Video Courtesy of MCL
Na Georgina Misama, MAELEZO
Na Georgina Misama, MAELEZO
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda na Mkurugenzi wa Uzalishaji na Vipindi wa Clouds Media Group Ruge Mutahaba wamekubaliana kumaliza tofauti zao na kuvitaka vyombo vya habari kuanza kuandika habari zinazomuhusu Mkuu wa Mkoa kama ilivyokuwa awali.
Akiongea na waandishi wa habar jijini Dar es salaam leo, Mwenyekiti wa TEF Theophil Makunga alisema kwamba wiki chache zilizopita viongozi wa jukwaa la Wahariri walikutana na Mkuu wa Mkoa ili kumsikiliza na kufikia muafaka kwa suala la Vyombo vya Habari kususia kazi zake.
“Adhabu tuliyoitoa haikuwa na muda maalum (Open ended) hivyo tusingeweza kuendelea kukaa katika mgomo huu kwani tayari muda mrefu ulishapita. Tulipoenda ofisini kwa Mkuu wa Mkoa, alitueleza mazingira yaliyopelekea yeye kufanya tukio lile Clouds na kwa pamoja tulikubaliana kuyamaliza kwani yaliyopita si ndwele sasa tugange yajayo”. Alisema Makunga.
Makunga alisema haikuwa rahisi kufikia muafaka huo, kwani walifanya majadiliano na Makonda zaidi ya mara moja hatimaye Alhamisi ya wiki iyopita walihitimisha mazungumzo yao na wote walikubaliana kufanya mkutano huu wa pamoja ili kuujulisha Umma kukoma kwa kifungo cha vyombo vya habari katika kuripoto kazi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam.
Kwa upande wake Makonda alisema kwamba waandishi wote wanafahamu upendo wake kwa vyombo vya habari, jambo ambalo kamwe halitokaa libadilike. Amekuwa tayari kukaa mezani na viongozi wa TEF kwa maslahi ya Umma kwani wote wanafanya kazi moja kwa maendeleo ya Taifa.
“Tumekubaliana na viongozi wenzangu baada ya kuja ofisini kwangu, kunisikiliza na kunihoji maswali sio chini ya masaa matatu. Mwishoni waliona hakuna haja ya kuendelea na kifungo kwa manufaa ya watanzania, pande zote mbili tumejifunza kutokana na tukio lile, na hatutegemei jambo lile kujirudia tena” Alisema Makonda
Akiongelea mahusiano yake na Mutahaba, Mkuu wa Mkoa alisema kwamba wao ni marafiki wa siku nyingi nje ya kazi, na kwa heshima ya Mhe. Rais, wamekubali kuweka tofauti zao pembeni, kusameheana na kupendana ili kuendelea kufanya kazi kwa kushirikiana kama ilivyokuwa awali.
Akitolea ufafanuzi jambo hilo, Mutahaba alisema kwamba kwake yeye anajiona kama abiria katika lori ambalo Rais ni dereva, anajua tofauti zao na Makonda zimekuwa kero kwa Mhe. Rais hivyo bila kujali kauli yoyote ya Makonda, haoni sababu ya kuendeleza tofauti zao.
“Mhe. Rais ameshasema jambo hili liishe na tuendee na kazi, sioni sababu ya kuendelea kwa heshima ya kauli yake. Kwangu mimi haijalishi kama Makonda ameomba radhi au hajaomba, lakini naona umuhimum wa kulimaliza jambo hili ili kuruhusu mambo mengine yaendelee kwa maslahi ya Taifa. Alisema Mutahaba.
Takribani miezi 5 sasa imepita toka TEF kutoa tamko la kususia kazi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es saam Paul Makonda ikiwa ni adhabu baaba ya Makonda kudaiwa kuvamia kituo cha utangazaji cha Clouds.
No comments:
Post a Comment