Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu, Yusufali Manji amekutwa na kesi ya kujibu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na anatarajia kuwaita mashahidi 15 kumtetea.
Ni katika kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroine.
Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi watatu wa upande wa mashtaka ameridhika kuwa mshtakiwa huyo ana haki ya kujitetea na kuita mashahidi.
Wakili wa Manji, Hudson Ndusyepo alidai kuwa mteja wake atajitetea kwa njia ya kiapo na wana mashahidi 15.
Pia aliomba hati ya wito (samasi) kwa ajili ya kuwaita mashahidi hao. Kesi imeahirishwa hadi Agosti, 30 na 31,2017 ambapo Manji atajitetea.
Awali upande wa mashtaka ulisema ungeita mashahidi wasiozidi 10 kutoa ushahidi lakini watatu ndiyo waliotoa ushahidi kwenye kesi hiyo.
Manji alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 16, 2017 akidaiwa kuwa kati ya Februari 6 na 9, 2017 katika eneo la Upanga Sea View Ilala alitumia dawa za kulevya aina ya heroin.
Baada ya kusomewa shtaka hilo Manji alikana kuwa siyo kweli 'No amekosea' na kwenye kesi hiyo anawakilishwa na Mawakili Alex Mgongolwa, Hudson Ndusyepo na Mosses Kimaro na yupo nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja ambaye alisaini bondi ya Sh 10 milioni.
No comments:
Post a Comment