Hali ya kawaida imeanza kurejea katika miji mingi nchini Kenya baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa Ijumaa.
Watu wanaonekana kupuuza wito kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga wa kususia kazi leo kuomboleza watu waliouawa katika makabiliano kati ya polisi na waandamanaji waliokuwa wanapinga matokeo ya uchaguzi wa urais.
Wiki iliyopita, biashara nyingi zilifungwa watu wakihofia kuzuka kwa fujo kutokana na uchaguzi uliofanyika Jumanne.
Baadhi ya maeneo yakiwemo mitaa ya Mathare na Kibera jijini Nairobi na maeneo ya magharibi mwa Kenya yakiwemo Kisumu, Homa Bay na Migori.
Tofauti na hali ilivyokwa Ijumaa, biashara zimeanza kufunguliwa na magari ya uchukuzi wa abiria yameanza kufanya kazi katika barabara nyingi.
Baadhi ya wakazi mtaani Kibera wameambia BBC kwamba wanahitaji kufanya kazi kujipatia chakula na mahitaji mengine ya kimsingi.
Lakini wengine wameamua kutekeleza ushauri wa Bw Odinga na kususia kazi.
Bw Odinga, aliyewania urais kupitia muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) amekataa kukubali matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC).
Rais Kenyatta alipata kura 8, 203, 290 ambayo ni asilimia 54.27 naye Bw Odinga akapata kura milioni 6,762,224 ambayo ni asilimia 44.74.
Muungano wa Nasa umedai mitambo ya tume ya uchaguzi ilidukuliwa na matokeo kuchakachuliwa kuhakikisha Bw Kenyatta anashinda.
Msimamo wa muungano huo unaenda kinyume na waangalizi wa kimataifa kutoka Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Madola, miongoni mwa wengine, ambao walisema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.
Viongozi hao wa upinzani wamesema hawataenda kortini kupinga matokeo hayo.
Akiongea Jumapili katika mitaa ya Kibera na Mathare, Bw Odinga aliahidi kutangaza hatua zitakazochukuliwa na muungano huo Jumanne.
No comments:
Post a Comment