Wednesday, August 23

Sumaye atumia dakika 71 kutema nyongo


Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Frederick

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni  Katibu wa kanda hiyo, Casmir Mabina. Picha na Said Khamis 
Dar es Salaam. Amewahi kusema na ndio msimamo wake, lakini jana alionekana kama anataka aeleweke zaidi anamaanisha nini alipozungumza na waandishi wa habari.
Kutekeleza hilo, mwenyekiti wa Chadema wa Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye alitumia dakika 71 kuweka bayana msimamo wake, hasa wakati huu ambao ameshapoteza mashamba mawili makubwa yaliyotwaliwa na Serikali kwa maelezo kuwa hakuyaendeleza.
Pia alitumia dakika hizo kujibu hoja zilizotolewa na Serikali kuhalalisha kufuta hati za umiliki wa mashamba hayo, akiitaka iweke wazi sababu hizo, huku akiweka msimamo kuwa pamoja na hayo yote, hatarejea CCM.
“Kunyang’anywa mashamba haya ni uamuzi wa juu,” alisema waziri huyo mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu.
“Wanataka nirudi CCM, lakini mimi siwezi kurudi CCM hata kidogo. Kwa nini wananilazimisha? Nilieleza sababu siku ya kuihama CCM.”
Sumaye, ambaye kabla ya CCM kupitisha mgombea urais alisema angekihama chama hicho kama kingempitisha mla rushwa, alisema sababu za kuondoka chama hicho ni pamoja na kuhitaji mabadiliko nje ya CCM na kukifanya chama hicho kikongwe kizinduke.
Akijikita katika mashamba, Sumaye alisema sababu zilizotolewa wakati wa kufuta hati ya umiliki hazina ukweli, na kwamba utaratibu wa kisheria alioutumia kudai haki yake mahakamani, haujaheshimiwa.
Alisema shamba la Mabwepande lililokuwa la kwanza kufutiwa hati,  alilinunua mwaka 1999 kwa mzee  aliyemtaja kwa jina la Abdallah Kimberete kabla ya kupatiwa hati kwa jina la Frankline Frederick Sumaye mwaka 2002.
Sumaye alisema shamba hilo liliendelea kulimwa mazao mbalimbali hadi mwaka 2007 wakati Serikali ilipotoa tangazo la kulitambua eneo la Mabwepande kuwa eneo la mipango miji na hivyo kuzuia kilimo na badala yake kusubiri Serikali kutoa utaratibu.
“Tulipanga kujenga chuo kikuu kwa ubia na watu wengine wa ndani na nje, lakini wakati tunapanga mipango hiyo, Septemba 2015, shamba hilo na mengine ya viongozi wa CCM yalivamiwa,” alisema.
“Tulitoa taarifa polisi, lakini kilichoshangaza wavamizi waliondolewa katika mashamba ya viongozi wa CCM tu ila kwangu wakaachwa. Nilienda ofisi za wilaya na mkoa, lakini sikupata msaada na simu zangu (nilizowapigia) wakawa wanazima.”
Sumaye alisema shamba hilo lilimfanya akutane na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) wakati huo, Ernest Mangu lakini hakupata msaada na ndipo alipofungua kesi Mahakama Kuu.
Alisema kilichosikitisha zaidi, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni alipoingia madarakani, alisema shamba hilo litafutwa na kugawiwa wavamizi.
“Oktoba 27 mwaka jana, Waziri wa Ardhi (William Lukuvi) aliwaambia waandishi wa habari kuwa Serikali inawataka wananchi wasivamie maeneo yanayomilikiwa kihalali na hata kama hayajaendelezwa, waiachie Serikali ifanye kazi yake. Lakini akasema suala langu tayari walishatoa notisi ya kulifuta,” alisema.
Sumaye alihoji maswali manne; kwa nini Serikali haikuwaondoa wavamizi kwa miezi 14 na baadaye ikawaambia wasiondoke kwamba watakabidhiwa maeneo, na ni kwa mazingira gani angeweza kuliendeleza shamba hilo katikati ya mgogoro wa wavamizi?
Sumaye alihoji pia, ingewezekanaje kuendeleza eneo hilo ndani ya notisi ya siku 90 alizopewa? na ni kwa nini Serikali ilimpa notisi ya shamba hilo mwaka mmoja kabla ya kuvamiwa?
Kuhusu shamba la mkewe, Esther lililopo wilayani Mvomero, Sumaye alisema alilinunua katika Chama cha Msingi cha Ushirika cha Morogoro.
Baada ya kushindwa kulipa deni la mkopo, chama hicho kiliamua kuliuza kisheria na Esther Sumaye akalinunua.
Hata hivyo, Sumaye alisema Rais alipita Mvomero na kuagiza apelekewe orodha ya mashamba yote yasiyoendelezwa ili ayafute, shamba hilo halikuingia kwenye orodha ila baadaye mkuu wa mkoa huo alipewa maagizo kutoka juu ili hati ifutwe.
Akijibu tuhuma hizo, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema hoja kwamba chama hicho tawala kinahusika kufuta mashamba yake ili kumdhoofisha na baadaye arejee, hazina ukweli.
Alirudia hoja zake kuwa CCM ilifanya mageuzi makubwa mwaka jana yenye lengo la kuirejesha ili ifanye kazi ya wananchi.
“Tumejifunza muda mrefu, masilahi binafsi yaliturudisha nyuma sana katika kuisimamia Serikali na kuimarisha CCM. Viongozi wote walioondoka bila kujali walikaa kwa muda gani CCM, walikuwa na masilahi binafsi. Sumaye ni miongoni mwa vinara wa makundi masilahi,” alidai.
Polepole alisema CCM haimuhitaji Sumaye na hakuna dalili zozote za chama hicho kuwarudisha walioondoka na kuhamia upinzani.
Akitangaza uamuzi wa kufuta shamba la Mabwepande Novemba mwaka jana, mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi alisema alishindwa kuliendeleza.
Akieleza sababu za kufuta shamba la Sumaye la ekari 326, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mvomero, Frolent Kyombo alisema halikuendelezwa na hivyo kuwa pori lililokuwa linahatarisha maisha ya wanakijiji.

No comments:

Post a Comment