Thursday, August 10

SERIKALI YAMALIZA SINTOFAHAMU YA TANI 3,700 ZA TUMBAKU.


 SERIKALI imefanikiwa kumaliza sintofahamu ilikuwepo baina ya wakulima na wanunuzi wa tumbaku mkoani Tabora juu ya uwepo wa tani 3,700 zilizokosa soko.

Tani 3,700 zilikuwa zimekosa wanunuzi kwa sababu hazikuwa na mkataba kati ya wakulima na wanunuzi na hivyo kuhitaji utatuzi wa haraka wa Serikali ili kuinusuru tumbaku hiyo.

“Tumefanikiwa kuongea nao na tutauza zile tani 3,700 kwa wanunuzi,” alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kuamsha shangwe ukumbi mzima.

Waziri Mkuu alitoa ahadi hiyo jana jioni (Jumatano, Agosti 9, 2017) wakati akizungumza na wadau wa zao la tumbaku zaidi ya 600 wakiwemo wabunge, viongozi wa dini, chama na Serikali kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Isike-Mwanakiyungi, mjini Tabora.

Aliwashukuru wanunuzi kwa kukubali kumaliza tatizo hilo kwani litaleta ari mpya kwa wakulima na kuwafanya wajipange vizuri kwa msimu ujao. “Makampuni ya ununuzi yatapita kwenye maeneo yenu, WETCU watafuatilia na tumekubaliana nao kuwa tutafanya kazi pamoja,” alisema Waziri Mkuu.

Kufuatia sintofahamu hiyo, wiki iliyopita, wakazi wa mkoa huo waliomuomba Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli aingile kati ili kuwanusuru na adha ya zao hilo kukosa soko. Naye akawaahidi wananchi hao kwamba suala hilo atalikamilisha Waziri Mkuu.

Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bw. Aggrey Mwanri wakati akiwasilisha muhtasari wa taarifa ya mkoa huo alisema katika masoko ya tumbaku yanayoendelea, kuna tatizo la tumbaku kukosa  wanunuzi kwani hapakuwa na mkataba kati ya wakulima na wanunuzi.

“Tumbaku inayofikia kilo milioni 3.7 kwa sehemu kubwa ililimwa kwa ufadhili waWETCU Ltd, kwa fedha ambazo zilikuwa ziende APEX. WETCU walinunua pembejeo na kuwapa wakulima waliokuwa chini ya vyama sinzia, na sasa haina wanunuzi. Tunaomba ulisemee hilo ili tupate ufumbuzi wa suala hili,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni mbunge wa Urambo, Mheshimiwa Margareth Sitta aliiomba Serikali ikubali kuliangalia suala hilo la tani za ziada 3,700 kwani wakulima wamejaza tumbaku majumbani mwao na kwenye maghala.

“Wakulima wetu wanahitaji kuuza hii tumbaku ili wapate fedha za kuanzia msimu ujao wa kilimo. Lakini pia tunaomba liangaliwe suala la upangaji madaraja ya tumbaku, wasaidiwe kukabili bei isiyotabirika na kutatua ukosefu wa soko la uhakika,” alisema Mama Sitta.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, AGOSTI 10, 2017.

No comments:

Post a Comment