saturday, September 2

Bomoabomoa ni pasua kichwa


Sakata la bomoabomoa katika maeneo mbalimbali ya wakazi wa Toangoma, Bonde la Msimbazi na Kimara mkoani Dar es Salaam limeonekana kuwagonganisha viongozi wa Serikali.
Wachambuzi wameelezea hali hiyo kuwa inatokana na sheria kutofuatwa na baadhi ya viongozi serikalini.
Mgongano huo umetokana na uongozi wa juu serikalini kutengua uamuzi wa ngazi ya chini kwa kile ambacho wachambuzi wamedai ni kukosekana kwa mawasiliano ya operesheni hizo.
Bomoabomoa iliyoanza Agosti 16 mwaka huu, katika eneo la Kimara hadi Kiluvya kwa zaidi ya nyumba 1,000 yakiwamo mahekalu ya vigogo, nyumba za ibada na vituo vya mafuta, imesitishwa juzi kwa baadhi ya nyumba ambazo zina kinga ya Mahakama.
Bomoabomoa nyingine ya nyumba zipatazo 300 zilizokuwa zimeshawekwa alama ya X katika Bonde la Makamba lililopo Kata ya Toangoma, ilizuiwa juzi baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kusema ameagizwa na Rais John Magufuli kufanya hivyo.
Siku hiyo alitoa agizo kama hilo kwa nyumba zaidi ya 17,000 za Bonde la Msimbazi ambazo zilikuwa katika mpango wa kubomolewa huku nyingine zikiwa zimewekwa alama ya X tangu mwaka jana.
Makonda alisema Rais Magufuli ameshangazwa na bomoabomoa hizo huku akidai kuwa hata ofisi ya mkuu wa mkoa nayo haikuwa na taarifa.
Katika ufafanuzi wake, Rais aliagiza kusitishwa kwa ubomoaji wa nyumba za baadhi ya wakazi wa Kata ya Toangoma, Temeke ambao ungezikumba zaidi ya nyumba 300 kutokana na madai ya kujengwa katika eneo tengefu la Serikali kwa ajili ya kuendeleza ukanda wa kijani maarufu kama “Bonde la Makamba.”
Lakini utata umeibuka katika utaratibu uliotumika kwenye ushirikishwaji wa ngazi za uamuzi kabla ya operesheni hizo kufanyika.
Hali hiyo imeonekana kuyumbisha mamlaka ya viongozi wa Serikali katika uanzishaji wa opeshereni hizo kabla ya kutenguliwa.
Makonda alisema kutokana na utapeli na uuzaji holela wa viwanja katika eneo hilo la Toangoma, hakuna atakayebomolewa nyumba, wakati Agosti 29, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaviva aliwataka waliojenga nyumba kwenye bonde la hifadhi lililotengwa kwa ajili ya kuendeleza ukanda huo wa kijani kuondoka kwani si sehemu salama kwa makazi.
“Mimi nimekuja kuwaambieni ukweli kwamba maeneo mliyojenga si halali na hamstahili kujenga, pia mmeharibu mazingira kitu ambacho hakikubaliki,” alisema Lyaviva alipozungumza na wakazi wa eneo hilo huku mkurugenzi wa manispaa hiyo akitoa notisi ya wiki moja waondoke.
Lakini juzi, Makonda aliwaambia wananchi hao, “Inawezekana kuna baadhi ya watu wanafanya zoezi hili ili kumchonganisha Rais na wananchi, wamechelewa. Hakuna nyumba itakayobomolewa kwenye mkoa wangu, nasitisha zoezi la ubomoaji kuanzia sasa.”
Alipoulizwa kuhusu kusitishwa kwa ubomoaji wa nyumba 17,000, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Nemc, Dk Vedast Makota alisema hakuwa na taarifa rasmi, lakini akaahidi kutoa ufafanuzi baada ya kujiridhisha. “Jambo la msingi ni kwamba sisi kama Serikali tunawasiliana lakini ngoja nipate taarifa ili tusikie anasema nini, ndiyo nitaweza kutoa majibu,” alisema juzi.
Maoni ya wadau
