Monday, August 14

Mbunge atumia Sh 1.8 bilioni jimboni kwake


Mbunge wa Mbarali mkoani Mbeya, Haroon Pirmohamed ametumia Sh1.851 bilioni kutekeleza miradi minne ya maendeleo kwa wananchi wa jimbo hilo.
Mbunge huyo ambaye ni mfanyabiashara mkubwa nchini, anayetumia kauli mbiu yake ya ‘Maneno kidogo, kazi zaidi’ amesema   leo Jumatatu mjini Rujewa kuwa amedhamiria kuwasaidia wananchi wa jimbo lake wanapokwama kwenye shughuli za   maendeleo kwa kutumia rasilimali alizonazo pamoja na fedha za mfuko wa jimbo.
Alisema katika awamu ya kwanza aligawa trekta ndogo maarufu kwa jina la Powertiller   115   na kila kijiji na mtaa ilipata powertiller moja kwa ajili ya kushughulikia shughuli za maendeleo eneo husika. Wilaya ya Mbarali ina vijiji 102 na mitaa 11.
Miradi mingine aliyoitoa ni kuchimba visima 10 vya maji kwa kata saba ambavyo vimegharimu Sh129 milioni, bati 4,000  zenye thamani ya Sh84 milioni na kila kata ilipata bati 200 kwa ajili ya ujenzi  wa vyoo kwa shule za msingi na sekondari.
“Katika awamu ya nne, hivi sasa nagawa msaada wa saruji mifuko 8,475 yenye thamani ya Sh105 milioni na kila kijiji na mtaa kitapata mgawo wa mifuko 75. Hii yote kwa ajili ya kufanyia shughuli za ujenzi mbalimbali kma vile shule, zahanati  na miradi mingine inayonekana kijiji husika,”alisema mbunge huyo.
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune alipongeza juhudi anazozionesha mbunge huyo katika kuwaletea wananchi wake maendeleo, shughuli ambayo ingefanywa na Serikali.

No comments:

Post a Comment