Sunday, August 20

Masauni: Polisi, Temesa na NIT kuungana kukagua magari nchini


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu (kushoto), akimpokea Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati Mwenyekiti huyo alipofanya ziara katika ofisi hizo zilizopo Keko Mwanga, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuangalia jinsi gani Baraza lake linaweza kufanikisha Utekelezaji wa Mapendezo ya Kamati iliyoundwa na Baraza hilo ili kukabiliana ajali za barabarani nchini.  
Na Felix Mwagara (MOHA)
MWENYEKITI wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema Baraza lake litakutana kujadili uwezekano wa Jeshi la Polisi, Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) pamoja na Chuo cha Usafirishaji (NIT) ziweze kuungana ili kufanya ukaguzi wa lazima wa magari kwa lengo la kuondoa ajali nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kumaliza ziara yake ya kutembelea ofisi za Temesa na Chuo cha NIT, Masauni alisema ziara yake ilikua na mafanikio makubwa, hivyo anatarajia kukutana na Wajumbe wa Baraza lake katika vikao vyao na kuwasilisha uzoefu alioupata mara baada ya kuzitembelea Taasisi hizo za Serikali. 
“Nimeshuhudia Temesa na NIT mambo ambayo sikuyatarajia, inaonyesha kwamba katika vita ya kuzuia ajali nchini hatutaanza sifuri, tunasehemu fulani ya kuanzia, tutaanza na utaratibu wenye mfumo mzuri ambao utaweza kutekelezwa ili kufikia malengo ya kuwa na utaratibu wa lazima wa ukaguzi wa magari yote ambayo yanatumika katika nchi yetu,” alisema Masauni na kuongeza;
“Lengo la mipango hiyo ni kuhakikisha tunakuwa na magari mazuri ambayo hayawezi kusababisha ajali, hivyo nitawasilisha katika kikao hicho chha Baraza uzoefu huu nilioupata baada ya ziara hii ili nijadiliane na wajumbe wenzangu tuone jinsi tutakavyokubaliana kuhusiana na mafanikio niliyoyapata baada ya ziara hii.”
Pia alisema lengo la kuunganisha nguvu kwa kuungana kwa taasisi hizo za Serikali ni kufanikisha zaidi makabiliano ya ajali za barabarani, ambapo kwasasa Jeshi la Polisi pekee ndilo linalofanya ukaguzi wa lazima nchini, hivyo nguvu inahitajika endapo kutakua na muungano wa taasisi hizo ikiwa na lengo moja la kuijenga Tanzania.
Hata hivyo, Masauni aliongeza kuwa, katika kufanikisha hilo, kuna umuhimu wa kumtafuta mshauri mwelekezi ili afanye utafiti wa kina ili aweze kushauri jinsi ya kuvitumia vyombo na taasisi zetu zilizopo nchini, nini kifanyike ili kuweza kufikia muafaka wa namna bora ya kuweza kufanya ukaguzi wa magari wa lazima uanze  kazi haraka iwezekanavyo ili kuweza kupunguza ajali za barabarani ambazo nyingi zinasababishwa na ubovu wa magari.
Masauni akiwa Temesa alitembelea karakana ya utengenezaji wa magari na kujionea kazi mbalimbali ambazo zinafanywa na wataalamu katika karakana hiyo inayotengeneza magari ya Serikali pamoja na watu binafsi, ambapo aliona watalaamu wa Taasisi hiyo wanavyotumia vifaa mbalimbali vya matengenezo ya magari ikiwemo uwepo wa mashine ya kisasa ya kukagulia magari kwa njia ya umeme.
Alipokuwa katika Chuo cha NIT, Masauni alifanikiwa kupata taarifa fupi ya historia ya chuo hicho pamoja na kozi mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo zikiwemo za masuala ya usalama barabarani. Pia alitembelea sehemu ya kisasa ya ukaguzi wa magari chuoni hapo pamoja na madarasa ya Wahudumu wa Ndege pamoja na Marubani ambapo ni kozi ipya ya masuala ya anga inayotarajiwa kuanzishwa chuoni hapo hivi karibuni.
Aidha, Mkuu wa Chuo hicho, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Profesa Zakaria Mganilwa, alisema chuo chake kina kituo kilichofungwa mitambo ya kisasa ya kukagua magari ambapo kituo hicho kina uwezo wa kukagua magari mia sita kwa siku.
“Kama utaratibu utaweza kuwekwa wa kukagua magari, chuo kipo tayari kwasababu mitambo ipo na tumeajiri vijana ambao wanauwezo mkubwa wa kuhudumia idadi hiyo ya magari kwa siku,” alisema Mganilwa.

Masauni alimaliza ziara yake ya siku moja ambayo ilikua na lengo la kufanikisha utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati iliyoundwa na Baraza lake la Usalama Barabarani katika hatua ya kukabiliana na ajali za barabarani ambazo zinasababishwa na mambo makuu matatu, moja ni matatizo ya kibinadamu, pili matatizo ya miundombinu, na tatu ubovu wa magari au vyombo vya moto ambako ndio lengo kuu la kuunganisha taasisi hizo ili kupata nguvu zaidi katika ukaguzi wa magari nchini.

No comments:

Post a Comment