Thursday, August 24

Utumishi


Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya ajira kwa utumishi wa umma Bw. Malimi Muya akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani ) mapema leo Jijini Dar es Salaam kuhusu upatikanaji wa fursa za ajira kwa walemavu kulia ni Mkuu wa kitengo cha mawasiliano katika sekta hiyo Bi.Riziki Abrahamu
Picha Na Paschal Dotto-MAELEZO

Na. Georgina Misama, Agness Moshi - MAELEZO
Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Sekretariati ya Ajira Katika Utumishi wa Umma imewashauri walemavu kuchangamkia fursa za ajira zinazotolewa Serikalini kwani ni haki yao ya msingi kama ilivyo kwa watanzania wengine.

Akiongea na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi Wa Umma Riziki Abraham amesema Serikali inawahamasisha walemavu kuchangamkia fursa za ajira zinazotangazwa na Ofisi hiyo kwa sababu ni wachache wanaojitokeza.

“Mwamko wa walemavu katika uombaji wa ajira ni mdogo, ninawahamaisha kutuma maombi yao endapo wametimiza vigezo bila kuogopa changamoto zinazowakabili kwa sababu mchakato wote wa ajira unafanywa kwa kufuata kanuni na Sheria za Nchi ambayo inampa kila mtu haki ya kupata ajira”,Alisema Riziki.

Sheria namba 9  ya Ajira ya mwaka 2010 inasema “ Mwajiri yoyote awe wa Umma au Binafsi mwenye waajiriwa kuanzia 20 na kuendelea lazima asilimia 3 ya waajiriwa hao iwe kwa ajili ya watu wenye ulemavu” hii  inaonyesha kuwa walemavu wana haki ya kuajiriwa mahali popote.

Bi.Riziki amesema ni vyema walemavu kuzitaja changamoto zao kweye fomu za maombi ili Ofisi iweze kuwaandalia mazingira rafiki kwa ajili ya mchakato mzima wa upatikanaji wa ajira na baada ya kupata ajira waweze kupangiwa sehemu ambazo hazitakua changamoto kwao.

Aidha Serikali inawapa kipaumbele walemavu kuanzia wakati mchakato wa usajili hadi wakati wa kupanga ajira hivyo basi walemavu wenye vigezo vilivyoanishwa kwenye matangazo ya ajira wajitokeze kutuma maombi ya nafasi hizo.

Naye, Katibu Msaadizi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi Wa Umma Malimi Muya amesema kuwa Walemavu wanahaki kisheria hivyo waachane na mawazo ya kudhani wakitaja changamoto zao kwenye maombi hawatapatiwa nafasi.

“Serikali yetu haina ubaguzi kwenye utoaji ajira ukiwa na vigezo tutakuchukua, kuna upendeleo tunawapa walemavu kulingana na changamoto zao kama vile kuwaongezea muda wakati wa usaili, kuwatafutia wataalam wa mawasiliano na kuwaandalia mazingira rafiki wakati wa usaili kwa kuzingatia changamoto zao”, alisema Malimi.

Aidha Bw.Muya ameongeza kuwa Serikali inatambua nafasi ya Walemavu katika kuchangia maendeleo ya Nchi na ina wahamasisha kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza ili kujikwamua kiuchumi.

Ofisi ya Rais, Sekretariati ya Ajira Katika Utumishi wa Umma ina jukumu la msingi la kuendesha mchakato wa ajira kwa niaba ya waajiri mbalimbali na hatimaye kuwapangia vituo vya kazi wanaofaulu usaili.

No comments:

Post a Comment