Thursday, August 3

ROTARY DAR MARATHON KUFANYIKA KWA MARA YA TISA


Klabu saba za Rotary za Dar es salaam kwa kushirikiana na Benki M jana zimezindua mbio na matembezi ya Rotary Dar Marathon ambapo kwa mwaka huu yanafanyika kwa mara ya tisa mfululizo toka kuanzishwa kwake. Matembezi hayo yanayofanyika kila mwaka yatafanyika siku ya kumbukumbu ya kifo cha mwalimu Nyerere katika viwanja vya greens, Oystebay jijini Dar es salaam.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari hapo jana jijini, Mwenyekiti wa kamati ya maadalizi ya Rotary Dar Marathon Bi. Catherinerose Barretto alisema “tunayo furaha kuzindua na kusaini mkataba wa kushirikiana na Benki M kama mdhamini mkuu katika matembezi ya mwaka huu.

Kuna mambo mapya yameongezeka katika ushiriki wa matembezi mwaka huu, kwa mara ya kwanza tutakuwa na marathon iliyokamilika ya km 42.2, pia tutaongeza urefu wa mzunguko kwa waendesha baiskeli kutoka km 21.1 kufikia km 42.2. Matembezi ya km 9 mwaka huu yatarefushwa kufikia km 10, matembezi ya km 5 tu ndio yatabaki kama yalivyo.

Mbio na matembezi ya rotary Dar Marathon pamoja na kuwa na lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii, pia yamekuwa yakiboreshwa kila mwaka na kuvutia washiriki wengi wakiwemo wa kimataifa.

“kila mwaka tumekuwa tukiongeza vivutio katika matembezi haya. Mwaka huu tutakuwa na marathon nzima tofauti na miaka iliyopita ambapo ilikuwa ni nusu marathon”, aliendelea Barretto Mwaka huu, mbio na matembezi hayo yatalenga katika kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika hospitali ya CCBRT ambayo huhudumia wananchi wenye matatizo mbalimbali ya ulemavu ili kuwezesha hospitali hiyo kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi.

Akiongelea mipango ya wanachama wa Rotary katika kuwezesha huduma bora za afya, mwenyekiti wa bodi ya Rotary Dar Marathon Bi. Sharmila Bhatt amesema kuwa kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo wamekuwa wakichangisha fedha kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya na hatimaye wamefanikiwa kupata mradi ambao una manufaa zaidi kwa jamii hivyo fedha hizo zote zitaelekezwa katika mradi huu. “Tunayo furaha kuwa sehemu ya mradi huu ulioanzishwa na CCBRT wenye lengo la kuongeza huduma zilizo bora kwa watu wenye ulemavu mbalilmbali.

Akichangia juu ya ushiriki wa Benki M katika mbio na matembezi haya, mkurugenzi mkuu wa benki hiyo Bi. Jacqueline Woiso alisema kuwa wamekuwa wakishiriki katika shughuli mbalimbali maendeleo ya jamii, hivyo wamekuwa wakishirikiana na Rotary katika Rotary Dar marathon toka ilipoanzishwa mwaka 2009.

Aliongeza kuwa “tunasisistiza kuwa ni sera yetu kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazoheshimika katika kuleta mageuzi kwa wahitaji hapa nchini, tunaamini kabisa kuwa kwa pamoja tukishirikiana tutafanikisha ujenzi wa kituo hiki cha afya hapo CCBRT. Hii ina maana kubwa sana kwetu kuiona sekta ya afya katika jamii yetu inapewa kipaumbele, tunaamini kuwa kuweka nguvu zaidi katika sekta ya afya ni msaada wa moja kwa moja kwa jamiii ukuaji wa uchumi kwa ujumla”.

Tangu mwaka 2009 ilipoanzishwa, Rotary Dar Marathon kushirikiana na Benki M imefanikisha miradi mbalimbali ikiwemo upandaji wa miti, utoaji wa huduma ya maji safi na maji taka mashuleni pamoja na ujenzi wa wodi ya kansa ya watoto katika hospitali ya taifa ya muhimbili, wodi hii ni moja kati ya wodi bora kabisa za magonjwa ya kansa ya watoto hapa Afrika na pia mradi wa kujenga upya kituo cha kisasa cha kujifunzia katika maktaba ya chuo kikuu cha Dar es salaam.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Rotary Dar Marathon, Catherinerose Barretto (kulia) akiongea na waandishi wa habari katika hafla ya kutiliana saini mkataba wa makubaliano Dar es Salaam jana, ambapo Bank M na Rotary Clubs zitakusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika hospitali ya CCBRT mwezi wa Octoba kupitia matembezi ya Rotary Dar Marathon. Kulia kwake ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Bank M, Jacqueline Woiso, mwenyekiti wa bodi ya Rotary Dar Marathon Sharmila Bhatt na rais wa Rotary club ya Dsm aliyemaliza muda wake Nirmal Sheth.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Bank M, Jacqueline Woiso (kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya Dar Marathon Shamila Bhatt wakibadilishana mkataba wa makubaliano baada ya kutia saini katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, huku wakishuhudiwa na Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Rotary Dar Marathon, Catherinerose Barretto (kulia) , wengine ni marais wa klabu mbalimbali za Rotary.

No comments:

Post a Comment