Wednesday, August 16

Mahakama yatuma maombi ya mwenyekiti wa CWT


Mahakama Kuu imetupilia mbali maombi ya kufungua kesi ya kurejewa kwa kanuni za Tume ya Utumishi wa Walimu nchini yaliyoombwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Manispaa ya Dodoma, Samson Mkyota.
Katika kesi hiyo, Mkyota alikuwa akiwasilishwa na Wakili Tundu Lissu huku upande wa Serikali ukiwakilishwa na Wakili Chivanenda Luwongo.
Awali, Mkyota aliiomba mahakama kufungua kesi hiyo kwa madai kuwa kanuni za Tume ya Utumishi wa Walimu zinakiuka Sheria ya Tume ya Utumishi ya Walimu kwa kutengenezwa na  Rais Dk John Magufuli badala ya waziri mwenye dhamana.
Jaji wa Mahakama Kuu, Latifa Mansoul aliyekuwa akisikiliza maombi hayo alisema mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na pingamizi la Serikali kuwa pale ambapo kuna njia mbadala ya kukata rufaa itumike kabla ya kwenda mahakamani.
Serikali iliweka pingamizi kuwa utaratibu wa kukata rufaa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu kwa mwalimu aliyechukuliwa hatua za kinidhamu haukufuatwa.
Upande wa Serikali ulitaka muombaji kuachana na maombi hayo hadi hapo uamuzi kuhusu shauri hilo utakapokamilika kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya
Utumishi wa Walimu.
Mkyota akiwasilishwa Lissu aliomba mahakama hiyo kuruhusu kufunguliwa kwa kesi hiyo kwasababu mteja wake alisimamishwa kazi bila kupewa nafasi ya kusikilizwa na tume hiyo.
Alidai sababu nyingine ni kusimamishwa kazi kwa mteja wake ambako haukukuhusiana na shtaka linalohusiana na maslahi ya umma na kuwepo kwa upendeleo katika kufikia maamuzi hayo.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Luwongo alisema Rais ana mamlaka ya kugawa mamlaka au kubaki na hivyo kwa upande wa Tamisemi hakuyagawa kwa waziri, bali alibaki nayo mwenyewe.
Alisema kanuni hizo zilitengenezwa na waziri kama sheria inavyotaka kwa Rais kutumia mamlaka kama waziri.
Pia, alisema mlalamikaji hakuadhibiwa kama anavyodai bali alisimamishwa kazi ikiwa ni hatua mojawapo inayochukuliwa na mwajiri pale ambapo mwalimu anapokuwa ameshtakiwa kwa makosa ya kinidhamu.
Alisema hatua hiyo inaambatana na kukatwa mshahara nusu wakati utaratibu mwingine wa kikanuni ukiendelea kufanyika.
Pia Chivanenda alisema hakuna upendeleo uliofanyika katika kuchukua hatua hizo kwasababu mwalimu  anaposhtakiwa kwa makosa ya utovu wa nidhamu hatua zinazofuatwa zinajumuisha, kusikilizwa na kutoa utetezi.
Alisema pia inapoundwa kamati ya uchunguzi wa tuhuma mwalimu hupewa nafasi ya kujitetea, kuhoji, kuleta mashahidi na wakili kama ataamua hivyo.
Hata hivyo, alisema kabla ya kufikiwa hatua hizo za kusikilizwa na kujitetea, mlalamikaji alifungua kesi mahakama kuu ambayo ilisimamisha hatua zinazofuata za kikanuni.

No comments:

Post a Comment