Saturday, August 5

TASAF YASHIRIKI MAONYESHO YA NANE NANE KANDA YA KATI DODOMA.


Na Estom Sanga-TASAF 

Vikundi vya baadhi ya Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF kutoka mikoa ya Dodoma, Pwani Manyara na Singida vinashiriki kwenye maonyesho ya nane nane yaliyoanza mwanzoni mwa wiki hii mjini Dodoma. 

Vikundi hivyo vilivyoko kwenye banda la Ofisi ya Rais kwenye eneo la maonyesho la Nzuguni nje kidogo ya mji wa Dodoma, vinaonyesha bidhaa zilizotengenezwa na vikundi hivyo baada ya kuwezeshwa na TASAF ikiwa ni njia mojawapo ya kuinua shughuli za uzalishaji mali na kuongeza mapato ya walengwa wa Mpango huo wenye lengo la kusaidia jitihada za serikali za kuwapunguzia wananchi kero ya umasikini. 

Bidhaa zinazotengenezwa na vikundi hivyo na ambazo zimeletwa kwenye maonyesho hayo ni pamoja na sabuni na mafuta ya manukato ambavyo vimetengenezwa kwa kutumia mmea wa mwani ambao humea kwenye maeneo ya baharini. 

Bidhaa nyingine ambazo zimezalishwa na vikundi hivyo vya walengwa wa TASAF ni pamoja na asali,ubuyu,mafuta ya alizeti na mifuko bora ya kuhifadhia nafaka ambavyo vimetokana na kazi za mikono ya walengwa hao ikiwa ni maojawapo ya sharti la kuzifanya kuinua uchumi na kujiongezea kipato kwa njia ya vikundi. 

Walengwa hao wamepongeza hatua ya serikali kupitia TASAF kuwashirikisha kwenye maonyesho hayo kwani hatua hiyo inasaidia kutangaza shughuli za uzalishaji mali zinzofanywa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini ambao wanahitaji masoko ya bidhaa wanazozizalisha ili kukuza uchumi wao. 

“hii ni hatua muhimu katika kutangaza vikundi vya uzalishaji mali ambavyo kimsingi havina uwezo wa kutangaza bidhaa kupitia vyombo vya habari kutokana na gharama zake”amesema mwenyekiti wa kikundi cha uzalishaji asali cha Juhudi kutoka Kongwa mkoani Dodoma bwana Augen Lekas Makanda. 

Katika maonyesho hayo yaliyofunguliwa na Mkuu wa mkoa wa Singida, Dokta Rehema Nchimbi,TASAF pamoja na mambo mengine imekuwa ikitoa ufafanuzi wa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini pamoja na matumizi ya malipo kwa walengwa na kutumia utaratibu wa kielektroniki kama njia mojawapo ya kuboresha huduma zake kwa walengwa. 

Zifuatazo ni baadhi ya picha za wananachi wanaotembelea banda ya maonyesho la TASAF lililoko kwenye jengo la ya Ofisi ya Rais kwenye viwanja vya Nzuguni nje kidogo ya mji wa Dodoma.
 Baadhi ya maafisa wa TASAF wakitoa maelezo kwa wanafunzi waliotembelea banda la maonyesho la TASAF kwenye viwanja vya nane nane ,Nzuguni nje kidogo ya mji wa Doodoma.
 Mmoja wa walengwa wa TASAF kutoka kikundi cha Wakulima wa Mwani Msichoke cha Bagamoyo akitoa maelezo kwa wananchi waliotembelea banda la TASAF. Kikundi hicho kimewezeshwa na TASAF na sasa kinatengeza sabuni na mafuta kutokana na zao la mwani kama njia ya kujiongezea kipato.
Mtaalam wa Mawasiliano wa TASAF Bi. Zuhura Mdungi akitoa maelezo kwa baadhi ya watu waliotembelea banda la maonyesho la TASAF lililoko kwenye jingo la Ofisi ya Rais kwenye eneo la Nzuguni nje kidogo ya mji wa Dodoma.

 Mmoja wa maafisa wa TASAF, Bi. Grace Kibonde akitoa maelezo kwa baadhi ya watu waliotembelea banda la TASAF kwenye maonyesho ya nane nane  kwenye eneo la Nzuguni  nje kidogo ya mjini Dodoma
 Mmoja wa wajumbe wa kamati ya maandalizi ya Nane Nane kanda ya kati  Bi.Tabu Ally Likoko akipata maelezo kutoka kwa walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya masikini ambao wameunda kikundi cha kuzalisha sabuni na mafuta kwa kuwezeshwa na TASAF .
 Baadhi ya wanafunzi wakipata maelezo ya namna shughuli za TASAF zinazvyotekelezwa kutoka kwa watumishi  wa taasisi hiyo inayotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini nchini.

No comments:

Post a Comment