Monday, August 28

Wilaya yahamishia wanafunzi bwenini kuongeza ufaulu



Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Samwel Jeremiah

Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Samwel Jeremiah 
Wazazi na walezi wenye watoto wa kidato cha pili na cha nne katika Shule ya Sekondari Ifekenya wilayani Songwe, wametakiwa kuanzia leo Agosti 28 wahakikishe watoto wao wanahamia mabwenini ili kutoa muda mzuri kwao kujiandaa na mitihani ya kitaifa itakayofanyika Novemba.
Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Samwel Jeremiah ametoa agizo hilo alipozungumza na wazazi, walezi na wanafunzi wa shule hiyo baada ya ofisi yake kupeleka vitanda 12, magodoro 22, magunia mawili ya mahindi na maharage kilo 100 ili kuwawezesha wanafunzi hao kufanya vizuri katika mitihani yao.
Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Songwe, Rowllens Kabuje amesema kwa miaka mingi wilaya hiyo imekuwa ikifanya vibaya katika ufaulu wa wanafunzi kutokana na asilimia kubwa ya wazazi ambao ni jamii ya wafugaji na wachimbaji madini kutotilia mkazo elimu.
Amesema muda mwingi wanafunzi wamekuwa wakijihusisha na masuala ya kuchunga mifugo na wengine kujiingiza kwenye uchimbaji wa madini ya dhahabu, huku wakipata msukumo huo kutoka kwa wazazi na walezi wao.
Kabuje amesema, “Tunashukuru tumepata kiongozi mwenye kuthamini elimu na hata sisi wakuu wa idara tumekuwa tukiunga mkono juhudi zake.”
Kabuje amesema Halmashauri ya Songwe imeanza kugawa vifaa vya maabara katika shule nne za sekondari ili kuhakikisha wanatekeleza kaulimbiu ya ‘Ondoa ziro Songwe’.

No comments:

Post a Comment