Tuesday, August 1

SERIKALI, WADAU KUANDAA RIPOTI YA KWANZA YA KITAIFA YA UTEKELEZAJI WA HAKI ZA WATU WENYE ULEMAVU NCHINI


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza imeanza maandalizi ya ripoti ya utekelezaji wa haki za watu wenye ulemavu tangu Tanzania kuridhiria Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye ulemavu mwaka 2009.

Katika kufanikisha suala hili, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeandaa kikao kazi kinachoshirikisha wadau wa haki za watu wenye ulemavu nchini ili kushirikiana katika maandalizi ya rasimu ya awali ya ripoti ambayo itajadiliwa,kuboreshwa na hatimaye kuwasilishwa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ikiwa ni hatua stahiki katika utekelezaji wa Mkataba wa Haki za watu wenye Ulemavu.

Kikao kazi hiki kinafanyika Mkoani Morogoro kuanzia leo tarehe 31 Julai 2017 mpaka tarehe 2 Agosti 2017 kwa lengo mahususi la kua na uelewa wa pamoja wa mfumo wa uandaaji ripoti za haki za watu wenye ulemavu wa Umoja wa Mataifa,kujadili na kutathmini utekelezaji wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu,kutoa elimu kwa wadau kuhusu usimamizi na ulinzi wa haki za watu wenye ulemavu na kuandaa rasimu ya awali ya haki za watu wenye ulemavu.

Akifungua kikao kazi hicho,Ndugu Erick Shitindi , Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Vijana,Kazi,Ajira na Watu wenye Ulemavu ameeleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 35 sehemu ya i na ii, ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu, kila nchi inapaswa kuwasilisha ripoti ya kitaifa miaka miwili mara baada ya kuridhia mkataba husika jambo ambalo Tanzania haijwahi kulitekeleza kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa fedha kwa ajili ya maandalizi ya ripoti hiyo.

“Kwa mantiki hiyo,maandalizi ya ripoti hii yamekuja wakati muafaka na itaifanya Tanzania kuingia katika historia ya kutekeleza mikataba mbalimbali ya haki za binadamu ikiwemo haki za watu wenye ulemavu na kwa ujumla nchi ilishaanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kutunga Sheria ya watu wenye ulemavu (The Persons with Disabilities Act,2010)”.anasistiza Katibu Mkuu Shitindi.

Naye Bi. Sarah Mwaipopo, Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya Katiba na Haki za Binadamu,kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kua Serikali inao wajibu kisheria kuratibu maandalizi ya ripoti na kutolea taarifa masuala mbalimbali ya utekelezaji wa haki za binadamu nchini kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 14 cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ( Section 14 of the Attorney General (Discharge of Duties) Act,2005).

Pamoja na Katiba, Sheria na Mikataba mbalimbali ya Kimataifa kutambua haki za watu wenye ulemavu, Bwana Coomaaravel Pyaneandee, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Haki za watu wenye ulemavu ya Umoja wa Mataifa aneleza kuwa zipo changamoto ambazo zimeendelea kuwepokatika usimamizi na utekelezaji wa haki za watu wenye ulemavu ambazo ni pamoja na ukosefu wa takwimu sahihi za idadi ya watu wenye ulemavu,unyanyapaa katika jamii na ngazi ya familia,kukosekana mfumo mzuri wa elimu jumuishi,asasi za kiraia kushindwa kutumia nafasi yake kufanya kazi vizuri na serikali hivyo kushindwa kupaza sauti ipasavyo,kutokua na uelewa kuhusu watu wenye ulemavu na mahitaji yao na ukosefu wa miundombinu stahiki katika sehemu mbalimbali kwa watu wenye ulemavu.

Wadau wanaoshiriki katika maandalizi ya rasimu ya awali ya ripoti ya haki za watu wenye ulemavu ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Tanzania Bara na Zanzibar,Chama cha watu wenye Ualbino Tanzania,Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Tanzania, Tume ya Uchaguzi Tanzania Bara na Zanzibar, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,Chama cha Walemavu wenye Utindio wa Ubongo,Chama cha Wazazi wenye watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi,Wizara ya Habari, Sanaa,Utamaduni na Michezo,Jeshi la Polisi Tanzania,Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii,Wizara ya Afya Zanzibar,Chama cha Watu walioumia Uti wa mgongo Tanzania,Under the Same Sun,Wizara inayoshughulikia masuala ya uwezeshaji wazee,watoto na watu wenye ulemavu Zanzibar na Chama cha Wasiiona Tanzania na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

No comments:

Post a Comment