Mwezi uliopita akiwa mjini Morogoro, Rais Magufuli aliwaagiza wafanyabiashara walionunua viwanda wakati Serikali ilipoamua kuvibinafsisha na kushindwa kuviendeleza wavirudishe serikalini akiwamo Mbunge wa Morogoro Mjini.
Jana, alirejea kauli hiyo na kumtaja waziwazi Waziri Mwijage alipokuwa akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa kiwanda kipya cha saruji cha Kilimanjaro kilichopo mjini Tanga, akielezea kushangazwa jinsi viwanda vingi vilivyobinafsishwa kwa miaka zaidi ya 20 iliyopita lakini haviendelezwa.
Alisema vipo viwanda ambavyo walipewa baadhi ya wawekezaji kwa urafiki wa viongozi waliopita hivyo akamuagiza Waziri Mwijage kuvifuta bila kuangalia sura.
“Sasa wewe waziri usiangalie sura za marafiki wa wenzako waliotangulia, wewe wakung’ute kisawasawa, hicho ndicho ninachotaka ukafanye wewe na makatibu wakuu wako. Nataka kuona kiwanda kimefutwa, hiki kimefutwa atakayejidai anakwenda mahakamani ninajua tuta-deal naye vipi najua sheria zipo.
“Waziri nakuomba nimezungumza mara nyingi, sitaki kukaa narudia hili kila siku. Si vizuri kulizungumzia hili hapa Tanga lakini napenda nizungumze, nisingezungumza ningeondoka moyo unauma, nataka muelewe.”
Alimtaka Waziri Mwijage asiogope kuvifuta viwanda vilivyokaa bila kuendelezwa akimkumbusha kuwa yeye ndiye aliyemteua.
Pia Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa kufanya tadhimini kwenye mikoa yao kubaini viwanda ambavyo vilibinafsishwa lakini vimekaa kwa muda mrefu bila kuendelezwa.
“Kama wapo wawekezaji wanaotaka kujenga viwanda nyang’anya, mtu huyu na mpe masharti ya miezi mitatu au minne naye akishindwa kuendeleza nyang’anya.’’
Katika uzinduzi huo, Rais Magufuli alitumia muda mwingi akikumbusha historia ya viwanda ya Mkoa wa Tanga akivitaja baadhi, cha Mkonge, Amboni Plastic, Nondo na Saruji.
“Tanga kulikuwa na kila aina ya viwanda, leo tujiulize vimeenda wapi? Tanga kuna reli, bandari, mawasiliano na umeme, lazima tujiulize wapi tumeshindwa? alihoji.
Jana haikuwa siku mbaya kwa Waziri Mwijage peke yake, akifungua Kiwanda cha Maziwa Tanga Fresh, Rais alieleza kushangazwa kwake na Waziri wa Kilimo, Chakula na Mifugo, Dk Charles Tizeba kutokufika katika kiwanda hicho kutatua matatizo waliyo nayo.
Rais Magufuli alisema anakifahamu vyema kiwanda hicho kwa sababu wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne alipokuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, alikuwa akikitembelea.
Akizungumza baada ya Meneja wa Tanga Fresh, Michael Karata kueleza changamoto nne zinazokikabili zikiwamo kubwa mbili; Tume ya Ushindani wa Kibiashara (FCC) kukifikisha mahakamani na kutakiwa kulipa faini ya Sh 2.8 bilioni, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuzuia hati ya biashara kutokana na kampuni iliyokiuzia bidhaa ya Azania kuwa na limbikizo la kodi na hivyo kushindwa kuendesha biashara.
Baada ya taarifa hiyo, Rais Magufuli ambaye aliweka jiwe la msingi na upanuzi wa kiwanda hicho alisema changamoto hizo zimetokana na Waziri wa Mifugo kutokitembelea na kuzifanyia kazi.
“Tanga Fresh nakijua vizuri iweje waziri, katibu mkuu na wakurugenzi wengine hawajafika? Naagiza waziri afike hapa ndani ya wiki moja na changamoto azifanyie kazi,” alisema Rais Magufuli.
Rais pia alimwagiza Waziri Mwijage kuangalia kama maziwa ya Tanzania yakizuiwa kupelekwa nje ya nchi basi na yeye azuie ya nje yasiiingie nchini.
Alisema anafahamu kuwa sekta ya maziwa imekuwa na changamoto ya kupigwa vita na masoko ya nje. Aliahidi kuvilinda viwanda vya maziwa nchini.
Aliagiza hati iliyozuiliwa na TRA ipatikane haraka ili kiwanda hicho kifanye kazi bila vikwazo kwa sababu Tanga Fresh inamilikiwa na wananchi kwa asilimia 42 huku kikipokea maziwa kutoka kwa wafugaji 6,000.
Dk Magufuli hakuishia kwa mawaziri hao tu, pia alieleza kukasirishwa kwake na kitendo cha mawaziri wa wizara zinazohusika na usimamizi wa ujenzi wa flow meter bandarini kushindwa kutoa uamuzi baada ya mwaka mmoja kupita bila kujengwa huku akisema baadhi yao ni wapumbavu.
Alisema licha ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuagiza zijengwe, mwaka umepita na mawaziri wapo.
“Mawaziri wengine ni wapumbavu, hawatoi decision (uamuzi) haraka ndiyo maana nasema ni wapumbavu,”
Awali, akimkaribisha Rais Magufuli katika uzinduzi wa Kiwanda cha Saruji cha Kilimanjaro, Waziri Mwijage alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Marten Shigella kutenga ekari 2,000 kutoka kwenye ekari 14,000 za mashamba matano yaliyofutwa na Rais Magufuli ili aweze kuwakaribisha wawekezaji kujenga viwanda.
Imeandikwa na Emmanuel Mtengwa, Burhan Yakubu na Raisa Said
No comments:
Post a Comment