Wakizungumzia mgongano huo baadhi ya watetezi wa haki za binadamu na wanazuoni nchini walisema mkanganyiko huo wa maagizo ya bomoabomoa unaonyesha namna ambavyo baadhi ya mambo yanafanywa bila kufuata utawala wa kisheria.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema mkanganyiko unaojitokeza kuhusu bomoabomoa hiyo unaonyesha namna ambavyo baadhi ya viongozi wasivyofuata utawala wa kisheria.
Dk Bisimba alisema kama sauti ya Rais kuhusu kusitishwa kwa bomoabomoa Msimbazi imesikiliwa, uamuzi wa mahakama ulipaswa pia kusikilizwa mapema kwa sababu upo kwa mujibu wa sheria.
“Mfano ni kule Kimara, watu walikimbilia mahakamani na maamuzi yakatoka kwamba bomoabomoa isitishwe, lakini iliendelea. Sasa hii inaonyesha kwamba hakuna utaratibu wa kisheria na hii hali ni hatari zaidi,” alisema.
Hata hivyo, bomoabomoa hiyo ilisitishwa na Tanroads baada ya kupokea amri hiyo ya Mahakama huku ikisema kwamba iliendelea na operesheni hiyo kutokana na kuchelewa kuipokea.
Dk Bisimba hakuwa peke yake katika hilo. Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema kwa sababu katika eneo la Kimara, ilishatolewa amri ya Mahakama ya kusitishwa ubomoaji Serikali ilipaswa kutii mara moja.
Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Dk Jimson Sanga alisema ni sheria kufuata sheria na kwamba kama Mahakama ilitoa oda ya kusitishwa kwa bomoabomoa lakini Tanroads hawakutii wanapaswa kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema ipo hatari wananchi wanapogundua kuwa hata kama wakikimbilia mahakamani kupata haki hawasikilizwi.
“Unapowaumiza wananchi kwa ajili ya kuwanufaisha wengine kwa maana ya kuwaletea maendeleo, ni lazima kuangalia pia mustakabali wa wale uliowaumiza. Kama Rais Magufuli anavyoeleza kila siku, wananchi wanyonge wanapaswa kuhurumiwa,” alisema.
CCM yazuia bomoabomoa Tanga
Wakati hayo yakiendelea jijini Dar es Salaam, sakata la uwekaji alama za X katika nyumba zinazotakiwa kubomolewa jijini Tanga kupisha upanuzi wa reli limeingia sura mpya baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga kuingilia kati na kusema hazitabomolewa kwa sababu hakikushirikishwa.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Henry Shekifu alisema jana kuwa kamati ya siasa imeketi na kufikia uamuzi wa kuamuru ubomoaji huo usitishwe hadi wafahamishwe na wananchi washirikishwe.
Akizungumza na wanahabari jana, Shekifu alisema kamati ya siasa iliketi juzi na kujiridhisha kuwa uwekaji wa alama za X haukufanyika kwa kufuata taratibu hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi.
“Tumezungumza na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela na ametuhakikishia kuwa kuna dosari katika zoezi zima la uwekaji wa alama za X hivyo nachukua nafasi hii kuwaomba radhi waliokumbwa na zoezi hili,” alisema Shekifu.
Uwekaji wa alama za X ulianza mwezi uliopita kwa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco) kutoa notisi ya mwezi mmoja kwa wamiliki wa nyumba zilizopo mitaa ya Usagara, Chuda na baadaye mjini Muheza, Korogwe na Mombo.
Majengo mbalimbali yakiwamo makazi, hoteli za kifahari, maghala na viwanda viliwekewa X ikiwa na kupewa siku 30 kuhakikisha zimevunjwa.
Kitendo hicho kilizusha malalamiko kutoka kwa wananchi ambao walieleza kushangazwa kwao na hatua hiyo kwa sababu walimilikishwa na mamlaka zenye kuhusika na masuala ya ardhi na wanalipia kodi kila mwaka.
Imeandikwa na Kelvin Matandiko, Tumaini Msowoya, Cledo Michael, Hidaya Nyanga na Burhan Yakubu     

No comments:

Post a Comment